*Rais Kikwete: Rushwa inakipeleka Chama cha Mapinduzi pabaya
*Mbunge asema: �Kujivua gamba� kulishindwa kabla ya utekelezaji
* Nape ampinga, asema kiwango cha malalamiko ya rushwa ni kidogo
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye
Hoja ya Waziri
Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye kuhusu kushamiri kwa rushwa ya mtandao
ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inazidi kuungwa mkono ndani ya chama
hicho.
Mbunge wa Mwibara mkoani Mara (CCM), Kangi Logora, ameibuka na kusema
kushamiri kwa rushwa hiyo ni matokeo ya kushindwa kutekeleza dhana ya
‘kujivua gamba’, iliyoasisiwa na Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.
“Kujivua gamba kuliondoka hata kabla ya utekelezaji wake,” alisema
Lugora, mmoja wa wabunge waliosaini waraka wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini
(Chadema), Zitto Kabwe, kuhusu kupiga kura ya kutokuwa na imani na
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Dhana hiyo ilipitishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM katika
vikao vyake vilivyofanyika kati ya Aprili 10 na 11, mwaka jana, na
kuwataka watuhumiwa kwa ufisadi, kujiondoa kwenye chama hicho vinginevyo
wangefukuzwa.
Kujivua gamba kulipata nguvu kubwa ya kuenezwa nchini, kupitia viongozi
wa ngazi za juu wa chama hicho akiwemo, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi
wa CCM, Nape Nnauye.
Nnauye alisisitiza kuwepo utekelezaji wa ‘kujivua gamba’ huku akiwatisha
watuhumiwa wa ufisadi, kwamba barua zao zipo tayari na kuwataka
kuhakikisha wanajiondoa ndani ya chama hicho kabla ya kuondolewa.
Lugora alisema chaguzi ndani ya CCM zilitarajiwa kutoa jawabu la kero ya
rushwa na kuibua mtazamo mpya utakaojenga imani ya wananchi kwa chama
hicho.
“Tuliratajia chama chetu kirudi kwenye mstari, lakini sasa ni kama
tumepoteza mwelekeo, tumekubali kuingia kwenye mtego wa rushwa bila
kujiuliza watoa rushwa wanazipata wapi fedha hizo,” alisema.
Lugora alisema hali ilivyo sasa, inaashiria wasiwasi na kuwaacha
wanachama waadilifu kutojua nini kitafuata baada ya mafanikio
yanayotokana na rushwa.
CCM KUELEKEA SHIMONI 2015
Lugora alisema kutokana na mafanikio yaliyopatikana kupitia matumizi
makubwa ya rushwa katika ngazi za chini, ni dhahiri kuwa uchaguzi wa
ngazi ya taifa utatawaliwa na uovu huo.
“Kama wamefanikiwa kujipanga kutokana na nguvu ya rushwa, wakachukua
nafasi za ngazi ya chini za uongozi, uchaguzi wa taifa hauwezi kuiepuka
rushwa, hii ni hatari kubwa kwa chama chetu,” alisema.
Aliongeza, “bado ninaamini kwamba, kwa yaliyotokea hasa ngazi ya wilaya
na mikoa, watu wakachaguliwa kupitia rushwa, hata huko juu (Taifa) hali
itakuwa hivyo hivyo.”
Lugora alisema rushwa itakapotumika katika hitisho la uchaguzi ngazi ya
taifa, itakuwa ishara ya chama hicho ‘kuzama shimoni’ pindi Uchaguzi
Mkuu wa 2015 utakapofanyika.
“Tunakipenda chama chetu, lakini watu waliofanikisha kujipanga kwa
kutumia rushwa ili waingie madarakani, wananifanya niamini kwamba 2015
tunaelekea shimoni,” alisema.
NAPE ASEMA MAMBO YAPO SHWARI
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, aliiambia NIPASHE
Jumamosi jana kuwa, kiwango cha malalamiko ya rushwa katika chaguzi hizo
ni kidogo na kwamba mambo yapo shwari ndani ya chama hicho.
Nape aliyesisitiza kutaka apewe takwimu kuhusu idadi ya malalamiko
yaliyotolewa kuhusu rushwa ndani ya chaguzi hizo, alisema suala hilo
linakuzwa na vyombo vya habari.
“Tumia mshahara wako vizuri si kukurupuka, fanya utafiti badala ya
kusema kuna ongezeko la malalamiko ya rushwa kwa chaguzi za CCM, suala
hilo mnalikuza nyie wa vyombo vya habari,” alisema.
Nape alisema CCM imepokea malalamiko kutoka wilaya nane kati ya 161
zilizopo, ikiwemo Hanang’, yaliyowasilishwa na Sumaye, hivyo kuwa
kiashiria kwamba mambo ni shwari katika chaguzi hizo.
MHADHIRI UDSM AMKOSOA NAPE
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Sayansi ya
Siasa na Utawala, Dk Benson Bana, amekosoa kauli ya Nape, akisema hata
kama rushwa ingekuwa kwa kiwango cha tone la maji, haifai kuwa sababu
ya kujivunia.
Dk Bana alisema rushwa ni adui wa
haki na kwamba inapotumika katika chaguzi, inakuwa sehemu yenye kuathiri
misingi ya dekomrasia.
Alisema kutokana na hali hiyo, CCM inapaswa `kutoikimbia’ rushwa, bali
kuikabili na kuhakikisha inaondoka katika chaguzi zake. “CCM wapiti
kanuni na taratibu zao ili kuhakikisha kuwa mianya yote ya rushwa
inazibwa,” alisema.
JK: RUSHWA INAIPELEKA CCM PABAYA
Wakati Nape akiamini kuwepo kiwango kidogo cha rushwa kwenye chaguzi za
CCM, Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, ametoa kauli zinazoashiria
kukithiri kwa tatizo hilo na athari zake kwa chama hicho.
Rais Kikwete amekaririwa akizungumza katika mikutano ya uchaguzi kwa
Jumuiya ya Wanawake (UWT) na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) akisema
rushwa inayoendelea kujitokeza ndani ya chaguzi hizo, inaweza kukiua
chama hicho.
Ingawa kauli hiyo inatofautiana na ile ya Nape, lakini inaunga mkono
hoja zilizowahi kutolewa na wana-CCM kadhaa hususan walioshindwa katika
nafasi mbalimbali za uongozi, wakilalamikia kushamiri kwa rushwa.
UTABIRI, VILIO KUHUSU RUSHWA NDANI YA CCM
Viongozi waandamizi na wanachama ndani ya CCM, walishakitahadharisha
chama hicho, kujipanga ili kukabiliana na matumizi ya ‘fedha chafu’
wakati wa chaguzi za ndani.
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, akiwa katika
ziara mkoani Kagera hivi karibuni, alitahadharisha kuwepo dalili za
rushwa kuathiri chaguzi za chama hicho.
Naye Sumaye, baada ya kushindwa na
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk Mary
Nagu, aliibua ‘kilio’ cha matumizi ya rushwa ya mtandao ndani ya CCM.
Sumaye aliyekuwa anawania ujumbe wa Nec kupitia wilaya ya Hanang’ mkoani
Manyara, alisema rushwa ilitumika kwa kiasi kikubwa kumfanya ashindwe.
Hata hivyo alisema hali hiyo ilijitokeza kwenye maeneo mengine ya nchi,
lengo likiwa kuwawezesha viongozi wenye nia ovu kushika madaraka.
No comments:
Post a Comment