Usafiri wa reli wamchanganya Dk. Mwakyembe
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amesma sekta ya usafiri wa
reli nchini inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo gharama kubwa za
uendeshaji, kutoaminika, huduma duni, sheria, sera na mifumo ya udhibiti kutokana na kutokuwepo na uwekezaji wa kutosha usiokuwa na ushindani.
Dk. Mwakyembe alisema hayo wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa
watalaamu wa sekta ya usafiri wa reli uliokuwa ukijadili rasmu ya sera
ya reli nchini ambao ulifanyika jana jijini Dar es Salaam.
Dk. Mwakyembe alisema ili kurejesha sekta ya reli kama ilivyokuwa
miaka ya nyuma, serikali imeamua kuandaa sera ya reli itakayojitegemea
badala ya hivi sasa ambapo ipo sera ya uchukuzi ambayo ni pana na
inajumuisha mambo mengi.
Alisema miongoni mwa mambo ambayo yanatakiwa kuangaliwa na wataalam
hao ni kuona kama Tanzania tuwe na reli ya upana upi, kwani iliyopo ina
upana wa mita moja.
Aliongeza kuwa baadhi ya wadau wanaona kwamba upana wa mita moja ni
kama umepitwa na wakati japo zipo nchi kama Japana na nchi nyingine
barani Afrika zinazotumia reli yenye upana huo.
Dk. Mwakyembe alisema hata kwa nchi za Afrika Mashariki zinahitaji
kuwa na mfumo wa reli zenye upana mmoja ambazo ni mita 1.435 ambayo
inatumiwa na nchi nyingi duniani.
Alisema kwa nchi kubwa kama Tanzania yenye idadi ya takribani watu
milioni 40 kunahitaji kuwa na usafiri wa reli wa uhakika ambao ni muhimu
kwa maendeleo ya nchi.
Alisema katika kuhakikisha sekta ya usafiri wa reli inaboreshwa, serikali ipo katika mchakato wa kununua vichwa 13 vya treni na vingine 18 vya kukodishwa.
Hata hivyo, Dk. Mwakyembe alisema kukodisha vichwa vya treni imekuwa
ghali sana hivyo serikali inalenga kufufua vichwa vibovu vilivyopo
nchini kwa kuhakikisha mafundi wanafanya kazi hiyo usiku.
Mwenyekiti wa kamati iliyopewa jukumu la kutayarisha rasmu ya
kutengeneza sera ya reli, Dk. Malima Bundara, alisema wakati wa
kutembelea mikoa mbalimbali walibaini hali ya usafiri wa reli ni mbaya
na miundombinu yake imechakaa sana.
Dk. Bundara alisema changamoto nyingine walizobaini ni kuvamiwa kwa
njia za reli na uwekezaji hivyo kuna haja ya kuwa na miongozo kama
serikali katika kuboresha usafiri huo.
No comments:
Post a Comment