Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari- Mechi Ya Ngao Ya Jamii Kuchangia Hospitali Ya Temeke
Release No. 142
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Septemba 7, 2012
MECHI YA NGAO YA JAMII KUCHANGIA HOSPITALI YA TEMEKE
Asilimia
tano ya mapato yatakayopatikana kwenye mechi ya Ngao ya Jamii
(Community Shield) kati ya Simba na Azam yatakwenda kwenye Hospitali ya
Temeke mkoani Dar es Salaam.
Kabla
ya kukabidhi, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litakutana na
uongozi wa Hospitali ya Temeke kupanga maeneo ambayo fedha hizo
zitatumika kwenye hospitali hiyo.
Mechi
hiyo ya uzinduzi rasmi wa msimu wa 2012/2013 itafanyika Jumanne ya
Septemba 11 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa
10 kamili jioni.
Viingilio
kwenye mchezo huo vitakuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya bluu na
kijani, sh. 10,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 kwa viti vya
VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 20,000.
WACHEZAJI WAWILI WAOMBEWA ITC URENO
Shirikisho
la Mpira wa Miguu la Ureno (FPF) limetuma maombi Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) kupatia Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa
wachezaji wawili waliokuwa wakicheza mpira nchini.
Wachezaji
wanaoombewa ITC ni Hamis Thabit Mohamed (19) ambaye klabu yake ya
mwisho aliyoichezea nchini ilikuwa African Lyon wakati mwingine ni Abuu
Ubwa Zuberi (20) ambaye msimu uliopita alikuwa akiichezea timu ya Yanga.
Kwa
mujibu wa FPF, wote wawili wanaoombewa ITC kama wachezaji wa ridhaa
(amateur) ili waweze kujiunga na timu ya Atletico Sport Clube ya Ureno
ambayo hata hivyo haikuelezwa iko daraja gani nchini humo.
Pia
FPF imeombwa kupatiwa hati ya maelezo ya mchezaji (player’s passport)
kwa kila mmoja ikiwemo taarifa za ushiriki wao katika mechi rasmi
zinazotambuliwa na TFF wakiwa katika klabu zao hizo za zamani.
STARS YAPANGIWA UGANDA CHAN 2014
Timu
ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imepangiwa kucheza na Uganda (The
Cranes) katika raundi ya kwanza ya michuano ya kuwania tiketi ya kucheza
Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zitakazofanyika Afrika
Kusini mwaka 2014.
Kwa
mujibu wa ratiba iliyopangwa jana (Septemba 7 mwaka huu) makao makuu ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) jijini Cairo, Tanzania
imeingia moja kwa moja raundi ya kwanza ambapo itacheza na Uganda.
Mechi
ya kwanza itachezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kati ya Juni
21,22 na 23, 2013 wakati ya marudiano itakuwa Uwanja wa Mandela ulioko
Namboole jijini Kampala kati ya Julai 5,6 na 7, 2013.
Nchi
38 zinashiriki katika mechi hizo za mchujo ambapo nyingine zitaanzia
raundi ya awali itakayochezwa kati ya Novemba 30 na Desemba 1 na 2 mwaka
huu wakati mechi za marudiano zitakuwa kati ya Desemba 14,15 na 16
mwaka huu.
Ratiba
imepangwa kwa makundi ya kanda ambapo jumla ya timu 16 ndizo
zitakazocheza fainali hizo nchini Afrika Kusini. Kanda hizo ni Kaskazini
itakayopeleka timu mbili katika fainali, Magharibi A (timu mbili),
Magharibi B (timu tatu), Kati (timu tatu), Kati Mashariki (timu tatu),
Kusini (timu tatu akiwemo mwenyeji Afrika Kusini).
Kwa upande wa kanda ya Tanzania (Kati Mashariki), timu zinazoanzia raundi ya awali ni Burundi, Eritrea, Ethiopia na Kenya.
Fainali
za Kwanza za CHAN zilifanyika mwaka 2009 nchini Ivory Coast ambapo
Tanzania ilishiriki huku Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ikiibuka
bingwa. Fainali za Pili zilichezwa mwaka 2011 nchini Sudan ambapo
Tunisia ilitwaa ubingwa. Fainali za Kwanza zilishirikisha timu nane
kabla ya kuongezwa hadi 16 za sasa.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment