Wauguzi
nchini Kenya wakiwa wamewabeba watoto walipatikana kwa njia ya
mwananmke kupandikizwa mbegu za kiume, ripoti za nchini kenya
zinaonyesha watanzania 60 wamekwenda nchini humo kupata huduma hiyo.
Picha na Arthur okwemba
Florence Majani na Herieth Makwetta
TATIZO
la uzazi linaonekana kushika kasi nchini baada ya idadi kubwa ya
wanandoa kukimbilia Kenya kupata huduma ya upandikizaji wa watoto kwa
gharama ya zaidi ya Sh5 milioni.Kati ya wageni 10 wanaokwenda katika vituo vya upandikizaji vya Aga Khan na Nairobi IVF Centre nchini humo, wanne wanatoka Tanzania.
Licha
ya kuwapo kwa huduma hiyo nchini, imeelezwa kwamba Watanzania wengi
wanakimbilia huko kutokana na unafuu wa gharama na ubora wa huduma.
Huduma hiyo ni ya mwanamke kupandikizwa mbegu ya kiume ili kuweza kushika mimba na baadaye kupata mtoto. Mmiliki
wa Kituo cha Upandikizaji cha Nairobi (Nairobi IVF Centre), Dk Joshua
Noreh alisema kwa mwaka kliniki yake hupokea zaidi ya wagonjwa 270
kutoka mataifa mbalimbali likiwamo Bara la Ulaya.
Alisema wagonjwa kutoka Tanzania walianza kumiminika katika kliniki
hiyo kuanzia mwaka 2006 na ukiondoa gharama za matibabu ambazo ni Sh5.4
milioni zipo gharama za ushauri na uchunguzi wa tatizo.
“Gharama
ya ushauri peke yake ni Sh42,000 za Tanzania. Baada ya ushauri, mgonjwa
hutozwa Sh420,000 kwa ajili ya uchunguzi wa tatizo. Gharama za matibabu
hutegemea ukubwa wa tatizo. Tiba yenyewe ni upandikizaji wa mbegu, hadi
hatua za kuirutubisha,” alisema.
Dk Noreh alisema ukijumlisha
gharama za usafiri, malazi, mlo na tiba kwa wagonjwa wanaotoka Tanzania,
wengi wao hutumia kati ya Sh8milioni hadi Sh10 milioni, kwa ajili ya
kupata mimba.
Imeelezwa kuwa raia wa Uganda hukimbilia Kenya
kukwepa gharama kubwa kwani nchini humo hugharimu kiasi cha Sh500,000 ya
Uganda (sawa na Sh9.5 milioni) wakati huduma hiyo hupatikana Kenya kwa
Sh300,000 (sawa na Sh5.4 milioni) kwa mzunguko.
“Tuna vituo zaidi
ya vitano vya IVF hapa Kenya, ndiyo maana Kenya imekuwa kimbilio la
wanandoa au wapenzi kupata matibabu ya aina mbalimbali za ugumba.
Lakini kikubwa ni huduma bora na gharama nafuu ndiyo sababu ya ongezeko
hili la wageni kutoka nje.”
Alisema baadhi ya nchi hazina huduma ya IVF hivyo wanandoa huenda Kenya na wengine wanayo huduma hiyo katika nchi zao ila wanachagua Kenya kwa sababu ya urahisi wa tiba hiyo na kuwapo kwa mbegu za wanaume wa Kiafrika zilizohifadhiwa.
Nchi
nyingine ambazo wanandoa wake wanaongoza kwenda Kenya kwa ajili ya
kupata huduma ya upandikizaji wa watoto ni Uganda, Sudan ya Kusini,
Marekani na Ethiopia.
Mtaalamu kutoka Hospitali ya Chuo Kikuu cha
Aga Khan Nairobi, Dk Prafull Patel alisema idadi ya wanaohitaji huduma
hiyo imekuwa ikiongezeka kwa kasi kutoka mataifa ya Afrika, Uingereza na
Marekani.
Alisema zaidi ya robo tatu ya wanaopata huduma hiyo ni watu kutoka nje ya Kenya, lakini hasa ni kutokana na unafuu wa gharama za huduma hiyo ikilinganishwa na nchi nyingine.
Nchini
Uganda, IVF inagharimu Sh9,000,000 za Tanzania wakati Uingereza
inagharimu zaidi ya Sh10,800,000 za Tanzania na kwa wenza zinafikia
Sh21,600,000 kwa kila mzunguko huku Marekani ikigharimu Sh10,620,000 na
Sh19,800,000 kwa mzunguko.
