Sumaye Ateta Na Chadema
Na: Mussa Juma, Arusha na Boniface Meena,MWANANCHI
SIKU
chache baada ya kushindwa katika uchaguzi wa ndani kwenye nafasi ya
Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick
Sumaye amekutana na viongozi wa Chadema ikidaiwa kuwa ni kujadili pamoja
na mengine, uwezekano wa kuhamia huko ili agombee urais katika Uchaguzi
Mkuu ujao 2015.
Sumaye
ambaye anatajwa kuwa alikuwa na mpango wa kuwania urais kupitia CCM,
alishindwa katika uchaguzi wa kuwania ujumbe wa Nec, baada ya kupata
kura 481 dhidi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwezeshaji na
Uwekezaji), Dk Mary Nagu aliyepata kura 648.
Taarifa
zilizothibitishwa na baadhi ya viongozi wa Chadema, zimeeleza kuwa
Sumaye hakuridhishwa na mchakato wa uchaguzi huo wa Nec na kwa matokeo
hayo, alikutana na viongozi wa Chadema kujadili mustakabali wake
kisiasa.
Jana, mjumbe mmoja wa Kamati Kuu ya Chadema, ambaye aliomba jina lake
lisiandikwe gazetini, alithibitisha Sumaye kukutana na viongozi wa
Chadema.
Hata
hivyo alisema hawajafikia mwafaka.
Alisema mawasiliano ya Chadema na Sumaye yalianza mara tu baada ya
matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika Septemba 30, mwaka huu yaliyomwengua
kigogo huyo kwenye kinyang’anyiro hicho.
“Ni
kweli kuna watu wa CCM tumewasiliana nao baada ya uchaguzi ule (wa Nec)
na Sumaye tunawasiliana naye pia lakini siwezi kusema tumefikia wapi,”
alisema mjumbe huyo na kuendelea: “Suala kwamba amekubaliwa kujiunga na
Chadema au la, nadhani huu ni uamuzi wake. Ninachoweza kusema ni kwamba
vikao vilikuwepo na vinaendelea kukaliwa.
Alisema
baada ya matokeo ya Hanang’ na hali ya kisiasa ndani ya CCM, Chadema
kimekuwa kikiwasiliana na Sumaye na kikubwa ambacho kinajionyesha ni
kada huyo wa CCM kutoridhishwa na hali ya mambo ndani ya chama chake.
Mjumbe huyo wa Chadema alisema chama hicho Wilaya ya Hanang’ kinaandaa
mkutano maalumu wa kuwapokea wanachama wapya wa CCM, wengi wao wakiwa
baadhi ya walioanguka kwenye uchaguzi wa Nec wilayani humo.
Habari
zaidi zimeeleza kuwa Chadema kimepanga siku yoyote juma lijalo,
kuwapokea wanachama wapya kutoka CCM, baadhi wakiwa wale walioshindwa
kwenye uchaguzi wa ndani ya chama hicho uliofanyika wilayani Hanang’.
Mmoja wa watu wa karibu na Sumaye alisema anachojua ni kwamba Chadema
wanamtaka Sumaye na siyo Sumaye kukitaka chama hicho cha upinzani.
“Wamekuwa
wakimfuatafuata mara nyingi na mazungumzo ya aina hiyo si mageni baina
ya Sumaye na Chadema. Ila ninachoweza kusema, safari hii chochote
kinaweza kutokea kutokana na hasira alizonazo (Sumaye). Ngoja tusubiri,
atafanya mkutano na waandishi Jumapili.”
Sumaye, Mbowe wazungumza
Alipoulizwa kuhusu madai hayo, Sumaye alisisitiza kuwa atazungumzia
masuala yote yanayohusiana na uchaguzi huo wa Hanang’ atakapokutana na
waandishi wa habari, Dar es Salaam.
“Nitakutana
na waandishi wa habari kuzungumzia kilichotokea naomba tu mwendelee
kunipa muda,” alisema Sumaye na kuongeza kuwa alikuwa akijiandaa kwa
safari ya kwenda Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema
asingependa kuzungumzia suala hilo kwa kuwa yeye si msemaji wa Sumaye...
“Sitaki kumzungumzia Sumaye.
Mimi
si msemaji wake. Tumsubiri yeye azungumze kuhusu hilo.”
Kada wa CCM Hanang’ anena
Katika hatua nyingine, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Hanang’, Goma Gwaltu
amekionya chama hicho kuwa kisipodhibiti vitendo vya rushwa katika
chaguzi zake, kitakufa.
Gwaltu alisema jana kwamba kwa mazingira yaliyopo sasa ndani ya CCM bila
hatua kali kuchukuliwa, kiongozi asiye na fedha hawezi kushika uongozi
na ndiyo sababu anaungana na wana-CCM wengine katika wilaya hiyo, ambao
wanafikiria kukihama chama hicho.
“Kama
wewe una nia ya kuendelea na siasa siyo rahisi kushinda hapa Hanang’
ukiwa hukubaliani na watu fulani, sasa mimi naona ni bora tu kutafuta
chama kingine kwani siyo dhambi,” alisema Gwaltu bila kuwataja ambao
wanataka kuhama CCM.
Hata hivyo, Gwaltu alisema kwa upande wake, hafikirii kuendelea na mambo
ya siasa wala kulalamika makao makuu ya CCM kuhusiana na alichokiita
hujuma alizofanyiwa.
No comments:
Post a Comment