Hillary Clinton ziarani Algeria

Wapiganaji wa kiisilamu Kaskazini mwa Mali

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hilary Clinton yuko nchini Nigeria, kuzungumzia swala la kukithiri kwa tisho la usalama kutokana na makundi ya wapiganaji wa kiisilamu katika nchi jirani ya Mali.

Mapema mwezi huu, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, ilipitisha azimio linalotoa mwanya wa kikosi cha pamoja cha muungano wa Afrika kuzima uasi Kaskazini mwa Mali.

Algeria ni nchi muhimu katika eneo la Sahel kwa misingi ya kijeshi na kuungwa mkono kwake ni muhimu katika kuingilia kati mzozo wa Mali.

Wapiganaji wa kiisilamu kutoka Algeria wanasemekana tayari wameingia nchini Mali kusaidia harakati za wapiganaji wa Tuareg.

Aidha wapiganaji wa Mali,waliotumia mwanya wa usalama wakati wa mapinduzi yaliyofanyika mwezi Mei mjini Bamako kudhibiti Kaskazini mwa Mali, wana uhusiano na kundi la al-Qaeda.

Idadi yao pia imeongezeka kwa kusaidiwa na wapiganaji waliokuwa wanamuunga mkono kiongozi wa Libya aliyeuwawa hayati, Muammar Gaddafi.

Balozi wa Marekani aliyesafiri na Clinton alisema kuwa swala la Mali limepewa kipaombele katika ajenda ya mazungumzo kati ya Bi Clinton na rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika pamoja na waziri wa mambo ya nje Mourad Medelci.

Algeria ilikuwa imeelezea wasiwasi kuhusu mipango ya shirika la ECOWAS, kutuma wanajeshi elfu tatu kupambana na wapiganaji Kaskazini mwa Mali kwa hofu ya kutikisa uthabiti wa eneo hilo.

Lakini Algeria ambayo ina jeshi kubwa zaidi katika eneo la Sahel, imekuwa ikionyesha dalili ya kutaka kuingilia kati mzozo huo.

Wiki jana kulikuwa na ripoti za makundi ya wapiganaji wa kigeni kutoka Ageria na Magharibi mwa jangwa la Sahara,kuanza kuwasili katika ngome za wapiganaji ya Timbuktu na Gao.

No comments:

Post a Comment