Naibu Waziri wa wizara hiyo, Philipo Mulugo
Maafisa wa Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, wametoboa siri hatua ya Naibu Waziri wa
wizara hiyo, Philipo Mulugo, kukosea kutaja Zimbabwe badala ya Zanzibar
kama kisiwa kilichounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wakizungumza na NIPASHE jana, walisema pamoja na kwamba aliteleza kutaja
Zimbabwe akimaanisha Zanzibar, kimsingi suala hilo linakuzwa na baadhi
ya mahasimu wake wa ndani na nje wa kisiasa.
Walisema mahasimu wake hao ni wale ambao kwa namna moja au nyingine,
wameathirika kutokana na misimamo yake anayoitoa hususan katika suala la
kuzifunga shule na kuwatimua watendaji wanaobainika kushindwa
kutekeleza majukumu yao.
Mmoja wa maafisa hao ambaye aliambatana na Naibu Waziri huyo nchini
Afrika Kusini, Enock Barnabas, alisema kimsingi makosa yaliyofanywa na
Mulugo ni ya kibinadamu tu ambayo yanaweza yakafanywa na mtu yeyote.
Hata hivyo, alisema wameshangazwa kuona suala hilo linavyokuzwa na baadhi ya watu.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ufundi, David Kazuva, alisema
ufafanuzi uliotolewa na Naibu Waziri kuhusu suala hilo, umeeleweka kwa
jamii na wanaoendelea kulijadili wana lao jambo.
Maafisa hao walimtaka Mulugo kutokatishwa tamaa na watu wanaompiga vita
na badala yake aendelee kutekeleza majukumu yake kwa sababu baadhi ya
watu hawaangalii mafanikio ya mtu bali huangalia pale anapofanya makosa
ndipo wapate cha kusema.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi ambao wamechangia hoja zao kwenye
mitandao ya kijamii, walisema viongozi wengi wanaosafiri nje na ndani ya
nchi, wamekuwa wakifanya makosa madogo kama hayo wanapowasilisha
taarifa mbalimbali za serikali.
“Mti wenye matunda ndiyo upigwao mawe, tunamfahamu Mheshimiwa Mulugo kwa
utendaji wake kazi na ndiyo maana watu wanataka kumkatisha tamaa kwa
maslahi yao binafsi,” alisema Brown John.
Katika hatua nyingine, kampuni tano za nje zimekubali kuja kuwekeza
Tanzania katika sekta ya elimu upande wa ufundi na utaalam wa kompyuta.
Kampuni hizo zinatarajiwa kuja nchini kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Mulugo, kati ya Oktoba 4 na 8, mwaka huu, alikwenda mjini Capetown
nchini Afrika Kusini na maafisa wengine wanne wa wizara hiyo kuhudhuria
mkutano wa kimataifa uliokuwa unajadili masuala la elimu ya ufundi
ambapo kila nchi iliwasilisha taarifa ya elimu ya nchi yake kuelezea
changamoto na mafanikio yake.
Mkutano huo ambao uliwashirikisha mawaziri wa elimu na sayansi wa nchi
za Afrika, ulilenga kila nchi ieleze changamoto zinazokabiliana nazo
katika sekta ya elimu ili shirika la Kimataifa la African Brains
liangalie uwezekano wa kuwekeza.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment