Vijiji vinne vyashambuliwa upya Tana River

Shirika la msalaba mwekundu la Kenya , Kenya Red Cross, limeelezea kushuhudia mashambulizi mapya asubuhi ya leo katika vijiji vinne vya Semikaro, Laini, Nduru na Shirikisho katika kaunti ya Tana Delta.

Mamia ya washambulizi wameweza kujikusanya kwa makundi katika mashambulizi yanayoendelea huku nyumba zikiteketezwa na watu wakikimbilia usalama wao.

Duru zinasema kuwa polisi 3 zaidi wameuawa usiku wa kuamkia leo

Hapo jana rais Mwai Kibaki alitangaza marufuku ya kutotoka nje nyakati za usiku katika maeneo yaliyoathirika kutokana a na vita vya kikabila na vya kulipiza kisasi vinavyoendelea Tana Delta.

Duru zinasema kuwa polisi waliozidiwa nguvu walilazimika kuondoka katika eneo hilo.

Mnamo siku ya Jumatatu, watu 38 waliuawa katika mapigano mapya yaliyozuka eneo la Tana River siku tatu tu baada ya watu 12 wa kabila la Pokomo kuuawa katika mashambulizi yaliyofanya na jamii hasimu ya Orma.

Polisi 8 ni miongoni mwa waliouawa katika makabilianao ya hapo jana.

Kulingana na Red Cross, nyumba ziliteketezwa moto baada ya kijiji kimoja nkuvamiwa na zaidi ya watu mia tatu.

Tukio hilo linajiri siku kadhaa baada ya mashambulizi mengine kutokea kwenye eneo hilo la Tana Delta na kusababisha vifo vya karibu watu kumi na saba.

Polisi kwa usihirikiano na shirika la msalaba mwekundu waliweza kuokoa manusura. Inaarifiwa watu wameanza kuhama eneo hilo la Tana River kukimbilia usalama wao.

Mwezi jana zaidi ya watu 50 waliuawa katika mapigano mengine kati ya jamii za Pokomo na Orma.

Hizi ni ghasia mbaya zaidi kushuhudiwa hivi karibuni tangu zile za mwaka 2007 kufuatia uchaguzi uliozua utata mkubwa.

Jamii ya wapokomo ambao ni wakulima wanaoishi katika eneo la mto Tana huzozana mara kwa mara na jamii ya wafugaji ya Orma chanzo kikiwa malisho na maji.

Serikali ya Kenya imelaumiwa sana kwa kujikokota katika kuchukua hatua za kusitisha mashambulizi haya ya kulipiza kisasi ambayo yamekuwa yakiendelea kwa muda mrefu huko Tana Delta.

Wito umetolewa wa kuwapokonya silaha makundi ya watu waliojihami ili kukomesha mashambulizi hayo.

No comments:

Post a Comment