Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta (kushoto) akimsikiliza Rais
wa Shirikisho la Wasanii Tanzania (Taff), Simon Mwakifwamba (kulia)
wakati wasanii walipokutana na uongozi wa Bunge hilo mjini Dodoma jana
na kujadili mambo ya wasanii yanayopaswa kuwamo katika Katiba Mpya.
Picha na Emmanuel Herman
Dodoma. Kitendo cha Bunge
Maalumu la Katiba kukusanya maoni ya makundi na wananchi mbalimbali,
kimepokewa kwa hisia tofauti, baadhi ya wasomi wakisema ni kinyume cha
sheria na kuonyesha kutapatapa huku Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba akisema linafanya kazi ambayo
tayari tume yake ilishaifanya.
Hata hivyo, Katibu wa Bunge hilo, Yahya Khamis
Hamad amesema litaendelea kupokea mapendekezo kutoka kwa watu na makundi
mbalimbali hadi hapo litakapohitimisha kazi yake.
Kwa muda sasa, wawakilishi wa taasisi mbalimbali
wamekuwa wakifika Dodoma kuwasilisha mapendekezo yao wakitaka
yazingatiwe kwenye Katiba Mpya kwa maelezo ya kutoonekana katika rasimu
ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Suala hilo limezua mjadala hasa katika mitandao ya
kijamii ambako watu mbalimbali wamekuwa wakihoji sababu za Bunge hilo
kufanya kile kinachotafsiriwa kuwa ni ‘kukusanya maoni’, kazi ambayo
tayari ilishafanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Akitetea hoja hiyo, Hamad alitetea akisema
wananchi, watu au taasisi zinazotoa mapendekezo yao zinashirikiana na
wabunge katika mchakato wa kile kinachoendelea bungeni hivi sasa.
“Tutaendelea kupokea maoni ya wananchi kwa sababu
na sisi tunaendelea kujadili, kwa hiyo kadri makundi yatakavyoleta maoni
yao, tutayapokea na kuyapitisha kwenye mchakato wa kuyawezesha
kuzingatiwa kama yataonekana yanafaa,” alisema Hamad.
Warioba na wasomi
Akizungumzia hatua hiyo, Jaji Warioba aliponda
kitendo cha kukusanywa upya kwa maoni hayo akisema yalishachukuliwa na
Tume yake na kuingizwa katika Rasimu ya Katiba.
“Nyaraka zote za maoni, yakiwamo ya makundi hayo
tuliziwasilisha, sasa wanakusanya maoni mapya ili iweje? Wanatakiwa
kufuata maoni ya wananchi na si ya makundi na kama wanafanya hivyo basi
maoni ya makundi hayo yakusanywe hadharani ili wananchi wayasikie ili
nao waweze kuchangia,” alisema jana.
Alitolea mfano wa maoni yaliyotolewa na Jumuiya ya
Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT), kwamba ni makosa kuchukua maoni hayo
na kuyaacha yaliyotolewa nawananchi.
“Naona kuhusu ardhi eti wamechukua maoni ya Wizara
ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, hii si sahihi kabisa. Kama wanajadili
suala la serikali za mitaa, ardhi na maliasili wanatakiwa kuyaongeza
mambo hayo katika mambo ya muungano kwa sababu hivi sasa mambo hayo si
ya muungano na ndiyo maana Tume hatukuyaingiza katika Rasimu ya Katiba,”
alisema.
Jaji Warioba alilitaka Bunge hilo kutochakachua maoni kuhusu
ardhi, maliasili na ardhi ambayo Tume yake iliyawasilisha serikalini ili
baadaye yaingizwe katika Katiba ya Tanganyika, “Wakiyaingiza mambo hayo
katika Katiba ya Muungano, yatapingana na Katiba ya Zanzibar na kuleta
shida.”
Mtaalamu wa lugha na falsafa, Faraja Christoms
alisema, “Kinachofanyika Dodoma ni dalili ya kutapatapa. Wanatakiwa
kukumbushwa kuwa wanachokifanya si sahihi na ni kinyume na sheria,
kifupi ni kwamba Bunge la Katiba limepoteza mwelekeo.”
