TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI TOKA KWA JUKWAA LA KATIBA TANZANIA DHIDI YA MAUAJI YA MWANDISHI DAUDI MWANGOSI

MWANDISHI DAUDI MWANGOSI

JUKWAA LA KATIBA TANZANIA
P. O. Box 78466, Plot No. 714/18 Mwenge, Behind TRA Offices, Dar Es Salaam, TANZANIA
Tel: +255 22 2773795 Fax: +255 22 2773764 Cell: 0783 993088
TAMKO LA JUKWAA LA KATIBA TANZANIA DHIDI YA MAUAJI YA MWANDISHI DAUDI MWANGOSI
‘‘Mauaji Ya Waandishi Na Wananchi Yatavuruga Mchakato Wa Kupata Katiba Mpya Tanzania!’’
JUKWAA LA KATIBA TANZANIA tumepokea taarifa za kuuawa kinyama kwa Mwandishi Daudi Mwangosi wa Channel 10 na Mwenyekiti wa Chama cha waandishi wa Habari mkoani Iringa (IPC) kwa mshtuko na masikitiko makubwa. Kama ilivyokwishaelezwa na wengi, kifo cha mwandishi huyu ni cha kwanza cha aina yake katika tasnia ya habari nchini na kinatishia si tu uhuru wa kutoa maoni na uhuru wa habari kwa ujumla wake, bali pia kifo hiki na vingine vya siku za karibuni vinauweka mchakato wa Katiba Mpya njia panda.
Vitendo vya mauaji ya raia vinazidi kushamiri siku hadi siku. Wapo wananchi wanaouawa na watu wanaoitwa wenye hasira kali kwa tuhuma za uhalifu. Wapo raia wanaouliwa na majambazi na wahalifu wengine kwa sababu ya ulinzi duni katika maeneo wanayoishi. Aidha, wapo pia wananchi wanaopoteza maisha yao kila siku kwa tuhuma za kwamba ni wachawi. Ukiacha hao, idadi kubwa ya watanzania wanaishi na ulemavu wa ngozi wamepoteza maisha kwa kukatwa viungo au kuuliwa kabisa kwa imani za kishirikina. Hali sasa imefikia kuwa mbaya hadi kuna watanzania wanajisikia salama zaidi wakiwa mwituni kuliko majumbani. Yote haya yanasikitisha sana kwa ujumla wake! Haki ya kuishi inayowekwa na kulindwa na ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanza kuingia dosari katika Tanzania.
Ukiacha mauaji yanayofanywa na watu wasiojulikana au miongoni mwa raia, yamekuwepo pia mauaji yanayozidi kuongezeka ya raia yanayofanywa na wawekezaji au matajiri nchini. Zipo kesi kadhaa za mauaji ya namna hii. Hayo nayo yamekuwa yakitokea kwa sababu ya ulinzi mdogo ambao wananchi wanao kutoka kwa vyombo vya ulinzi na usalama nchini. Jeshi la Polisi, ambalo ndio lenye dhamana ya kulinda watu na mali zao haliwezi kukwepa lawama katika aina zote hizo za mauaji. Itakumbukwa pia kuwa ajali za magari, mabasi na meli zinagharimu sana maisha ya watanzania katika siku za karibuni. Kwa kiasi fulani, hata kukithiri kwa ajali hizi nako kunahusishwa na mwenendo mbovu wa usimamizi wa vyombo vya usafiri unaofanywa na idara mbalimbali za serikali ikiwemo kikosi cha usalama barabarani. Roho za watanzania zinazidi kupotea kutokana na udhaifu mkubwa unaosababishwa na rushwa na mambo mengine ya ukosefu wa maadili katika vyombo vya usimamizi wa haki.
Mauaji ya raia yanayofanywa moja kwa moja na askari wa Jeshi la Polisi nayo yanazidi kuongezeka sana kiasi cha kutishia amani na utulivu wa nchi yetu. Aidha, mauaji yanayohusishwa na siasa nayo yanazidi kuongezeka na kuzidisha chuki ya kisiasa ambayo ni mbaya sana kwa ustawi wa nchi yetu. Kwa mfano katika miezi ya Karibuni, kumekuwepo matumizi ya nguvu kuzidi kiasi kwa raia wanaokuwa wakipanga na kufanya maandamano au mikusanyiko yenye lengo la kujadili au kupinga jambo fulani. Matokeo yake, kumetokea majeruhi na mauaji ambayo yamesababishwa na vurugu ambazo zinatokana na Jeshi la Polisi kudhibiti vitendo halali vya wananchi. Kwa sababu hiyo, JUKWAA LA KATIBA TANZANIA tunatoa wito ufuatao kwa Jeshi la Polisi na idara nyingine za serikali zenye dhamana ya kulinda usalama wa raia, mali na mipaka ya Nchi yetu:
  1. Jeshi la Polisi liache kutumia nguvu kuzidi kiasi katika matukio yote ya kulinda mikutano na matukio ya hadhara. Tujuavyo sisi, Jeshi la Polisi linalotumia risasi za moto, mabomu ya kivita, maji ya kuwasha na gesi ya kutoa machozi dhidi ya raia ambao hawajabeba hata fimbo za kuchungia mifugo. Ni Jeshi lisilojiamini na linaloonesha woga wa ajabu.
Kwa hadhira kama za Nyololo, Morogoro, Mbeya, Dar es Salaam na nyinginezo miezi ya Karibuni, Jeshi la Polisi lingeweza kuwatuliza wananchi kwa kutumia filimbi tu. Matumizi ya nguvu na kumwagia maji ya kuwasha hata wazee wastaafu wanaodai haki zao inaweza kuwa ndio laana inayopelekea Polisi kusikia furaha kuua kila mara. Ipo kanuni ya kimataifa inayowataka Polisi kutumia nguvu kidogo sana inayolingana tu na nguvu ya umma wanaokabiliana nao katika kutuliza ghasia.
  1. Wakati huu wa mchakato wa kutengeneza Katiba mpya ya Tanzania na hata baada ya hapo, Jeshi la Polisi lijiepushe kuingilia shughuli za Kisiasa kwa kuziunga mkono au kuzivuruga. Mikusanyiko mingi ambayo imepelekea mauaji wakati polisi ikijaribu kuivunja ni matukio yaliyolenga kupata majibu ya kisiasa na siyo ya kipolisi. Wajibu wa Jeshi la Polisi katika wakati kama huo ni kulinda na kuwezesha wananchi husika kueleza madai yao kwa uhuru na bila kuvurugwa na kundi jingine lolote la watu wasiopendezwa na madai ya kundi husika. Tabia inayozidi kushamiri ya Jeshi la Polisi kutaka kujibu au kuzima hoja za Kisiasa au kiuchumi kwa mtutu wa bunduki, mabomu, maji ya kuwasha na virungu ni tabia ya Jeshi kutaka kuingilia kazi isiyo yake na ndio maana inawashinda. Aidha, kama Polisi wangekuwa ni wataalam wa Siasa, wangegundua kuwa wanachokifanya ni kuahirisha matatizo na si kuyatatua!
  2. Jeshi la Polisi na vyombo venye dhamana ya ulinzi vijitambue upya kuwa vina wajibu wa kulinda raia, mipaka na mali zao si vinginevyo. Mauaji yanayoendelea nchini ni uporaji wa haki ya kuishi na haki nyingine nyingi chini ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar. Aidha, Jeshi la Polisi na serikali kwa ujumla wana wajibu wa kuhakikisha na kudumisha ustawi wa wananchi kwa mujibu wa ibara ya 8 (1) (b) na hawana mamlaka ya kuua raia. Ikumbukwe kuwa mamlaka yote kikatiba katika Tanzania yako kwa wananchi na serikali pamoja na Jeshi lake la Polisi watapata madaraka na mamlaka hayo kutoka kwa Wananchi. Nani amewapa Polisi mamlaka ya kuua watanzania? Nani amewapa Jeshi la magereza mamlaka ya kuwapiga na kumwaga damu za Waandishi? Nani amewapa askari wanyamapori mamlaka ya kupiga risasi hovyo na kuua ng’ombe mbele ya wenye mali yao?
  3. Athari za matukio ya mauaji na fujo zinazosababishwa na Jeshi la Polisi kutawanya waandamanaji au mikusanyiko mingine ni kubwa sana katika kuathiri vibaya hamasa ya wananchi kwenye Mchakato wa Katiba. Mpaka sasa, tayari watu wengi wameingia wasiwasi na wameamua kutoshiriki mikutano ya kutoa maoni ya Katiba inayoendeshwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini. Endapo Jeshi la Polisi halitaacha kuua na kutishia raia kwa kila wanachokifanya, mchakato wa Katiba utavurugika kabla Katiba mpya haijapatikana. Kwa mwenendo wa sasa, Jeshi la Polisi litakuja kupiga mabomu na kuua hata wananchi watakapokuwa katika Mabaraza ya Katiba wakijadili na kupinga baadhi ya vipengele vitakavyoingizwa katika rasimu ya Katiba. Pia, itafika wakati wananchi watataka kuandamana kwa amani kuunga mkono au kupinga mambo Fulani katika Katiba. Kwa hali ilivyo, Jeshi la Polisi litaona hiyo ni fursa ya kutumia mabomu na risasi kuzuia wasiseme wanayotaka kusema. Hii ni hatari kubwa sana!
