Serikali ‘yaipiga stop’ Tanesco kupandisha bei ya umeme
Shirika la Umeme Nchini (Tanesco)
Wizara ya Nishati
na Madini imelizuia Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) kupandisha bei ya
umeme kama lilivyokuwa limepanga kufanya hivyo Januari, mwakani.
Waziri wa Wizara hiyo, Profesa Sospeter Muhongo, alisema hayo juzi
wakati akihojiwa kwenye kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na Kituo cha
Televisheni ya ITV.
“Kumekuwa na madai kwamba, Tanesco watapandisha bei ya umeme ifikapo
Januari 2013. Lakini nimewaelekeza Tanesco na Ewura (Mamlaka ya Udhibiti
wa Huduma za Nishati na Maji) wasipandishe bei ya umeme,” alisema
Profesa Muhongo.
Alisema ameielekeza Tanesco isipandishe bei kwa sababu katika deni la
dola za Marekeni milioni 250 inazodaiwa, serikali imekuwa ikilisaidia
kulipa.
Profesa Muhongo alisema hadi sasa serikali imekwishatoa dola za marekani
milioni 50 kupunguza deni hilo, ambalo limebaki dola za Marekani
milioni 200.
Alisema serikali imepunguza bei ya kuunganisha umeme wananchi ili
ifikapo mwaka 2015 asilimia 30 ya Watanzania wawe wanapata nishati hiyo
tofauti na sasa, ambapo wanaopata ni asilimia 18.4 tu.
Profesa Muhongo alisema wizara yake imejipanga kuongeza kiwango cha
uzalishaji wa umeme kifikie megawati 2,780 kutoka megawati 1,438
zinazozalishwa hivi sasa ifikapo mwaka 2015.
Alisema uzalishaji huo utaongezeka kutokana na mkakati uliopo wa
kuongeza vyanzo vya uzalishaji umeme na kwamba, hivi sasa matumizi ya
umeme kwa nchi nzima ni megawati 830.
“Mgawo wa umeme haupo na wala hautakuwapo, wengine wanaufurahia uwapo
kwa sababu zao binafsi za kibiashara na kisiasa. Lakini nawahakikishia
wananchi hakutakuwa na mgawo wa umeme,” alisema Profesa Muhongo.
Akizungumzia suala la gesi, alisema wizara yake imewasilisha sera ya
gesi katika Baraza la Mawaziri na rasimu ya sera hiyo imepelekwa kwa
wakuu wa mikoa ili wananchi waweze kutoa maoni yao kabla ya kupelekwa
bungeni Februari, mwakani.
Profesa Muhongo alisema rasimu ya sera hiyo imepelekwa katika mikoa,
ambayo gesi na mafuta inapatikana na, ambayo inatumia gesi hiyo kwa
wingi ni Lindi, Mtwara, Tanga, Pwani, Rukwa (Sumbawanga), Katavi, Mbeya
na Arusha.
No comments:
Post a Comment