Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola.
Na Aidan Mhando, Mwananchi
Mwanza. Shughuli za wakazi na
wafanyabiashara wa Soko Kuu na Mtaa wa Makoroboi jijini Mwanza jana
zilisimama kwa zaidi ya saa nne baada ya kuibuka vurugu kati ya
Wamachinga na polisi na kusababisha maduka katika maeneo hayo kufungwa.
Vurugu hizo ziliibuka saa sita mchana na kusababisha polisi waliokuwa kwenye magari manne aina ya Land Rover Defender na Toyota Land Cruiser kurusha mabomu ya machozi kuwatawanya wafanyabiashara waliokuwa wakijibu mapigo kwa kuwarushia mawe.
Hali hiyo ilisababisha magari yaliyokuwa
yameegeshwa pembeni mwa Barabara ya Nyerere kuvunjwa vioo pia madirisha
ya Msikiti wa Singasinga na ya nyumba kadhaa za Mtaa wa Makoroboi pia
yalivunjwa vioo. Zaidi ya Wamachinga 50 walikamatwa na polisi ingawa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola alisema ni mapema
kutaja idadi.
Kwa mujibu wa polisi, chanzo cha vurugu hizo ni
baadhi ya wafanyabiashara walioondolewa Mtaa wa Makoroboi karibu na
Msikiti wa Singasinga, kurejea hivyo kuondolewa kwa nguvu.
Mwandishi wa habari
hii alishuhudia mamia ya wakazi wa Jiji la Mwanza katika barabara za
Pamba, Nyerere na Kituo cha Sokoni wakiwa wakikimbia huku na kule
kutokana na mabomu ya machozi yaliyokuwa yakirushwa. Moja ya mabomu hayo
yaliangukia katika jengo la Benki ya Access na kusababisha wafanyakazi
wake kutoka nje.
Kamanda Mlowola alisema operesheni hiyo ni ya
kawaida na kwamba wamefanya hivyo kuondoa wafanyabiashara waliorejea
maeneo wasiyotakiwa.
No comments:
Post a Comment