Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights
Watch, linasema kuwa lina ushahidi mpya kuonyesha ukiukwaji mkubwa wa
haki za binadamu uliofanywa na waasi wa M23 kwa usaidizi wa wanajeshi wa
Rwanda.
Shirika hilo linasema limefanya mahojiano na
watu 190, walioshuhudua matukio hayo Mashariki mwa Jamuhuri ya
Kidemokrasia ya Congo.
Utafiti wa shirika hilo unasema kuwa waasi wa M23 waliwasajili vijana wadogo na wanaume jeshini.
33 kati ya wale waliosajiliwa, wamesemekana
kuuawa walipojaribu kutoroka. Baadhi walifungwa kamba na kupigwa risasi ,
hatua hiyo ikisemekana kuwa mfano wa adhabu itakayotolewa kwa
watakaojaribu kutoroka.
Jamii ya kimataifa ilisitisha msaada kwa Rwanda
baada ya madai ya jeshi la Rwanda kusaidia waasi hao ingawa baadaye
msaada ulianza kutolea tena pale Uingereza iliposema kuwa imeweza
kuzungumza na Rwanda kuhusu swala hilo.
Shirika hili linasema liliwahoji familia za
waathiriwa wanyarwanda, maafisa wa utawala pamoja na wapiganaji wa
zamani wa kundi la M23 kati ya mwezi Mei na Septemba.
Kwa mujibu wa afisaa mkuu wa utafiti,Anneke Van
Woudenberg, waasi wa M23 wanafanya visa vya kuogofya vya ukiukwaji wa
haki za binadamu, Mashariki mwa Congo.
Moja ya visa walivyodokezewa watafiti wa HRW, ni
kile cha mwanamke mwenye umri wa miaka 32 aliyesema kuwa waasi
wallivunja mlango wake na kumpiga mtoto wake mwenye umri wa miaka 15
hadi kufariki na kisha kumteka nyara mumewe. Kabla ya kuondoka waasi hao
walimbaka kila mmoja kwa zamu, na kisha kumwagia mafuta taa kwenye
miguu yake na kuiteketeza. Aliokolewa na jirani zake baada ya waasi hao
kuondoka.
HRW imetoa wito kwa jamii ya kimataifa
kuwachukulia hatua waasi wa M23 huku akipendekeza maafisa wa Rwanda
waliohusika na vita hivyo kufunguliwa mashtaka kwa kusaidia waasi hao
kukiuka haki za binadamu pamoja na kutoa mafunzo, silaha na zana nzito
za vita kwa waasi hao.
Hata hivyo serikali ya Rwanda imekuwa ikikana madai kuwa jeshi lake linahusika na uasi Mashariki mwa DRC.
No comments:
Post a Comment