Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa akiwa amebebwa na
madereva bodaboda kabla ya kuanza kwa mkutano wake na waendesha vyombo
hivyo vya usafiri uliofanyika mjini humo jana. Picha na Geofrey
Nyang’oro
Na Geofrey Nyang’oro na Berdina Majinge, Mwananchi
Iringa. Jeshi la Polisi
limelazimika kutumia nguvu ikiwamo kupiga risasi za moto hewani ili
kutuliza vurugu zilizoibuka katika eneo la mkutano ulioitishwa na Mbunge
wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.
Katika mkutano huo, mbunge huyo alikuwa na lengo
la kuzungumza na waendesha pikipiki maarufu bodaboda pamoja na
kusikiliza kero zao.
Hata hivyo, wakati Mchungaji Msigwa akiwa
ameitisha mkutano huo, Mwenyekiti wa Chama cha Madereva Bodaboda (CMB)
Manispaa ya Iringa, Joseph Mwambopa aliitisha mwingine kwa wanachama
wake muda huo huo katika Viwanja vya Mwembetogwa.
Hali hiyo ilielezwa kama njia ya kuleta vurugu
ingawa waendesha bodaboda wengi walihudhuria mkutano ulioandaliwa na
mbunge huku idadi ndogo ikihudhuria kwa Mwambopa aliyekuwa na msimamo
tofauti.
Kuanza kwa vurugu
Vurugu hizo zilianza muda mfupi baada ya Mwambopa
na watu waliokuwa wakimuunga mkono kuwasili katika mkutano wa Mchungaji
Msigwa na kushinikiza kuingia kwa nguvu.
Baadhi ya washiriki walipinga hatua ya kiongozi
huyo wa waendesha bodaboda kuingia kwa madai kwamba hawamtaki kutokana
na kitendo chake cha kuwakataza wanachama wake kutoshiriki mkutano huo.
Hatua hiyo iliibua mzozo na kusukumana jambo
lililosababisha polisi kufika eneo hilo na kupiga risasi za moto hewani
ili kutuliza ghasia na hatimaye kumkamata Mwambopa na kuondoka naye.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Msigwa aliwataka
vijana wakiwamo waendesha bodaboda kuepuka kutumiwa na wanasiasa kama
daraja la kufikia malengo yao. “Uongozi ni zaidi ya misaada, kiongozi
anapaswa kuwaonyesha watu njia ya kufikia mafanikio,”alisema Msigwa.
Pia aliwashauri waendesha bodaboda kuanzisha chama kingine kama wanaona kuna sababu ya kufanya hivyo.
No comments:
Post a Comment