Shy-Rose adaiwa kumpiga mbunge mwenzake Nairobi

 

Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Shy-Rose Bhanji.

Na Nuzulack Dausen, Mwananchi


Dar es Salaam. Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Shy-Rose Bhanji ameingia katika mgogoro mpya baada ya kutuhumiwa kumpiga mbunge mwenzake kutoka Tanzania, Dk Nderakindo Kessy jijini Nairobi, Kenya.

Bhanji, ambaye amekuwa katika mgogoro na wabunge wenzake kwa kipindi cha miezi miwili sasa, anadaiwa kumvamia Dk Kessy na kumpiga mgongoni. Akizungumza kwa simu kutoka Nairobi, Dk Kessy alisema tukio hilo lilitokea bungeni juzi jioni baada ya kikao kuahirishawa.

“Kwa kuwa muda wa Bunge ulikuwa umeisha nisingeweza kuipeleka kesi hiyo bungeni badala yake ikawa shambulizi na niliambiwa kiutaratibu nikaripoti Kituo cha Polisi cha Bunge ambako baadaye nilikwenda na kupatiwa cheti cha matibabu,” alisema Dk Kessy.

Alisema baada ya kupatiwa cheti cha matibabu na polisi alikwenda katika Hospitali ya AAR jijini humo ambako alipimwa na kupewa majibu aliyoyapeleka polisi kwa uchunguzi.

Hadi tukio hilo linatokea, alisema hakuwa amekwaruzana na Bhanji zaidi ya kushangaa akimvamiwa.

“Baada ya kunipiga hakukuwa na madhara ya papo kwa papo kama alama yoyote mwilini au damu ila nayasikia maumivu, sijui hapo baadaye,” alisema Mbunge huyo ambaye ni kada wa NCCR-Mageuzi.

Bhanji hakupatikana jana kuzungumzia tuhuma hizo, kwani simu yake ilikuwa imezimwa na hata ujumbe wa barua pepe alioandikiwa hakurudisha majibu. Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa Eala, Bobi Odiko alisema: “Nimesikia kwamba mmoja ya wabunge alimpiga mwenzake ‘kipepsi’ lakini ilikuwa nje ya Bunge, bado ninaendelea kutafuta ukweli wa kina juu ya tukio hilo.”

Bunge la Eala, tangu mwanzoni mwa mwaka huu, limekuwa likitawaliwa na vioja na mivutano ya hapa na pale na mikakati ya kumng’oa Spika Magreth Zziwa kwa madai ya kutofanya kazi kwa weledi.

Hivi karibuni, Bhanji aliliingiza Bunge hilo katika mvutano baada ya kudaiwa kuliaibisha wakati wa ziara ya Ubelgiji iliyowashirikisha wajumbe wa tume na wenyeviti wa kamati za Bunge hilo.

Alituhumiwa kufanya fujo ndani ya ndege kwa kutoa lugha chafu kwa wabunge wenzake na matamshi yasiyo ya staha katika hafla iliyoandaliwa na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Dk Diodorus Kamala.

Baada ya tukio hilo, baadhi ya wabunge walitaka Bhanji achukuliwe hatua za kinidhamu.

Hali hiyo ilifanya vikao vilivyokuwa vikifanyika jijini Kigali, Rwanda mwezi uliopita kuahirishwa kila baada ya dakika 20 au 30 kutokana na wabunge kutumia kanuni ya 31 kutoa hoja zao kutaka mjadala kuhusu Bhanji ufanyike kwanza kabla ya kuendelea na kazi nyingine.

 

Bhanji alikanusha tuhuma zote na kuziita uzushi na zenye nia ya kuzimisha juhudi zake za kupinga njama ovu za kumng’oa Spika Zziwa.

Kabla ya Bunge hilo kuanza Nairobi Novemba 14, Bhanji aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook: “Kwa Tanzania kuna sahihi mbili tu… lengo kubwa la kumwondoa Spika ni sehemu ya ‘mchezo mchafu ili kikundi fulani’ wamuweke Spika mwingine kwa masilahi ya wachache.”

