Ni vita ya visasi


Wachezaji wa Yanga wakifanya mazoezi ya kukimbia
WAANDISHI WETU

NI vita ya visasi! Ndivyo unavyoweza kulizungumzia pambano la watani wa jadi Yanga na Simba litakalipogwa kesho Jumatano usiku kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwani baada ya visa vingi vya nje ya uwanja, mambo yatakuwa hadharani. Mechi hiyo ni ya Ligi Kuu Bara.

Katika msimamo wa ligi, Wekundu wa Msimbazi wapo kileleni wakiwa na pointi 12 kibindoni ikifuatiwa na Azam yenye pointi 10. Yanga inashika nafasi ya saba ikiwa na pointi nne.

Pambano hilo litakalorushwa laivu kuanzia saa moja usiku na Kituo cha Televisheni cha SuperSport cha Afrika Kusini linasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka kutokana na fitina, mikasa na vituko vingi vilivyotokea katika siku za karibuni kabla ya mchezo wenyewe.

Uwepo wa SuperSport nao unatarajiwa kuwa burudani kwani kamera zao ziliwahi kusaidia utata wa bao Mei 5, 2011 baada ya mwamuzi Oden Mbaga kukubali bao la kusawazisha la Mussa Hassan 'Mgosi' wa Simba baada ya marudio ya picha za SuperSport. Timu hizo zilifungana 1-1.

Kuna mambo ya nje ya uwanja ambayo yameongeza uhasama baina ya timu hizo katika siku za karibuni.

Ukiachia kupigania pointi na kusafisha njia ya kutwaa ubingwa wa Bara, kila upande utakuwa unasaka ushindi kwa udi na uvumba ili kutuliza presha za mashabiki na wanachama wake.

Timu hizo zimeingia mafichoni kujiandaa na mchezo unaotarajiwa kuwa mkali.

Yanga, ambao watakuwa wenyeji wa mchezo huu, wameingia kambini katika Hoteli ya Double Tree iliyoko Masaki, jijini Dar es Salaam. Hoteli hiyo imegeuzwa kuwa 'chimbo' lao katika siku za karibuni.

Masaki iko pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam ikijulikana kwa ukimya wake kutokana na eneo hilo kukaliwa na watu wenye uwezo wa kifedha na viongozi wa taasisi za Serikali na binafsi.

Simba nao wamejichimbia Zanzibar katika eneo la Mbweni. Simba tangu miaka ya 1990 wana kawaida ya kujichimbia huko na kuburudika na 'marashi ya karafuu'.

Fomesheni za makocha

Kocha wa Yanga, Mholanzi Ernie Brandts ataingia kuivaa Simba akiwa na malengo ya kumaliza hesabu mapema kwa kupata bao la fasta.

Kocha wa Simba, Milovan Cirkovic, raia wa Serbia ameahidi timu yake kuibuka na ushindi.

Brandts atasimama kwenye benchi la ufundi kukiongoza kikosi chake hicho kipya katika mchezo huo na Mjumbe wa Bodi ya Udhamini ya Yanga, Seif Ahmed 'Magari' amethibitisha kuwa atakaa kwani shughuli za kupata kibali cha kazi, ilianza tangu aliposaini mkataba, Jumamosi iliyopita.

Katika mchezo huo, Brandts amekuna kichwa kuhakikisha anapata kikosi bora kitakachofanya vizuri.

"Nimewaona Simba (walipocheza na Prisons) ni timu ngumu inahitaji umakini kuwafunga lakini ninachowaahidi mashabiki ni pointi tatu.

"Tutaingia uwanjani tukiwa na malengo ya kupata bao la fasta hilo ni jambo muhimu kwetu ili kujiwekea mazingira mazuri mchezoni," alisema Brandts ambaye kwa miaka miwili aliyoifundisha APR aliwapa ubingwa wa Ligi Kuu Rwanda.

Yanga inaingia ikiwa na kocha huyo mpya, Brandts ambaye ni muumini mzuri wa fomesheni ya 4-4-2 na 4-3-3, sawa na anayotumia Milovan.

