Serikali ya Rwanda imepuuza madai kuwa maafisa wake wa usalama waliwatesa na kuwadhulumu watu.
Waziri wa sheria, Tharcisse Karugarama,
alifahamisha BBC kuwa madai hayo ambayo yako kwenye ripoti ya shirika la
Amnesty International, yalikuwa ni njama ya kutaka kuipaka tope Rwanda.
Rwanda imetaja madai hayo kama upuzi mtupu.
Lakini alisema kuwa maafisa wa
usalama walikiuka sheria walipochukua hatua wakati wa mashambulizi ya
maguruneti katika mji mkuu Kigali miaka miwili iliyopita.
Aliongeza kuwa, washukiwa walizuiliwa kinyume na
sheria huku akitaja hatua za maafisa hao wa usalama kama ambazo
zilizokuwa na kishindo.
Amnesty International imeitaka Rwanda kuchunguza
madai dhidi ya maafisa wake wa ujasusi kuwa waliwazuilia watu kinyume
na sheria pamoja na kuwatesa.
Kwa mujibu wa shirika hilo kati ya mwezi Machi
mwaka 2010 na mwezi Juni mwaka huu, lilikusanya taarifa za madai ya visa
45 vya kuwazuilia watu kinyume na sheria na vingine kumi na nane vya
mateso na dhulma.
Aidha shirika hilo lilikubali kuwa Rwanda
inapiga hatua katika kukabiliana na mateso na dhulma lakini serikali
imekanusha kuwa ilifanya vitendo kama hivyo.
Washukiwa wengi walikamatwa na kuzuiliwa
kufuatia milipuko kadhaa ya maguruneti, mjini Kigali mwezi Machi mwaka
2010 na pia wakati wa kampeini za uchaguzi mwaka huo.
Waziri wa sheria hata hivyo alikiri kuwa huenda maafisa wa usalama waliwazuilia washukiwa kwa muda mrefu kinyume na sheria.
No comments:
Post a Comment