Bomu laua watoto watano


  *Waliliokota na kuanza kulichezea
  *Ajali yaua watu wawili yajeruhi 20
Kamanda wa Oparesheni Maalum wa Jeshi la Polisi, Peter Mvulla, akiwa na bomu la kutoa machozi alilolichukua kutoka kwa mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kimnyaki iliyopo wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha jana. Bomu hilo lilirushwa kwa wanafunzi hao na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) bila ya kulipuka na kuwaepusha na madhara ambayo yangeweza kutokea.
Watoto watano wamekufa baada ya kulipukiwa na bomu la kutupa kwa mkono walilookota wakati wakikusanya vyuma chakavu wilayani Karagwe Mkoa wa  Kagera.

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Philip Kalangi, alithibitisha kutokea tukio hilo jana asubuhi katika Kijiji cha Rugarama Kata ya Iyande wilayani humo wakati wakichezea bomu hilo nyumbani ambalo liliokotwa juzi na Evadius Robert (17) akidhani kilikuwa chuma chakavu.

Aliwataja watoto  kuwa ni Fenias Frank (3);  Faraji Frank (1); Edgar Gidion (15); Faustin Alfonce (17) na Patric Kamali (12).

Alisema watalaam wa mabomu wa Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) walifika eneo hilo kufanya uchunguzi  ili kubaini bomu hilo lilitoka wapi hadi kufika hapo.

Aliwataka wakazi wa eneo hilo kuacha kuokota kitu wasichokijua ambacho kinachofanana na chuma ili kuepuka majanga ya kulipukiwa na mabomu kama yamebakia sehemu hizo.

TAARIFA ZA AWALI

Taarifa za awali kabla Kamanda Kalangi kuzungumza na NIPASHE jana jioni, zilieleza kuwa watu saba wakiwamo wanne wa familia moja, wakazi wa kijiji hicho wamekufa kwa kulipukiwa na  bomu.

Taarifa hizo kutoka wilayani Karagwe zilieleza kuwa tukio hilo lilitokea jana  saa nne asubuhi kijijini hapo na kusababisha vifo vya watu saba wakiwa watoto chini ya miaka 18.

 Waliotajwa kufa o ni  Eladius Robert (15), Fenius Frank (3), Faraja Frank (1), Scatus Kamali (15), Nelson Alphonce (14), Edger Gidion (14) na mmoja ambaye jina lake halikufahamkika, lakini alikadiriwa kuwa na umri wa miaka 17.

Imeelezwa kuwa watoto hao walikuwa katika shughuli ya kuokota vyuma chakavu katika kijiji hicho kwa ajili ya kuuza kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na ununuzi wa vyuma chakavu wilayani humo.

Mmoja wa wazazi wa watoto hao, Frank Robert (35),  mkazi wa kijiji hicho, aliwaambia waandishi wa habari kuwa watoto hao walionekana asubuhi wakiokota vyuma chakavu kwa ajili ya kuuza na kuwa ghafla alisikia mlipuko wa kishindo ambao ulisababisha vifo vyao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Luteni Kanali  Benedict Kitenga, alithibitisha kutokea kwa vifo hivyo  ambavyo vinadaiwa kusababishwa na bomu la kutupwa kwa mkono.

 

Kitenga  aliwataka wakazi wa wilaya za Karagwe na Kyerwa hususani zile zinazopakana na nchi jirani kuwa waangalifu.

WAWILI WAFA, 20 WAJERUHIWA

Watu wawili wamefariki papo hapo na wengine 20 kujeruhiwa vibaya katika ajali ya lori aina ya Canter walilokuwa wakisafiri  kutoka Muheza mjini kuelekea Tarafa ya Amani, mkoani Tanga.

Ajali hiyo ilitokea jana  jioni katika maeneo ya Daraja Mbili  kijiji cha Ubembe, Kata ya Nkumba wilayani Muheza na kuthibitishwa na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Tanga, Jafari Mohamed.

Inadaiwa kuwa Canter hilo lenye namba za usajili T 497 ATU lilipata ajali hiyo wakati likiwa limebeba zaidi ya watu 30 na mizigo.

Waliokufa ni  Omari Salim, mkazi wa Kazita Amani na Renard Yusuph (7). Miili yao imehifadhiwa chumba cha maiti cha Hospitali Teule ya Wilaya ya Muheza.

Waliojeruhiwa ni Zena Kasimu; Zuena Husseni; Mele Yohana; Salimu Luka; Mariam Mchongoma; Moza Omari; Rehema Omari; Happy Mkai; Mathayo Kusaga; Sadiki Omari; Emanuel Bakari na Godfrey Pesambili.

Wengine ni Chedi Hassan; Omari Juma; Joseph Logasila; Ibarahimu Rashidi;  Ramadhani Ally; Ally Abdallah; Ramadhani Athumani na Ibarahim Makame.

Kundi la watu jana jioni walifurika katika hospitali hiyo kuwatafuta ndugu zao ambao walikuwa wakisafiri kwa lori hilo huku vilio vikitawala.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Ibrahim Matovu; Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Amiri Kiroboto; Mkuu wa Wilaya hiyo, Subira Mgalu na madiwani walifika hospitalini hapo kuwajulia hali majeruhi hao na kuwapa pole.

No comments:

Post a Comment