UMOJA WA VILABU VYA WAANDISHI WA HABARI TANZANIA YATOA TAMKO KUHUSIANA NA MAUAJI YA MWANDISHI WA CHANNEL TEN DAUDI MWANGOSI MKOANI IRINGA


Wajumbe wa Mkutano Mkuu UTPC wakiwa wamesimama kwa
dakika moja kumuombea Marehemu Daudi Mwangosi aliefariki katika Vurugu
za Chadema na Polisi mkoani Iringa

UMOJA wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC)umesema kuwa
kufuatia mauaji ya mwandishi wa habari wa Wa kituo cha Channel Ten
Mkoani Iringa Bw. Daudi Mwangosi kimeitaka serikali kuwasimamisha
kazi askari waliohusika katika tukio la mauaji ya kinyama ya mwandishi
huyo.
Umoja huo umesema kuwa askari walioshiriki katika oparesheni hiyo
ambayo ni haramu kusimamishwa mara moja ili kupisha uchunguzi
kufanyika.
Hayo yalisemwa jana Jijini Dar Es Salaam na Rais wa UTPC Bw.Keneth
Simbaya wakati alipokuwa akitoa tamko Kwa Viongozi wa Vilabu Mikoani
kuhusiana na mauaji dhidi ya mwandishi wa habari Huyo aliyeuwawa
akiwa mikononi mwa polisi katika kijiji cha Nyololo Wilayani Mufindi.
“Hapa tunataka uchunguzi huu ukikamilika tunaitaka serikali
kuutangazia umma na kupisha sheria kwa wale watakaobainika kuhusika
kwa uzembe huo kwa namna moja au nyingine wachukuliwe hatua dhidi ya
mauaji hayo ya mwandishi wa habari Bw. Daudi Mwangosi”alisema.
Hata hivyo Bw. Simbaya alisema wakati uchunguzi ukiwa unaendelea
serikali iridhie na kurasimisha malipo kwa ajili ya Mjane wa
mwandishi huyo na watoto walioachwa na marehemu ili waweze kujikimu.
Aidha alisema licha ya kutoa tamko hilo wanaendelea kulitazamia jeshi
la polisi kama mdau mwenye shaka kwa namna wanavyotenda kazi zao
na waandishi wa habari mikoani na kwamba watataarifu umma kuhusu
mwenendo wao hapo baadae.
“Lakini pia katika mkutano huu tumeridhia kushirikiana na taasisi
zingine za haki za binadamu ,uwakili na Utetezi ili kubaini namna
bora ya kuishitaki serikali kama mwenendo wa suala hili hautakuwa
unaleta tija Kutokana na vithibitisho hivyo tunakaribisha mashirika
ya haki za binadamu ,asasi zisizokuwa za kiserikali ili kuweza
kufanikisha azma hii”alisema Bw. Simbaya.
Akizungumzia kuhusu usalama kwa waandishi wa habari Bw. Simbaya
alisema katika kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanafanya kazi yao
kwa usalama amelitaka jeshi la polisi kutoa utaratibu ambao
utawezesha wanahabari nchini kufanya kazi kwa usalama bila hofu wala
dharau,kutoa elimu kwa jeshi la polisi kuhusu umuhimu wa wanahabari
na jukumu lao katika Taifa.
Hata hivyo baadhi ya viongozi wa Vyama vya waandishi wa habari
Tanzania ambao wanahudhulio mkutano mkuu wa UTPC walisema tamko hilo
halijapewa uzito kutokana na tukio la mauaji lenyewe na jinsi lilivyo
huku wakitaka Tamko hilo kupewa uzito wa kina.
“Hili Tamko lilitakiwa kupewa uzito sana kwani sisi tuliokuwepo
katika msiba huo kwa ujumla inasikitisha sana hivyo tamko ni muhimu
lipewe uzito zaidi kulingana na mauaji yenyewe yanavyotisha hivyo
tufuate maamuzi ya viongozi wa clabu waliotoa matamko ya kususia
habari za polisi mpaka pale watakapokuwa wameridhia kukaa meza moja
na wanahabari juu ya mauaji hayo”alisema mmoja wa viongozi wa clabu
za waandishi wa habari Tanzania Bw. Christopher Nyenyembe.

No comments:

Post a Comment