  4. Mikusanyiko, maandamano na shughuli za mikutano ya Siasa ni matendo halali na haki ya kila mtanzania kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, 1977 ibara ya 8, 20 na 21. Suala la kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kwa mujibu wa sheria ya Jeshi la Polisi ni suala la kuwajulisha tu kwa lengo la kuwaweka tayari endapo kutahitajika msaada wa Jeshi la Polisi wakati wa shughuli kama hiyo. Tabia iliyoota mizizi ya Polisi kujiona kama wamepewa taarifa ili watoe au kukataa kibali ni uelewa finyu wa Katiba na sheria za Nchi. Ipo haja ya kuongeza uelewa wa wasimamizi wetu wa sheria ili wawe na uelewa mpana wa sheria na ibara za Katiba wanazozisimamia badala ya kujiona kama wana wajibu wa Msajili wa vyama vya Siasa wa kuratibu shughuli za vyama. Mikutano, mikusanyiko, mihadhara, maandamano na mijadala ni haki ya Kikatiba ya Kila mtanzania binafsi na kwa makundi.
Kwa kuwa haki ya kuishi iliyoporwa kwa Mwandishi Daudi Mwangosi ndio haki kubwa kuliko zote, JUKWAA LA KATIBA TANZANIA tunataka jambo hili lisiishie kuunda Tume za uchunguzi pasipo kufanyia kazi mapendekezo yake. Aidha, kwa kuwa uchunguzi unaofanywa hauhusiani na kilichomuua ndugu Mwangosi wala kundi gani limemuua, tunapendekeza busara itumike kwa viongozi wa Jeshi la Polisi, kuanzia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa kuachia ngazi ili kupisha uchunguzi huru wa Tume itakayoundwa na Mheshimiwa Rais ikihusisha na kuongozwa na mhimili wa Mahakama. Taarifa ya uchunguzi ipelekwe Bungeni na Mheshimiwa Rais kwa ajili ya kujadiliwa na ushauri wa kibunge. Kamati iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi tunaitamka rasmi kuwa batili kwa kutumia kanuni ya sheria za kiasili inayosema kuwa mtu au kundi hawezi kuwa hakimu wa kesi inayomhusu mwenyewe. Bila kufanya hivyo, tunapata wasiwasi kama Tume ya namna hiyo inaweza kufanya kazi yake kwa uhuru. Kuachia ngazi kwa Kamanda wa Polisi mkoani Iringa kutakuwa ishara kuwa Jeshi la Polisi linahitaji kuwa makini zaidi katika kufanya kazi yake ya kulinda amani, mali na maisha ya watanzania. Kwa sasa, zipo hisia kuwa Jeshi la Polisi lipo juu ya sheria na Katiba, jambo ambalo tunapenda kulikanusha vikali!
Mwisho, tunapenda kutoa rai kwa serikali kutangaza rasmi kuwa itachukua jukumu la kutunza, kusomesha, kulisha na kuhudumia familia aliyoiacha Daudi Mwangosi kuanzia sasa kwa muda wa miaka 20 watakapoweza kujitegemea wenyewe. Itakuwa ni fedheha kuiona familia aliyoianzisha Marehemu Mwangosi ikisambaratika kwa sababu kichwa cha nyumba hiyo kimesambaratishwa na bomu la Polisi ambalo kodi yake Mwangosi ilichangia kulinunua.
Kufikia hapa, tunapenda kutangaza rasmi kuwa msiba huu ni msiba wa KIKATIBA na tunaomba ufahamike hivyo kwa umma wote wa watanzania na kote duniani.
Mungu ailaze roho ya Marehemu Mwanahabari Daudi Mwangosi mahali pema peponi – Amina!
Imetolewa na kusainiwa kwa niaba ya JUKWAA LA KATIBA TANZANIA,
Deus M Kibamba
Mwenyekiti

No comments:

Post a Comment