Awali, Yanga chini ya kocha Tom Saintfiet ilikuwa ikitumia 5-1-2-2 na 4-4-2 akijihami zaidi, kwa hali hiyo itabidi, Brandts kutumia muda mwingi atakapokuwa kwenye benchi la ufundi, kushauriana na msaidizi wake, Fred Minziro ambaye anawajua vizuri wachezaji wa Yanga ili kwenda sawa.

Naye Kocha wa Simba, Milovan alisema: "Tumepania kushinda mchezo huu kwa sababu tuna timu imara japo itakuwa mechi ngumu kutokana na ushindani uliopo kwa timu hizo.

"Nimewaona Yanga walipocheza na African Lyon ni wazuri. Hata hivyo, sijali kwa sababu ninachoangalia ni timu yangu kuona namna gani tutashinda."

Kwa upande wa Milovan ambaye anapenda kujaza viungo wengi kikosini mwake, atakuwa hana shida kwani amekuwa na kikosi hicho kwa kipindi kirefu na anawajua zaidi wachezaji wake.

Vita ya mastaa uwanjani

Pamoja na watu kuzungumzia zaidi masuala ya nje ya uwanja kuhusu mchezo huo, burudani kubwa inatarajiwa uwanjani.

Sehemu ya kiungo inatarajiwa kuwa kivutio kutokana na umahiri wa kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima 'Fabregas' lakini atakuwa na kazi pevu dhidi ya Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba na Ramadhan Chombo 'Redondo' wa Simba.

Pia mastraika wa timu zote mbili watakuwa na pilika pilika kwani Felix Sunzu, Haruna Moshi na Ngassa watakuwa wanasaka upenyo kuwapita mabeki wa Yanga, Mbuyu Twite, Nadir 'Cannavaro' na Kelvin Yondani.

Mabeki wa Simba, Kapombe na Nyosso watapaswa kuwa macho kuwaangalia Saidi Bahanuzi, Didier Kavumbagu na Hamisi Kiiza wa Yanga.

Majeruhi na kadi

Simba itawakosa straika tegemeo Emmanuel Okwi na beki wa kushoto, Amir Maftah wanaotumikia adhabu za kuonyeshwa kadi nyekundu.

"Tutakuwa bila ya Okwi na Maftah lakini Simba ina wachezaji wengi wazuri ambao wataziba mapengo yao.

"Kama kocha najua namna nitakavyowatumia wachezaji wangu katika mchezo huo," alisema Milovan.

Akimzungumzia, Haruna Moshi 'Boban' ambaye alianza mazoezi ya pamoja na kikosi hicho jana Jumatatu kutokana na kusumbuliwa na malaria, Milovan alisema anafurahi kuimarika kwa afya yake na atamwangalia hali yake hadi kesho Jumatano kujua namna atakavyomtumia.

Kulikuwa na uvumi kuwa Sunzu na Kapombe wanaweza kukosa mchezo huo mazoezini lakini wako fiti tayari kuingia dimbani.

Ngassa, Yondani dhidi ya timu zao za zamani

Nyota wawili Mrisho Ngassa watavaana na timu zao za zamani kwa mara ya kwanza na kinachosubiriwa ni mapokezi watakayopata kutoka kwa mashabiki wao wa zamani.

Ngassa alikuwa Yanga kabla ya kuhamia Azam msimu wa 2011/12 ambako ameondoka na kuibukia Simba.

Winga huyo machachari aliwahi kuibusu jezi ya Yanga wakati akiwa Azam lakini cha ajabu akaibukia Simba na kudai kuwa ni timu anayopenda tangu utotoni.

Yondani naye anapaswa kujiandaa na mapokezi ya mashabiki wake wa zamani kwani usajili wake ulisababisha mvutano kati ya timu yake ya zamani ya Simba na Yanga.

Kumbuka Yondani alitoroshwa kwenye kambi ya Taifa Stars na wakatumia udhaifu wa mkataba wake na Simba kumsajili.

