Bunge lajigeuza Tume ya Warioba

Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta (kushoto) akimsikiliza Rais wa Shirikisho la Wasanii Tanzania (Taff), Simon Mwakifwamba (kulia) wakati wasanii walipokutana na uongozi wa Bunge hilo mjini Dodoma jana na kujadili mambo ya wasanii yanayopaswa kuwamo katika Katiba Mpya. Picha na Emmanuel Herman 



Dodoma. Kitendo cha Bunge Maalumu la Katiba kukusanya maoni ya makundi na wananchi mbalimbali, kimepokewa kwa hisia tofauti, baadhi ya wasomi wakisema ni kinyume cha sheria na kuonyesha kutapatapa huku Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba akisema linafanya kazi ambayo tayari tume yake ilishaifanya.

Hata hivyo, Katibu wa Bunge hilo, Yahya Khamis Hamad amesema litaendelea kupokea mapendekezo kutoka kwa watu na makundi mbalimbali hadi hapo litakapohitimisha kazi yake.

Kwa muda sasa, wawakilishi wa taasisi mbalimbali wamekuwa wakifika Dodoma kuwasilisha mapendekezo yao wakitaka yazingatiwe kwenye Katiba Mpya kwa maelezo ya kutoonekana katika rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Suala hilo limezua mjadala hasa katika mitandao ya kijamii ambako watu mbalimbali wamekuwa wakihoji sababu za Bunge hilo kufanya kile kinachotafsiriwa kuwa ni ‘kukusanya maoni’, kazi ambayo tayari ilishafanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Akitetea hoja hiyo, Hamad alitetea akisema wananchi, watu au taasisi zinazotoa mapendekezo yao zinashirikiana na wabunge katika mchakato wa kile kinachoendelea bungeni hivi sasa.

“Tutaendelea kupokea maoni ya wananchi kwa sababu na sisi tunaendelea kujadili, kwa hiyo kadri makundi yatakavyoleta maoni yao, tutayapokea na kuyapitisha kwenye mchakato wa kuyawezesha kuzingatiwa kama yataonekana yanafaa,” alisema Hamad.

Warioba na wasomi

Akizungumzia hatua hiyo, Jaji Warioba aliponda kitendo cha kukusanywa upya kwa maoni hayo akisema yalishachukuliwa na Tume yake na kuingizwa katika Rasimu ya Katiba.

“Nyaraka zote za maoni, yakiwamo ya makundi hayo tuliziwasilisha, sasa wanakusanya maoni mapya ili iweje? Wanatakiwa kufuata maoni ya wananchi na si ya makundi na kama wanafanya hivyo basi maoni ya makundi hayo yakusanywe hadharani ili wananchi wayasikie ili nao waweze kuchangia,” alisema jana.

Alitolea mfano wa maoni yaliyotolewa na Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT), kwamba ni makosa kuchukua maoni hayo na kuyaacha yaliyotolewa nawananchi.

“Naona kuhusu ardhi eti wamechukua maoni ya Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, hii si sahihi kabisa. Kama wanajadili suala la serikali za mitaa, ardhi na maliasili wanatakiwa kuyaongeza mambo hayo katika mambo ya muungano kwa sababu hivi sasa mambo hayo si ya muungano na ndiyo maana Tume hatukuyaingiza katika Rasimu ya Katiba,” alisema.

Jaji Warioba alilitaka Bunge hilo kutochakachua maoni kuhusu ardhi, maliasili na ardhi ambayo Tume yake iliyawasilisha serikalini ili baadaye yaingizwe katika Katiba ya Tanganyika, “Wakiyaingiza mambo hayo katika Katiba ya Muungano, yatapingana na Katiba ya Zanzibar na kuleta shida.”

Mtaalamu wa lugha na falsafa, Faraja Christoms alisema, “Kinachofanyika Dodoma ni dalili ya kutapatapa. Wanatakiwa kukumbushwa kuwa wanachokifanya si sahihi na ni kinyume na sheria, kifupi ni kwamba Bunge la Katiba limepoteza mwelekeo.”

Mhadhiri wa Idara ya Sayansi za kwenye Maji na Uvuvi Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM),Dk Charles Lugomela alisema: “Bunge limekosa mwelekeo kwa sababu Katiba ni suala la maridhiano ya kisiasa na linatakiwa kuendeshwa kwa nguvu ya hoja na si hoja ya nguvu.”

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba alisema Bunge hilo sasa linakwenda mwendo wa gari bovu, huku akimtuhumu Mwenyekiti wake, Samuel Sitta kuwa analiendesha kwa mtindo wa comedy (vichekesho) na si kufuata kanuni na sheria.

“Ndiyo maana tulimtaka Sitta aliahirishe Bunge kwa sababu anaweza kwa mujibu wa Kifungu cha 28(4) ambacho walikibadili na kujipa mamlaka ya kulifanya Bunge hilo kuendelea mpaka pale itakapoonekana inafaa,” alisema Kibamba.

Mtaalamu wa lugha ya Kiswahili, Dk Aldin Mutembei alisema: “Kinachofanyika Dodoma ni makosa na wajumbe wanafanya mambo ambayo hayakutakiwa kufanyika, kifupi ni kwamba wanakwenda kinyume na utaratibu.”

Mutembei alisema kitendo hicho kinastaajabisha na ni matokeo ya kutofuatwa kwa sheria zilizozalisha Bunge hilo na mchakato wote wa kuandika Katiba Mpya.

Maoni ya Takukuru

Miongoni mwa makundi yaliyowasilisha maoni ni Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru) ambayo imependekeza kuanzishwa kwa divisheni katika Mahakama Kuu ya Tanzania itakayokuwa na wajibu wa kusikiliza kesi zote zinazopelelezwa na kufikishwa mahakamani na taasisi hiyo.

Pia, inashauri kuanzishwa kwa ‘Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi’ ambayo itakuwa moja ya taasisi za uwajibikaji zinazotajwa katika sura ya 13 ya Rasimu ya Katiba.

Katika Rasimu iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Takukuru haikutajwa kwani ilipaswa kuwa kwenye Katiba ya Tanganyika.

 

Mapendekezo ya Takukuru ni miongoni mwa mengine saba ambayo uongozi wa Bunge Maalumu umeyapeleka katika kamati zote 12 ili kubaini iwapo yanafaa kuingizwa kwenye Rasimu ya Katiba kabla ya kamati hizo kuwasilisha taarifa zake za uchambuzi bungeni kuanzia wiki ijayo.

“Si kwamba yote ni sura mpya, mengine ni nyongeza katika ibara sura zilizopo kwenye Rasimu ya Katiba, kwa hiyo kwa sababu wajumbe walishafanya uchambuzi wa sura zote, itakuwa rahisi kwao kujua wapi waingize kipi,” alisema Hamad.

Mapendekezo mengine

Mapendekezo mengine yaliyofanyiwa uchambuzi ni yale yanayohusu muundo wa serikali ambayo yamewasilishwa na mwanasheria na mwalimu, Onesmo Kyauke ambaye katika mapendekezo yake, ametaka muundo wa muungano usizingatie idadi ya Serikali, bali mgawanyo wa madaraka wa nguzo tatu za dola ambazo ni Mahakama, Bunge na Serikali.

Pia yapo mapendekezo yanayohusu masuala ya ardhi, mazingira na rasilimali za Taifa, kutoka Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ni mapya kwani hayamo kwenye rasimu ya sasa.

Taasisi nyingine zilizowasilisha mapendekezo ya sura inayohusu masuala ya ardhi, mazingira na rasilimali za Taifa ni Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, pamoja na wajumbe wa Bunge Maalumu wanaotetea wakulima, wafugaji na wavuvi.

Pendekezo jingine ni lile la sura mpya ya Serikali za Mitaa na ugatuaji wa madaraka kwa wananchi yaliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na Alat.

Pia yapo mapendekezo kuhusu haki za wakulima kutoka Chama cha Wakulima wa Pamba Tanzania (TACOGA), ambayo uongozi wa Bunge umeelekeza yajadiliwe pamoja na yale yanayohusu ardhi bila kusahau mapendekezo ya Shirikisho la Wasanii (Taff).

No comments:

Post a Comment