Matokeo Uchaguzi Wa Madiwani CCM Na CHADEMA Wachuana Vikali
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeendelea kukipa wakati mgumu
Chama cha Mapinduzi (CCM) katika siasa, ambapo kwenye matokeo ya udiwani
katika uchaguzi uliofanyika leo, chama hicho kimefanikiwa kutetea
kata zake na kunyakua nyingine za CCM.
Hata hivyo uchaguzi huo ambao ulifanyika kwenye kata 29 katika
halmashauri mbalimbali nchini, umemalizika huku vurugu kubwa zikitawala
na kusababisha wafuasi wa vyama hivyo kuumizana.
Hadi sasa matokeo ya kata 14 yanaonyesha kuwa CCM
ilikuwa imefanikiwa kurejesha kata zake saba, huku CHADEMA ikinyakua
kata sita, ambapo mbili zilikuwa za kwao na nne imewanyang’anya CCM na
CUF ikiwa na kata moja.
Matokeo ya udiwani katika baadhi ya kata yalikuwa yakiendelea kutolewa
huku CHADEMA ikiendelea kuikaba CCM kwa kuzitwaa baadhi ya zilizokuwa
kata zake.
Jijini Arusha katika Kata ya Daraja Mbili, CCM ilipoteza kata hiyo
kwa CHADEMA iliyozoa kura 2,192 dhidi ya 1,315 za chama tawala.
CHADEMA wameweza kuzirejesha kata zao mbili za Nangerea jimboni
Rombo, ambapo mgombea wao Frank Sarakana alijizolea kura 2,370 dhidi ya
1,134 za Dismas Silayo wa CCM pamoja na ile ya Mtibwa, mkoani Morogoro.
Wilayani Sikonge katika Kata ya Ipole, CCM walipoteza kata hiyo kwa
CHADEMA iliyopata kura 577 dhidi ya 372 za washindani wao, na vilevile
kuitwaa kata nyingine ya Lengali wilayani Ludewa iliyokuwa ya CCM.
CHADEMA pia ilikuwa ikiongoza katika Kata ya Mpwapwa, mkoani Dodoma, hadi tunakwenda mitamboni usiku.
Nayo CCM ilifurukuta kwa kuzirejesha kata zake za Msalato ya mkoani
Dodoma, Bang’ata ya Arumeru Magharibi kwa kuwa 1,177 dhidi ya 881 za
CHADEMA, Mletele ya Songea CCM ilishinda kwa kura 950 na CHADEMA ilipata
295.
Pia CCM iliweza kutetea kata zake za Mwawaza mjini Shinyanga,
Lwenzela mkoani Geita, Bungala wilayani Kahama na Bagamoyo mkoani Pwani
kwa kuibwaga CHADEMA wakati Chama cha Wananchi (CUF) kilishinda kata
ya Newala.
No comments:
Post a Comment