MVOMERO YAZINDUA KITUO CHA‘KUCHIMBA DAWA’

WILAYA ya Mvomero mkoani Morogoro, imefungua kituo cha wasafiri kujisaidia ‘kuchimba dawa’ eneo la Lugono, Kata ya Mlali.

Kituo hicho ambacho kipo barabara kuu ya Morogoro-Iringa kilifunguliwa juzi na Mkuu wa Wilaya, Anthon Mtaka na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali.

Mtaka aliahidi kuishawishi halmashauri ya wilaya hiyo kusaidia kusogeza huduma za kijamii ikiwemo maji na kuliboresha eneo hilo, ili kuwavutia vijana na kinamama wajasiriamali.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Ofisa Afya wa Mkoa wa Morogoro, Carry Lyimo na Ofisa Afya wa Wilaya ya Mvomero, Ransom Fue, walisema eneo hilo lilianza kama kituo cha kupumzika na biashara ya mkaa.

Walisema eneo hilo liliendelea kukua kwa biashara ikiwemo kuuzwa maji, matunda, mama na babalishe hususani jamii ya wafugaji ambao walianza kuchinja mifugo hapo na kuuza nyama choma.

Awali, katika risala yake mzee aliyetoa eneo na kujenga kituo hicho, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Kisawani Agribusiness Investment Ltd, Kolekeni Kisawani, iliyosomwa na George Kisawani, alisema pamoja na changamoto mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa maji, wanakusudia kulifanya eleo hilo kuwavutia wasafiri na kujiongezea kipato.

Chanzo: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment