Mahakama nchini Zimbabwe imetupilia
mbali kesi iliyowasilishwa mahakamani na mwanamke mmoja kumzuia waziri
mkuu wa nchi hiyo Morgan Tsvangirai kufunga ndoa na mpenzi wake
Elizabeth Macheka Jumamosi hii.
Locadia Tembo alisema kuwa harusi hiyo haiwezi kufanyika kwani yeye ni mke wa kitamaduni wa Tsvangirai
Waziri mkuu Morgan Tsvangirai
Lakini jaji wa mahakama kuu Antonia Guvava alisema kuwa harusi za kitamaduni sio halali tena nchini Zimbabwe.
Rais Robert Mugabe, anatarajiwa kuhudhuria harusi hiyo.
Mwandishi wa BBC, mjini Harare Brian Hungwe,
anasema kuwa harusi hiyo inatarajiwa kufanyika katika mtaa mmoja wa
kifahari Kaskazini mwa Harare.
Rais Mugabe pia anatarajiwa kuandaa dhifa ya baada ya harusi ambayo itahudhuriwa na marais walioalikwa kwa harusi hiyo.
Bwana Tsvangirai, mwenye umri wa miaka 59 na rais Mugabe ambao ni viongozi wa muungano wa vyama tawala,
MDC na Zanu-PF wanatarajiwa, kugombea urais kila mmoja kwa chama chake mwaka ujao.
Kesi iliyowasilishwa na Bi Tembo mwenye umri wa
miaka 39 dhidi ya Tsvangirai, ilisikilizwa faraghani katika mahakama kuu
mjini Harare.
Jaji aliamua kuwa ndoa za kitamaduni sio halali
ila ikiwa tu kwa mazingira maalum mfano ikiwa ni kwa misingi ya kugawana
mali za wanandoa.
Pia alisema kuwa kesi hiyo ilipaswa kushughulikiwa na afisaa anayehusika na maswala ya ndoa katika mahakama ya hakimu.
Wakili wa Bi Tembo Everson Samkange, alisema
kuwa atawasilisha pingamizi zaidi katika mahakama ndogo ambayo itaweza
kupelekea kuundwa kwa tume maalum ikiwa kesi itaendelea.
No comments:
Post a Comment