Hata hivyo, bado haijabainika wazi iwapo hatua ya kumvaa Dk Kessy ilikuwa ni sehemu ya mvutano huo kwani Dk Kessy alisema hajui chanzo.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema wamepata taarifa za tukio hilo na wamezipa umuhimu mkubwa na kimeshafikisha malalamiko rasmi kwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.

Mwenyekiti wa wabunge wa Tanzania ndani ya Eala, Adam Kimbisa alisema hakuwa ameambiwa chochote juu ya tukio hilo... “Nipo kwenye kikao. Sijaambiwa chochote.” Alipoulizwa iwapo alikuwa na taarifa za awali juu ya tukio hilo alisema: “Sina uhakika na habari hizo.”

Waziri Sitta alikiri kusikia tukio hilo na kubainisha kuwa lilitokea kwa bahati mbaya wakati Bhanji anapita katika kundi la wabunge na kumgonga Dk Kessy na kwa kuwa alikuwa na haraka hakuweza kusimama.

Alisema Kwa kuwa Dk Kessy hakupata maumivu makali wabunge hao jana asubuhi walikaa pamoja na kuelewana.

Aliongeza kuwa taarifa rasmi kutoka kwa naibu wake, Dk Abdallah Sadala aliyepo Nairobi, ni kwamba baada ya maelewano hayo Sajenti wa Bunge alikwenda kituoni hapo kueleza kwamba Bhanji hakufanya kitendo hicho kwa makusudi na walikuwa wamemalizana.

Mwanza kwachafuka tena

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola.

Na Aidan Mhando, Mwananchi

Mwanza. Shughuli za wakazi na wafanyabiashara wa Soko Kuu na Mtaa wa Makoroboi jijini Mwanza jana zilisimama kwa zaidi ya saa nne baada ya kuibuka vurugu kati ya Wamachinga na polisi na kusababisha maduka katika maeneo hayo kufungwa.

Vurugu hizo ziliibuka saa sita mchana na kusababisha polisi waliokuwa kwenye magari manne aina ya Land Rover Defender na Toyota Land Cruiser kurusha mabomu ya machozi kuwatawanya wafanyabiashara waliokuwa wakijibu mapigo kwa kuwarushia mawe.

Hali hiyo ilisababisha magari yaliyokuwa yameegeshwa pembeni mwa Barabara ya Nyerere kuvunjwa vioo pia madirisha ya Msikiti wa Singasinga na ya nyumba kadhaa za Mtaa wa Makoroboi pia yalivunjwa vioo. Zaidi ya Wamachinga 50 walikamatwa na polisi ingawa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola alisema ni mapema kutaja idadi.

Kwa mujibu wa polisi, chanzo cha vurugu hizo ni baadhi ya wafanyabiashara walioondolewa Mtaa wa Makoroboi karibu na Msikiti wa Singasinga, kurejea hivyo kuondolewa kwa nguvu.

Mwandishi wa habari hii alishuhudia mamia ya wakazi wa Jiji la Mwanza katika barabara za Pamba, Nyerere na Kituo cha Sokoni wakiwa wakikimbia huku na kule kutokana na mabomu ya machozi yaliyokuwa yakirushwa. Moja ya mabomu hayo yaliangukia katika jengo la Benki ya Access na kusababisha wafanyakazi wake kutoka nje.

Kamanda Mlowola alisema operesheni hiyo ni ya kawaida na kwamba wamefanya hivyo kuondoa wafanyabiashara waliorejea maeneo wasiyotakiwa.