Hii inamaanisha kwamba gharama nchini
Kenya ni nusu ya gharama inayolipiwa Marekani, Ulaya na nchi nyingine za
Afrika. Hiyo inaelezwa kuwa chanzo cha ongezeko la idadi ya wageni
kwenda Kenya kusaka tiba ya ugumba.
Upandikizaji unavyokuwa Upandikizaji huo hufanyika kwa kuchukua mbegu za mwanamume na kuzipandikiza katika mirija ya uzazi ya mwanamke.
Mwanamke mwenye matatizo huweza kwenda peke yake kupandikizwa kwa kununua mbegu zilizohifadhiwa katika kliniki au wanandoa kwenda pamoja na mwanamume kutoa mbegu ambazo zitapandikizwa kwa mwanamke.
“Tiba
huchukua mwezi mmoja, huanzia siku ya pili baada ya mwanamke kumaliza
hedhi na siku ya yai kurutubishwa lakini mwanamume hutumia siku moja tu
pale mbegu zake zinapohitajika.”
Dk Noreh alisema sababu ya kuanza
tiba siku ya pili baada ya mwanamke kumaliza mzunguko wake wa mwezi ni
kulenga tarehe za uchavushaji, kwani kipindi hicho mbegu za mwanamume
hupandikizwa na kusababisha mimba kutungwa.
“Mbegu
zilizorutubishwa huachwa kwa siku mbili mpaka tano ndani ya chombo
maalumu ili kukuza kiinitete (embryo) kabla ya kuhamishwa katika nyumba ya uzazi ya mwanamke kwa ajili ya kutungisha mimba ya kawaida.”
Alisema
tatizo la ugumba linaongezeka duniani na njia hiyo inatumika kuwasaidia
wanawake wasiokuwa na mayai ambao mirija yao ya kuyasafirishia imeziba
na wanaume ambao manii yao ni dhaifu na hushindwa kuogelea hadi kufikia
yai la mwanamke...
“Tatizo la ugumba kwa sasa ni wastani wa
asilimia 10, hiyo ina maana kwamba kati ya wanandoa 10 mmojawapo hana
uwezo wa kushika mimba. Kiwango hiki kwa sasa kinakua kutokana na sababu
mbalimbali ikiwamo wanawake wa sasa kuchelewa kuolewa wakitoa
kipaumbele kumalizia masomo,” alisema Dk Noreh.
Wataalamu wa Tanzania Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba cha Muhimbili, Dk Henry Mwakyoma
alisema ongezeko la Watanzania kufuata huduma hiyo Kenya, limesababishwa
na kukua kwa tatizo la uzazi nchini.
Dk Mwakyoma alisema huduma
hiyo hutolewa kama tatizo la uzazi analo mwanamke. Alisema kama
mwanamume ndiye mwenye tatizo, huduma hiyo haiwezi kutolewa.
“Kama
mwanamke ana tatizo la uzazi, kwa mfano mirija imeziba, kizazi
kimelegea, anaweza kufanyiwa upandikizaji na kupata mtoto, lakini kama
mbegu za mwanamume ni dhaifu, hakuna kitu kinafanyika,” alisema.
Dk
Mwakyoma ambaye aliwahi kufanya utafiti na kubaini kuwa asilimia 80 ya
wanaume nchini wana tatizo la ugumba wa kudumu au wa muda, alisema mfumo
wa maisha wa sasa ndicho chanzo cha ongezeko la tatizo la uzazi.
Daktari kutoka kituo kimoja cha upandikizaji nchini ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema huduma hiyo inapatikana katika kituo hicho kwa bei nafuu kuliko huko Kenya.
“Gharama
za hapa zinategemea ukubwa wa tatizo la mhusika, mchakato wake na afya
yake. Wapo wengine hawahitaji kupandikizwa, wengine wanahitaji tu dawa,
pia wapo wengine wanaweza kufanyiwa upandikizaji kwa zaidi ya mara
moja,” alisema.
Alisema tangu kufunguliwa kwa kituo hicho Februari
mwaka huu, idadi ya wanandoa wanaokwenda kupata huduma hiyo imekuwa
ikiongezeka. Hata hivyo, hakutaka kuweka wazi takwimu rasmi kwa mwezi au
tangu kufunguliwa kwake.
|
No comments:
Post a Comment