Mbuyu Twite kikangooni

Twite atakuwa na kazi ngumu kwani atakumbana ana kwa ana na Simba, ambao alichukua fedha yao ya usajili halafu baadaye akawatosa.

Yanga walitumia ujanja kumnasa Twite baada ya kusikia Lupopo ya Congo ndiyo ilikuwa ikimliki mchezaji huyo na si APR.

Simba ilikuwa tayari imempa kiasi cha Dola 30,000 (Sh 45 milioni) ili kumsajili lakini ilifanya kosa la kutozungumza na timu yake ya zamani ya Lupopo.

Vikosi

Simba

Juma Kaseja atasimama wakati beki wa kulia ni Said Nassor 'Cholo', beki ya kushoto ni Paul Ngalema. Amri Kiemba atacheza kiungo mkabaji na Mwinyi Kazimoto atacheza kiungo mshambuliaji wakati winga ya kulia itachezwa na chipukizi, Edward Christopher na ya kushoto ni Mrisho Ngassa, washambuliaji wa kati ni Felix Sunzu na Ramadhan Chombo 'Redondo'.

Yanga

Kipa ni Yaw Berko, beki ya kulia atacheza Mbuyu Twite. Beki ya kushoto ni Stephano Mwasyika na mabeki wa kati ni Kelvin Yondan na Nadir Haroub 'Cannavaro' wakati Athuman Idd 'Chuji' atacheza kiungo mkabaji na Haruna Niyonzima 'Fabregas' atacheza kiungo mshambuliaji.

Kinda, Simon Msuva atacheza winga ya kulia na Khamis Kiiza atacheza winga ya kushoto wakati washambuliaji wa kati ni Didier Kavumbagu na Said Bahanuzi.

Visasi mpango mzima

Si siri mashabiki wa Yanga wataingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu mbaya kutokana na ukweli kuwa timu hizo zilipokutana kwa mara ya mwisho Mei 6, mwaka huu, timu yao ilibugia mabao 5-0.

Kitendo hicho kimekuwa kikiwasonenesha viongozi wa Yanga kwani wakitaka kuwatania basi wale wa Simba wanaonyesha ishara ya vidole vitano.

Yanga wamepania kulipa kisasi na ishara zao zilionekana mapema kwa kitendo chao cha kuwadhoofisha Simba kwenye usajili.

Viongozi wa Yanga wawalizidi kete kwa kumsainisha Yondani na Mbuyu Twite wakitumia udhaifu wa Simba kwenye masuala ya mikataba.

Yanga baada ya mafanikio hayo ya nje ya uwanja,itataka kudhihirisha kuwa ina kikosi cha kutisha.

Umafia wa Yanga ulimfanya Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage kuangua kilio mbele ya waandishi wa habari. Kutokana na hali hiyo ni wazi viongozi wa Simba watakuwa na dhamira ya kulipa kisasi.

Simba itataka kudhihirisha kuwa pamoja na umafia waliofanyiwa, bado wana ubavu wa kuinyanyasa Yanga.

Mechi za Oktoba ngoma droo

Pambano hilo linafanyika Oktoba na kufanya kuwapo kwa idadi ya mechi 12 zilizokutanisha timu hizo mbili katika kipindi hicho.

Tangu mwaka 1979, timu hizo zimekabiliana mara 12 Oktoba, Yanga ikiibuka kidedea mara sita sawa na wapinzani wao Simba. Timu hizo zimetoka sare mara sita.

Yanga iliifunga Simba mabao 3-1(Oktoba 20, 1990), 2-1 (Oktoba 9, 1991), 1-0 (Oktoba 23, 1996), 1-0 (Oktoba 26, 2008), 1-0 (Oktoba 16, 2010) na 1-0 (Oktoba 29, 2011).

Simba iliisulubu Yanga mabao 3-1 (Oktoba 7, 1979), 3-0 (Oktoba 4, 1990), 1-0(Oktoba 27, 1992), 2-1(Oktoba 4, 1995)., 1-0 (Oktoba 24, 2007) na 1-0 (Oktoba 31, 20 09).

Timu hizo zimetoka nguvu sawa kwenye mechi mwezi huu zilizofungana mabao 1-1(Oktoba 11, 1997) na 0-0(Oktoba 29, 2006).

Acha tu Simba mechi za usiku!

Ukiangalia rekodi za mechi za usiku baina ya timu hizo, utagundua kuwa Simba ndio wameibuka kidedea mara nyingi zaidi.

Timu hizo zimekabiliana mara tano usiku na Simba imeibuka na ushindi mara nne.

Hata hivyo, Yanga ilikuwa timu ya kwaza kumfunga mpinzani wake usiku wakati timu hizo zilipokutana Januari, 1975 katika fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Yanga ilishinda 2-0 kwa mabao yaliyofungwa na wakali wake wakati huo, Sunday Manara na Gibson Sembuli.

Simba pia iliiliza Yanga 5-4 kwa penalti mwaka 1992 kwenye fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, ilishinda 1-0 (Ligi Kuu ya Muungano Oktoba 27, 1992) mabao 2-0 (Kombe la Mapinduzi, Januari 12, 2011) na mabao 2-0 (Ngao ya Hisani-Agosti 17, 2011).

Makocha wapya kuanzia kazi kwa Simba

Yanga imekuwa haina simile na makocha wake kigeni kwani kila mambo yanapokwenda kombo wamekuwa wakiwatimua.

Kibaya zaidi kuna baadhi yao kama Mserbia Kosta Papic, ambaye alikalia benchi la ufundi la timu hiyo kwa mara ya kwanza Oktoba 31, 2009 wakati wa mechi dhidi ya Simba baada ya kukabidhiwa timu na Mserbia mwenzake Dusan Kondic.

Papic, hata hivyo, alipoteza mchezo huo baada ya timu yake kufunga bao 1-0.

Mserbia huyo aliondoka mwaka 2010 lakini alirejea Tanzania mwaka jana na alianza kuinoa kwenye mechi na Simba, Oktoba 29, 2011.

Papic, hata hivyo, hakurudia makosa kwani aliiongoza Yanga kushinda bao 1-0 katika mchezo huo.

Presha ya viongozi

Pambano hilo lina umuhimu mkubwa kwa viongozi wa timu hizo kwa matokeo mabaya yanatosha kabisa kuwaondoa viongozi wake madarakani.

Mwenyekiti wa zamani wa Yanga, Lloyd Nchunga alionyeshwa mlango na wanachama baada ya timu yake kucharazwa 5-0 na Simba kwenye mechi ya ligi iliyopigwa Mei 6, mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Kutokana na hali hiyo, uongozi mpya wa Yanga ulichaguliwa Julai na pambano hilo ni majaribio makubwa kwao.

Uongozi wa Simba chini ya Ismail Aden Rage utatumia pambano hilo kudhihirisha kuwa bado uko kamili licha ya kupigwa na dhrouba nyingi za nje ya uwanja na wapinzani wao.

Kuwapoteza Kelvin Yondani na Mbuyu Twite waliosajiliwa Yanga kuliitikisa Simba.

Kiingilio na mwamuzi

Kiingilio cha chini kwenye mechi hiyo ni Sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani. Watazamaji watakaoketi kwenye viti vya rangi watalipa Sh. 7,000. Sh. 10,000 ni kwa viti vya rangi ya chungwa wakati VIP C itakuwa Sh. 15,000.

Kwa upande wa VIP B, tiketi ni Sh. 20,000 na VIP A kiingilio kitakuwa Sh. 30,000.

Wakati huo huo, mwamuzi Mathew Akrama kutoka Mwanza ndiye atakayechezesha mechi hiyo. Waamuzi wasaidizi ni Samuel Mpenzu kutoka Arusha na Ephrony Ndissa wa Dar es Salaam wakati mwamuzi wa mezani ni Oden Mbaga pia wa Dar es Salaam.


Habari hii imeandaliwa na Doris Maliyaga, Calvin Kiwia na Samson Mfalila.

No comments:

Post a Comment