Pembe za mabilioni zamakatwa jijini Dar


  *Zakutwa kwenye nyumba jijini Dar
  *Zilikuwa zikisafirishwa kwenye jeneza
Baadhi ya watuhumiwa wanaodaiwa kukutwa na meno ya tembo katika eneo la Kimara Stop Over Jijini Dar es Salaam wakiwa chini ya ulinzi wa polisi. Nyuma yao (kwenye gari) ni baadhi ya meno hayo yenye thamani ya Sh. Bilioni 2.2

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limekamata shehena ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh. bilioni 2.15.

Aidha, watu wanne wanashikiliwa kwa tuhuma za kukutwa na shehena hiyo.


Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Suleiman Kova, jana aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kwamba, shehena hiyo ni vipande 214 vya meno ya tembo na mifupa mitano ya mnyama huyo yenye uzito wa kilo 450.6.


Alisema watuhumiwa hao walikamatwa eneo la Kimara Stop Over juzi baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kwamba kuna nyumba inashukiwa  kuwa na mali zilizoibiwa pamoja na nyara za serikali.


Kamanda Kova aliongeza kuwa, baada ya Jeshi hilo kupata taarifa lilijipanga na kuipekua nyumba hiyo aliyopanga Peter Kami ambaye anaishi pamoja  na Leonida Kabi na kukuta vipande 214 vilivyokuwa vimehifadhiwa kwenye chumba kimojawapo.


Alisema meno hayo yalikutwa yakiwa yamehifadhiwa kwenye magunia 12 huku yakiwa yamefunikwa kwa bendera ya Taifa.


“Pamoja na meno hayo, pia zilikutwa pembe za ng’ombe 10 zikizokuwa zimeshindiliwa pamoja na chokaa, pamoja na mifupa ya tembo mitano, yenye kilo 450.6,” alisema Kova.


Aidha, Kamanda Kova aliwataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni pamoja na dereva wa daladala aliyekuwa akijifanya kuwa ni ofisa wa polisi aliyejulikana kama Polisi Simoni (42), Charles Wainaine (41), mkazi wa Rombo Tarakea, ambaye ni ndugu yake na Peter Kabi, ambao wote ni Wakikuyu kutoka nchini Kenya.


Kamanda Kova alifafanua kwamba uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa watuhumiwa hao ni wahalifu wazoefu katika matukio ya mtandao wa ujambazi, usafirishaji, pamoja na umiliki wa nyara za serikali.


“Mpango wa siri uliokuwepo ni kutumia gari aina ya Coaster, iliyokuwa iendeshwe na dereva Polisi Simon na kuweka jeneza lenye meno hayo na kulifunika na bendera ya Taifa ili ionekane wanasafirisha maiti ya mtu maarufu serikalini kwa lengo la kuvihadaa vyombo vya dola,” alisema Kamanda Kova.


Kwa mujibu wa Kova, mtuhumiwa Leonida Kabi, anashikiliwa kwa kosa jingine ambalo ni kumshawishi askari aliyezikamata nyara hizo kwa kutaka kumpa rushwa ya Sh. milioni  15, na kuahidi kuwaongezea kiasi kingine siku ya pili yake.


Aidha alisema kuwa uchunguzi wa kina utafanyika ili kubaini mtandao mzima wa wizi wa nyaraka za serikali hapa nchini pamoja na nchi za Kenya na Mashariki ya mbali na popote duniani ili kukomesha uhalifu huo.


Watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.


Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, kiasi hicho cha meno ya tembo ni sawa na tembo 91 waliouawa.


Aidha, kukamatwa kwa meno hayo kunakuja siku moja tu baada ya Waziri Kivuli wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa, kueleza kwamba mwendelezo wa matukio ya kuuawa kwa tembo ni matokeo ya kuwalinda majangili badala ya kuwachukulia hatua.


Akizungumza na waandishi wa habari juzi jijini Dar es Salaam Mchungaji Msigwa alimshauri Rais Jakaya Kikwete kuingilia kati na kuvunja mtandao wa ujangili ili kunusuru wanyamapori na maliasili nyingine za Taifa.


Mchungaji Msigwa ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), alisema mpaka sasa ni miezi mitatu tangu alipowasilisha taarifa za ujangili bungeni na kumtaka Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, achukue hatua dhidi ya majangili hao na matokeo yake amewaajibisha watu watatu wa Idara ya Wanyamapori huku watuhumiwa wakubwa wakiachwa jambo ambalo alidai ni hatari na kusababisha idadi ya wanyama kupungua kila wakati.


Alisema wiki iliyopita pembe za ndovu zenye uzito wa tani nne kutoka Tanzania na Kenya zenye thamani ya Sh. bilioni 2.5 zimezipotiwa kukamatwa na vyombo vya usalama vya mamlaka ya Jiji la Hong Kong.


Katika Mkutano wa Bunge uliopita, Kambi ya Upinzani bungeni pamoja na maoni ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliwataja vinara wa ujangili akiwemo Bryson Baloshingwa ambaye ni kiongozi wa mtandao wa ujangili kwa kufadhili uwindaji wa faru na biashara haramu ya meno ya tembo; uharamia unaofanyika katika hifadhi za Serengeti, Katavi, Tarangire, Ziwa Manyara na Ngorongoro.


Alisema Baloshingwa anafadhili pia majangili wanaoua wanyama katika mapori ya akiba ya Ugalla, Rungwe, Moyowosi na Maswa.


Alisema inashangaza kwamba wafadhili na majangili wanafahamika kwa majina lakini hawachukuliwi hatua na pindi wanapokamatwa hufunguliwa kesi rahisi zenye dhamana hivyo huachiwa kwa dhamana.


“Usalama wa tembo uko hatarini kutokana na serikali kutochukua hatua dhidi ya ujangili wa tembo pamoja na taarifa hizi kuwepo serikalini na viongozi wa CCM kushiriki katika ujangili," alisema.


WATUHUMIWA MAUAJI YA BARLOW


Wakati huo huo, Jeshi la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeeleza kwamba watu waliomuua aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Liberatus Barlow, walikimbilia jijini humu na kufanya uhalifu kabla ya kukamatwa.


Kamanda Kova alisema watu hao ni watuhumiwa wakubwa wa ujambazi wa kutumia silaha nchini na hususani katika majiji ya Dar es Salaam na Mwanza.


WATUHUMIWA SUGU MBARONI


Katika tukio jingine, Kamanda Kova alisema polisi wamekamata watuhumiwa sita sugu wa ujambazi, silaha mbili na risasi 25 za SMG pamoja na jambazi sugu akiwa na sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment