Kocha Stewart Hall kutua Azam leo

Aliyekuwa kuwa kocha wa Azam, Stewart Hall, atawasili nchini leo kuanza kuifundisha tena timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kutwaa nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mrithi wake wakati akiondoka nchini, Mserbia Boris Bunjak.

Afisa Habari wa Azam, Jaffer Idd, alisema jana kuwa maamuzi ya kumrejesha kocha wao wa zamani ambaye alikuwa akiifundisha Sofapaka inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya yametokana na ushauri wa kiufundi walioupata kutoka kwa wadau mbalimbali wa timu hiyo.

Idd alisema kwamba Bodi ya Wakurugenzi ya timu hiyo ilifikia maamuzi hayo baada ya kuamua kuvunja mkataba wa Bunjak, ambaye alianza kuiongoza Azam tangu mwishoni mwa Julai mwaka huu.

Aliongeza kwamba Hall ambaye mwaka huu aliifikisha Azam kwa mara ya kwanza katika fainali za Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), ataanza kazi yake rasmi kesho wakati atakapoiongoza timu hiyo katika mechi yao dhidi ya Coastal Union kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Chamazi, Mbagala jijini Dar es Salaam.

BUNJAK ASHANGAA

Akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana, Bunjak alisema kuwa amesikitishwa na uamuzi wa kutimuliwa kwake Azam kwani hadi kufikia jana alikuwa hajapata maelezo ya kina kuwa ni kwanini amefungashiwa virago.

“Kesho (leo) napanda ndege kurejea kwetu (Serbia). Uamuzi huu umenishtusha sana kwa sababu tumecheza mechi nane bila kufungwa kabla ya kupoteza mechi moja dhidi ya Simba,” alisema Bunjak aliyekuwa ameambatana na kocha wa makipa aliyetimuliwa pia baada ya siku 25 tangu watue Oktoba 5, Torlakovic Slobodan. 

“Niamini, sijui sababu za kutimuliwa kwangu, lakini naamini watu wanaozunguka klabu ya Azam ndiwo wameshauri hivyo.

“Nimesikitishwa sana na uamuzi huu wa Azam kwani nilikuwa na ndoto za kuipeleka mbali timu yao.”

Aidha, Bunjak aliyekuwa na mkataba wa miaka miwili ya kuinoa Azam, hakusita kusifia wachezaji na uongozi wa klabu kwa kumpa ushirikiano wa kutosha katika muda wote aliokaa nao.

“Baada ya kupewa taarifa hizo jana (juzi) nilienda klabuni kuagana na wachezaji. Naushukuru uongozi kwa kutimiza kila kitu kilichomo katika mkataba wetu. Meneja wa Azam (Patrick Kahemele) amenilipa kila kitu na kunipatia tiketi ya ndege ya kuirejea Serbia,” alisema Bunjak huku akikataa kutaja kiasi alicholipwa kwa kile alichodai kuwa ni siri.

Kwa upande wake, Kahemele alisema jana kuwa wakurugenzi wamefikia uamuzi huo baada ya kutoridhishwa na kiwango cha timu yao tangu waikabidhi kwa kocha huyo.

Alisema wameamua kumrejesha Hall kwa kuwa wachezaji walikuwa wameshazoea mfumo wake wa ufundishaji na kwamba kocha huyo amewaahidi kujirekebisha kwa mambo mbalimbali aliyowakosea na kuamua kumtimua.

“Bunjak ni kocha mzuri, lakini mfumo wake unahitaji muda mrefu kuzoeleka kwa wachezaji wetu. Tumeamua kumrejesha Stewart na atatua kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kesho saa moja usiku,” alisema.

No comments:

Post a Comment