Wapinzani wamsulubu Mwakyembe bungeni


 Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe

Dodoma. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, jana ilimsulubu Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ikieleza kuwa wizara yake iliingia mkataba wa mradi wa treni za kisasa kutoka Stesheni ya Dar es Salaam hadi Pugu kupitia Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) bila kufuata taratibu.
Kambi hiyo ililieleza Bunge kuwa mkataba huo ulisainiwa baina ya mmiliki wa Kampuni ya M/s Shumoja, Robert Shumake na Shirika la Reli Tanzania huku Waziri Mwakyembe akishuhudia.
Msemaji Mkuu wa kambi hiyo, Ofisi ya Waziri Mkuu,  Uwekezaji na Uwezeshaji, Pauline Gekul alitoa madai hayo wakati akiwasilisha maoni ya kambi hiyo kuhusu muswada wa marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP).
Gekul alisema taratibu hazikufuatwa kwa kuwa haieleweki ni lini Serikali, wakala au Wizara ya Uchukuzi ilitangaza zabuni ya mradi wa treni kutoka Stesheni hadi Pugu kupitia JNIA.
“Pia haijulikani ni lini Serikali ilifanya upembuzi yakinifu kuhusu mradi huo wa reli kwa kufuata taratibu kama zinavyoainishwa na Sheria ya PPP ya mwaka 2010 ambayo inafanyiwa marekebisho hivi sasa,” alisema Gekul na kuongeza: “Haijulikani ni kampuni ngapi ambazo ziliomba tenda ya ukandarasi wa treni na kwamba M/s Shumoja ilishinda tenda hiyo kwa vigezo gani.”
Alisema kwa kifupi ni wazi kuwa Dk Mwakyembe na wizara yake walikiuka vifungu vya Sheria ya PPP. Alivitaja vifungu hivyo kuwa ni 4(1) na (2) vinavyomtaka waziri kutangaza katika Gazeti la Serikali miradi mbalimbali inayotegemewa kufanywa na sekta ya umma kwa ubia na sekta binafsi.
Gekul alisema pia kifungu cha 5(1) kilikiukwa ambacho kinaitaka mamlaka inayohusika kufanya upembuzi yakinifu baada ya kupembua mradi ambao utafanywa kwa ubia.
“Pia kifungu cha 9 kinachotaka mzabuni kutoa nyaraka mbalimbali za miradi ikiwamo jina, mahesabu yaliyofanyiwa ukaguzi pamoja na vielelezo vya uwezo wa kifedha,” alisema Gekul.
Alihoji kulikuwa na uharaka gani wa utekelezaji wa mradi huo ambao umekiuka Sheria ya PPP bila kuwahusisha wadau wengine ambao wangeweza pia kushindana na Shumoja?
“Ingekuwa ni vyema kama Serikali ingeweka bayana undani wa mkataba wa mradi huo ambao kama Watanzania hatujawahi kusikia ukitangazwa ili kutoa fursa kwa wazabuni wenye uwezo kushindania zabuni hiyo zaidi ya kuona na kuusikia mradi siku ya utiaji saini,” alisema.
Alisema Serikali ikishabanwa kutoa majibu juu ya uvunjwaji wa sheria, huja na majibu ya kejeli, hivyo Watanzania waelewe kuwa sheria zimekuwa zikipindishwa ili kupitisha miradi ambayo baadaye hugeuka kuwa mzigo kwao kama ilivyokuwa IPTL na Escrow.
Alisema pamoja na adha ya usafiri jijini Dar es Salaam, ukweli utabaki palepale kwamba, Dk Mwakyembe alisimamia mchakato wa mradi uliokiuka sheria ambao ikiwa utashindikana katika utekelezaji na mzigo wa uvunjwaji ama usitishwaji wa mkataba, gharama zitarudi kwa Watanzania.

Muswada

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Mary Nagu aliwasilisha bungeni muswada wa marekebisho ya Sheria ya Ubia baina ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma wa mwaka 2014 ukiwa na madhumuni ya kufanya marekebisho katika sheria mbalimbali.

Nagu alisema mabadiliko hayo ni katika Sheria ya Ubia baina ya sekta ya umma na binafsi ili kuweka mazingira bora zaidi ya kubainisha na kutekeleza miradi ya ubia baina ya sekta hizo.

“Mabadiliko hayo yataongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya ubia nchini na yatawezesha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika kuwekeza kwenye miradi ya kiuchumi na huduma za jamii,” alisema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, Luhaga Mpina alitaka Serikali iweke mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji nchini ili sekta iongeze ushiriki wake katika miradi ya maendeleo.

Alisema kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa mitaji, kwani Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) haina mtaji wa kutosha kuhudumia sekta binafsi.

Mpina alisema madeni ya sekta binafsi kwa sasa yamefikia Sh1.3 trilioni huku madeni ya Mifuko ya Jamii yakifikia Sh8 trilioni.