Simba,Yanga viwanjani leo
Ligi Kuu ya Soka
Tanzania Bara ambayo imefika kwenye raundi ya 11 ya mzunguko wa kwanza
itaendelea leo kwenye viwanja vitano tofauti ambapo timu 10 zitashuka
dimbani kuwania pointi tatu muhimu, zikiwamo za Simba na Yanga zilizo
kileleni mwa ligi hiyo.
Mechi nyingine ya ligi iliyotarajiwa kufanyika leo kati ya Ruvu Shooting
dhidi ya Prisons ya Mbeya imeahirishwa hadi itakapotangazwa baadaye
kufuatia ajali ya gari waliyoipata wachezaji wa Prisons wiki iliyopita
wakati walipokuwa njiani kuelekea jijini Tanga.
Vinara wa ligi hiyo, Simba, ambao waliwasili Morogoro jana saa 7:00
mchana, watakuwa wageni wa Polisi Morogoro katika mechi itakayofanyika
kwenye Uwanja wa Jamhuri wakati watani zao wa jadi, Yanga, wanaoshika
nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi watawakaribisha JKT Mgambo kwenye
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kocha wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic, aliliambia gazeti hili kwamba
wachezaji wake wako tayari kwa mechi hiyo ya ligi na jana jioni
walitarajiwa kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Jamhuri ili kuuzoea kabla
ya kushuka dimbani leo jioni.
Mserbia huyo alisema kwamba licha ya ushindani mkali wanaokabiliana nao
katika mechi zao za mikoani, Simba inataka kuendeleza kasi yake ya
kufanya vizuri na hatimaye kuendelea kubaki kileleni mwa msimamo na
kutowapa nafasi mahasimu wao, Yanga kuwashusha.
Alisema kwamba amewataka nyota wake kutoidharau Polisi Morogoro licha ya
kuonekana kuwa hawakufanya vizuri katika mechi zao zilizopita kwani
timu ya aina hiyo huwa ni hatari zaidi.
"Tunatarajia kushinda na nimewaeleza kuwa wasiidharau kwa sababu
haijashinda mechi yoyote tangu ligi ilipoanza," alisema kocha huyo.
Kocha Mkuu wa Yanga, Ernest Brandts, alisema kwamba kikosi hicho sasa kimeiva na kinataka kusonga mbele tu.
Brandts alisema kwamba kila siku amekuwa akiwakumbusha wachezaji wake
kupambana katika dakika zote 90 za mechi na kutoruhusu wapinzani
kukaribia lango lao.
Daktari wa timu hiyo, Juma Sufiani, alisema kuwa wachezaji, Kevin
Yondani, Said Bahanunzi na Didier Kavumbagu ambaye jana alirejea
mazoezini kuungana na wenzake, wako vizuri na maamuzi ya kucheza au
kutocheza yako kwa kocha Brandts.
Daktari huyo alimtaja beki Salum Telela ambaye aliteguka kifundo cha
mguu ndiye anayeendelea na matibabu kwenye Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili na hana nafasi ya kucheza mechi ya leo na ya Jumapili dhidi ya
Azam.
Mechi nyingine zitakazochezwa leo ni kati ya Toto Africans dhidi ya
Kagera Sugar kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba jijini Mwanza huku JKT Ruvu
wakiikaribisha African Lyon kwenye Uwanja wa Chamazi, Mbagala na jijini
Arusha, wenyeji JKT Oljoro nao wataikaribisha Mtibwa Sugar kwenye Uwanja
wa Sheikh Amri Abeid.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Arusha, kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky
Maxime, alisema kwamba timu yake haijapata matokeo mazuri hivi karibuni
lakini hali hiyo ni ya kimchezo kwa sababu wachezaji wamekuwa
wakipambana kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mchezo.
Maxime alisema kwamba wanaamini watazinduka na kurejesha kasi yao
kuanzia leo na watatumia vyema uwanja wa nyumbani katika mechi zote
zinazofuata.
Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwenye Uwanja wa Chamazi kwa
kuzikutanisha Azam inayoshika nafasi ya nne kwenye msimamo dhidi ya
Coastal Union iliyo kwenye nafasi ya pili.
No comments:
Post a Comment