Kikwete na ujumbe mzito

Rais Jakaya Kikwete 


Dodoma. Rais Jakaya Kikwete kesho ataambatana na ujumbe mzito wa marais wastaafu wa pande zote za Muungano, wake wa waasisi wa taifa na mawaziri wakuu wastaafu atakapokwenda kuzindua Bunge Maalumu la Katiba.

Hatua ya Rais kuambatana na ujumbe huo imepongezwa na viongozi wa vyama vikuu vya upinzani nchini, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na mwenzake wa Chadema, Freeman Mbowe.

Mbali na viongozi hao, Rais Kikwete pia ataambatana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad.

Wanaotarajiwa kuwamo katika msafara huo ni Rais wa pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, Rais wa tatu, Benjamin Mkapa na marais wastaafu wa Zanzibar, Dk Salmin Amour na Amani Abeid Karume, Mama Maria Nyerere na Mama Fatma Karume.

Miongoni mwa mawaziri wakuu wastaafu wanaotarajiwa kuwamo ni pamoja na Jaji Joseph Warioba, ambaye juzi aliwasilisha bungeni hapo Rasimu ya Katiba kwa kutoa hotuba iliyoliteka Bunge kwa jinsi alivyofafanua mambo mengi yenye utata kuhusu muundo wa Muungano.

Mawaziri wakuu wengine ni Cleopa Msuya, John Malecela, Dk Salim Ahmed Salim, Frederick Sumaye pamoja na Edward Lowassa na Mizengo Pinda ambao ni wajumbe wa bunge hilo.

Wengine walioalikwa ni mabalozi wa nchi mbalimbali, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, viongozi wa dini, vyama vya wafanyakazi, vyama vya siasa, wafugaji, wakulima, wavuvi na wawakilishi wa sekta binafsi.

Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yahaya Khamis Hamad aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Rais Kikwete atahutubia Bunge hilo kwa mujibu wa Kanuni ya 75 (1).

Rais Kikwete atapokewa katika Viwanja vya Bunge na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta na baadaye kukagua gwaride maalumu kabla ya kuhutubia Bunge kuanzia saa 10:00 jioni.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana, baada ya Rais kuhutubia saa 11:35 jioni, aliyekuwa mwenyekiti wa muda wa bunge hilo, Pandu Ameir Kificho atatoa neno la shukurani kabla ya Rais kupiga picha za kumbukumbu na wajumbe wa Bunge hilo.

Suala la hotuba ya Rais Kikwete limekuwa sehemu ya mjadala katika Bunge hilo kutokana na baadhi ya wajumbe kuhoji sababu za Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu kabla ya Rais kuzindua Bunge kwa mujibu wa kanuni.

Mjadala huo uliwafanya baadhi ya wajumbe kumzuia Jaji Warioba Jumatatu iliyopita kuwasilisha rasimu hiyo kama ilivyokuwa imepangwa hadi kilipofanyika kikao cha maridhiano siku hiyohiyo usiku na kufikia mwafaka kwamba Mwenyekiti huyo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba awasilishe Rasimu juzi na Rais ahutubie kesh

Lipumba, Mbowe na Mtatiro

Akizungumzia ujumbe huo, Profesa Lipumba alisema hiyo inaonyesha jinsi mkuu huyo wa nchi alivyolipa uzito bunge hilo.

Profesa Lipumba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ulioundwa na baadhi ya wajumbe wa bunge hilo alisema ni jambo jema kwa Rais kulizindua Bunge hilo kwa kuwa ndiye mwasisi wa mchakato wa Katiba Mpya... “Ujio wake utasherehesha Bunge hili na nasaha zake zitatusaidia.”

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni alisema tendo la kuandika Katiba ni kubwa na linalohusu wananchi wote hivyo ni dhahiri kuwa marais wastaafu na wake wa waasisi wa Muungano wana fursa ya kipekee kuhudhuria uzinduzi huo.

“Nina hakika wapo viongozi wengine walioalikwa. Kwa msingi huu, sina tatizo na ushiriki au ualikwa wao kwani bado wana heshima katika jamii kama viongozi wastaafu,” alisema na kuongeza:

“Ni matumaini yangu kuwa hotuba ya Rais itasaidia kupunguza hofu na hisia hasa kwa makundi yanayohasimiana katika Bunge hili na siyo kuongeza hofu na ufa.”

Alisema wapo viongozi wa Bunge ambao wamekuwa wakiwaona baadhi ya viongozi kama ni wafanya fujo... “Bunge la Katiba ni tofauti na Bunge la kawaida na linahitaji kuvumiliana na kustahimiliana sana wanachokitazama kama fujo kwa wengine ni staili muhimu ya kudai kusikilizwa. Walichokiona kama fujo kimesaidia wabunge wote na hata Watanzania kusikia kwa kina taarifa ya mheshimiwa Warioba. Fujo zile ndizo zilizozaa saa nne alizopewa mheshimiwa Warioba na timu yake na kuleta utulivu mkubwa katika nchi.”

Alisema kilichoonekana kama rabsha na fujo kwa Rais wakati alipozindua Bunge la 10 ndicho kilichozaa mchakato huu wa Katiba. Katika Bunge hilo, wapinzani walisusia hotuba ya Rais Kikwete ambayo pamoja na mambo mengine, alitangaza kuanza kwa mchakato wa Katiba Mpya.

Mjumbe wa Bunge hilo, Julius Mtatiro alisema anatarajia Rais atasisitiza umuhimu wa maridhiano, maelewano, kuheshimiana baina ya wajumbe na kuwataka watilie maanani masilahi ya taifa badala ya kundi mojamoja au vyama.

No comments:

Post a Comment