Mhadhiri wa Idara ya Sayansi za kwenye Maji na
Uvuvi Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM),Dk Charles Lugomela alisema:
“Bunge limekosa mwelekeo kwa sababu Katiba ni suala la maridhiano ya
kisiasa na linatakiwa kuendeshwa kwa nguvu ya hoja na si hoja ya nguvu.”
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata),
Deus Kibamba alisema Bunge hilo sasa linakwenda mwendo wa gari bovu,
huku akimtuhumu Mwenyekiti wake, Samuel Sitta kuwa analiendesha kwa
mtindo wa comedy (vichekesho) na si kufuata kanuni na sheria.
“Ndiyo maana tulimtaka Sitta aliahirishe Bunge kwa
sababu anaweza kwa mujibu wa Kifungu cha 28(4) ambacho walikibadili na
kujipa mamlaka ya kulifanya Bunge hilo kuendelea mpaka pale
itakapoonekana inafaa,” alisema Kibamba.
Mtaalamu wa lugha ya Kiswahili, Dk Aldin Mutembei
alisema: “Kinachofanyika Dodoma ni makosa na wajumbe wanafanya mambo
ambayo hayakutakiwa kufanyika, kifupi ni kwamba wanakwenda kinyume na
utaratibu.”
Mutembei alisema kitendo hicho kinastaajabisha na
ni matokeo ya kutofuatwa kwa sheria zilizozalisha Bunge hilo na mchakato
wote wa kuandika Katiba Mpya.
Maoni ya Takukuru
Miongoni mwa makundi yaliyowasilisha maoni ni
Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru) ambayo imependekeza
kuanzishwa kwa divisheni katika Mahakama Kuu ya Tanzania itakayokuwa na
wajibu wa kusikiliza kesi zote zinazopelelezwa na kufikishwa mahakamani
na taasisi hiyo.
Pia, inashauri kuanzishwa kwa ‘Taasisi ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi’ ambayo itakuwa moja ya taasisi
za uwajibikaji zinazotajwa katika sura ya 13 ya Rasimu ya Katiba.
Katika Rasimu iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Takukuru haikutajwa kwani ilipaswa kuwa kwenye Katiba ya Tanganyika.
Mapendekezo ya Takukuru ni miongoni mwa mengine saba ambayo
uongozi wa Bunge Maalumu umeyapeleka katika kamati zote 12 ili kubaini
iwapo yanafaa kuingizwa kwenye Rasimu ya Katiba kabla ya kamati hizo
kuwasilisha taarifa zake za uchambuzi bungeni kuanzia wiki ijayo.
“Si kwamba yote ni sura mpya, mengine ni nyongeza
katika ibara sura zilizopo kwenye Rasimu ya Katiba, kwa hiyo kwa sababu
wajumbe walishafanya uchambuzi wa sura zote, itakuwa rahisi kwao kujua
wapi waingize kipi,” alisema Hamad.
Mapendekezo mengine
Mapendekezo mengine yaliyofanyiwa uchambuzi ni
yale yanayohusu muundo wa serikali ambayo yamewasilishwa na mwanasheria
na mwalimu, Onesmo Kyauke ambaye katika mapendekezo yake, ametaka muundo
wa muungano usizingatie idadi ya Serikali, bali mgawanyo wa madaraka wa
nguzo tatu za dola ambazo ni Mahakama, Bunge na Serikali.
Pia yapo mapendekezo yanayohusu masuala ya ardhi,
mazingira na rasilimali za Taifa, kutoka Tume ya Mabadiliko ya Katiba
ambayo ni mapya kwani hayamo kwenye rasimu ya sasa.
Taasisi nyingine zilizowasilisha mapendekezo ya
sura inayohusu masuala ya ardhi, mazingira na rasilimali za Taifa ni
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, pamoja na wajumbe wa
Bunge Maalumu wanaotetea wakulima, wafugaji na wavuvi.
Pendekezo jingine ni lile la sura mpya ya Serikali
za Mitaa na ugatuaji wa madaraka kwa wananchi yaliyowasilishwa na Tume
ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na Alat.
Pia yapo mapendekezo kuhusu haki za wakulima
kutoka Chama cha Wakulima wa Pamba Tanzania (TACOGA), ambayo uongozi wa
Bunge umeelekeza yajadiliwe pamoja na yale yanayohusu ardhi bila kusahau
mapendekezo ya Shirikisho la Wasanii (Taff).