|
Bi Kidude kabla ya kuhamishiwa Hindu Mandal, alipokuwa Zanzibar |
Na Princess Asia
HALI
ya afya ya msanii mkongwe nchini, Fatuma Bint Baraka, maarufu Bi Kidude ni
mbaya na akiwa amehamishwa kutoka Zanzibar hadi katika hospitali ya Hindu
Mandali Dar es Salaam na jana watu walikuwa wanazuiwa kwenda kumuona.
Bi
Kidude alianza kusumbuliwa na maradhi mwezi uliopita, lakini baadaye akapata
ahueni na kufanya mahojiano hadi na vyombo vya habari, lakini ghafla mambo
yamebadilika tena na amerudi hospitali.
Bi
Kidude ni gwiji wa muziki katika Bara la Afrika, katika fani ya muziki wa
mwambao ambao hujulikana kwa jina la Taarabu. Muziki huu ambao ni mchanganyiko
wa muziki toka nchi za Kiarabu na vionjo vya muziki wa Kiafrika umekita sana
katika mwambao wa Afrika Mashariki yaani Zanzibar, Mombasa, Lamu na kwingineko.
Fatuma
binti Baraka au Bi Kidude, alizaliwa katika kijiji cha Mfagimarigo Zanzibar
katika familia ya watoto saba (7). Baba yake Mzee Baraka alikuwa ni
mfanyabiashara wa nazi, zao ambalo ni la kutumainiwa sana Zanzibar.
Bi
Kidude anasema hafahamu tarehe halisi aliyozaliwa, isipokuwa anachojua ni
kwamba alizaliwa wakati rupia ikitumika kama fedha, na vilevile ana hakika ni
kabla ya Vita Kuu ya Kwanza ya Ulaya.
Wataalamu
wa mahesabu baada ya kupata taarifa hizo wakampigia mahesabu na kumkabidhi
miaka yake kwamba ni zaidi ya miaka 90.
Bi
Kidude anasema uimbaji aliuanza tangu alipokuwa na umri wa miaka 10 na
alijifunza kutoka kwa msanii mkongwe na aliyetamba sana enzi hizo Sitti Binti
Saad. Anasema wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali walikuwa wakifika Zanzibar
kuja kumwona Sitti, na kwa vile Bi Kidude na Sitti walikuwa wako karibu basi
yeye alikuwa akiwapeleka wageni wale nyumbani kwa Bi Sitti, wakifika huko
wageni walikuwa wakiingia ndani na yeye kubakia nje, kule ndani Bi Sitti
alikuwa akiwaimbia wale wageni, na yeye huku nje alikuwa akimsikiliza kwa
makini na kumfuatiza jinsi alivyokuwa akiimba. Aliendelea hivyo hadi akawa
mahiri sana katika uimbaji.
Alipokuwa
na miaka 13, kwa mara ya kwanza alitoroka nyumbani kwao Zanzibar na kukimbilia
Tanzania Bara, baada ya kulazimishwa kuolewa. Lakini alipokuwa kigoli wa
kutosha kuolewa aliolewa ingawa ndoa hiyo nayo haikudumu kutokana na manyanyaso
aliyokuwa akiyapata, hivyo aliamua kukimbilia kaskazini mwa Misri ikiwa ni
katika miaka ya 1930, huko aling'ara sana katika fani yake ya uimbaji na
uchezaji ngoma. Lakini ilipofika miaka ya 1940 aliamua kurudi nyumbani Zanzibar
ambako aliendelea na shughuli zake uimbaji.
Bi
Kidude hategemei kazi moja tu ya kuimba, kwani pia ni mfanyabiashara ya 'wanja'
na 'hina' ambavyo anavitengeneza yeye mwenyewe, pia ni mtaalamu wa matibabu kwa
dawa za mitishamba na zaidi ya hayo ni mwalimu mzuri sana wa 'Unyago' na
ameanzisha chuo chake mwenyewe na anasema katika wanafunzi wake wote hakuna
aliyepata talaka kutoka kwa mumewe.
Watu
wanasema 'Utu uzima dawa' Bi Kidude ana upeo mkubwa sana wa akili kwani pamoja
na kukulia katika mazingira yaliyogubikwa na tamaduni za kiarabu ambapo
mwanamke anatakiwa wakati wote akiwa hadharani ajifunike, Bi Kidude aliliona
hili katika upeo mwingine kwamba ni sheria tu ya kitamaduni toka Uarabuni,
hivyo aliamua kuvunja sheria hiyo na kuondoa hijabu mwilini mwake, na sasa hivi
anavaa kama Mtanzania na si kama Mwarabu. Lakini hakubakia hapo alivunja na
miiko mingine zaidi ya kutokunywa na kuvuta, kwani Bi Kidude anakunywa pombe na
kuvuta sigara jambo ambalo si kawaida kwa wanawake Zanzibar.
Bi
Kidude amekwisha tembelea nchi nyingi sana ikiwa ni pamoja na Oman, Ufaransa,
Hispania, Ufini, Ujerumani na Uingereza.
Amekwisha
pata tuzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ile ya Tamasha la Filamu la Nchi za
Jahazi (ZIFF) mwaka 1999 tuzo ni ya maisha. Pia mwaka jana tuzo ya WOMAX
ilienda kwake.
Nyimbo
alizowahi kuimba ni pamoja na Muhogo wa jang'ombe, na anaimba kwa Kiswahili na
Kiarabu. Hakuwahi kupata elimu nyingine zaidi ya Kurani. BIN ZUBEIRY inaungana na
Watanzania wote kumtakia kila la heri Bi Kidude, apone na kurejea nyumbani.
No comments:
Post a Comment