Sudan kuishtaki Israel kwa UN


Shambulizi dhidi ya kiwanda cha Sudan liliwaua watu wawili

Sudan imesema kuwa inapanga kuishtaki Israel kwa Umoja wa Mataifa kuhusiana na madai ya shambulizi dhidi ya kiwanda chake cha silaha mjini Khartoum.

Balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa Daffa-Alla Elhag Ali Osman, amesema kuwa Israel imevamia kiharamu anga zake mara tatu katika miaka ya hivi karibuni.

Sudan hata hivyo bado haijatoa ushahidi wowote kuunga mkono madai yake na Israel nayo haijatoa tamko lolote kuhusu madai hayo dhidi yake.

Duru nchini Sudan zinasema kuwa kiwanda hicho kilimiaminika kuendeshwa na Iran.

Mwandishi wa BBC w amaswala ya ulinzi anasema inaaminika kuwa kiwanda hicho kilikuwa kinatengeza roketi na zana zengine kwa niaba ya Iran ili kuzipeleka kwa wapiganaji wa Hamas.

Na kwa hivyo Israel iliona umuhimu wa kusitisha shughuli za kiwanda hicho nchini Sudan badala ya kuchukua hatua ambazo zingeudhi Misri.

Ingawa srael bado haijatoa tamko lolote kuhusu madai ya Sudan, afisaa mmoja wa ulinzi aliambia vyombo vya habari kuwa Sudan ni nchi hatari ya kigaidi.

''Serikali ya Sudan inaungwa mkono na Iran na inatumiwa kama kivukio cha silaha kupitia Misri na kuingia Hamas pamoja na kuyaendea makundi mengine ya kigaidi. '' alisema afisaa huyo.

Mwezi Aprili mwaka jana,Khartoum ilidai kuwa Israel ilihusika na shambulizi lengine la angani dhidi yake ambalo liliwaua watu wawili karibu na mji wa Port Sudan.

Israel pia ililaumiwa kwa shambulizi lengine dhidi ya msafara wa magari Kaskazini Mashariki mwa Sudan mwaka 2009.

No comments:

Post a Comment