Wapiganaji wa
kigeni wamewasili katika mji wa Gao Kaskazini mwa Mali, kwa mujibu wa
taarifa za meya wa mji huo ambaye yuko uhamishoni.
Taarifa hii inathibitisha ongezeko la wapiganaji wa kiisilamu Kaskazini mwa Mali.
Sadou Diallo amesema kuwa kati ya
wapiganaji 60 na 100 raia wa Algeria na wapiganaji wenye asili ya
Sahrawis waliingia mjini humo siku nne au tano zilizopita.
Mwenyeji mmoja wa Timbuktu aliambia shirika la
habari la AFP kuwa siku ya Jumatatu, wapiganaji wengine kutoka nchini
Sudan waliwasili katika eneo hilo mwishoni mwa wiki.
Mipango inaendelea ya serikali za nchi za Ukanda
wa Afrika Magharibi, ECOWAS kutatua mzozo huo kijeshi baada ya
wapiganaji kutwaa Kaskazini mwa Mali mapema mwaka huu.
Wiki mbili zilizopita, baraza la usalama la
Umoja wa mataifa liliipatia shirika la ECOWAS siku arobani na tano
kuunda mkakati na kutoa maelezo yake kuhusu mpango wa kutuma wanajeshi
3,000 katika eneo hilo.
Wapiganaji wa kiisilamu wa Tuareg walidhibiti eneo hilo baada ya mapinduzi ya kijeshi mwezi Machi.
Wanajeshi wa Mali walipindua serikali ya Mali
baada ya kumtuhumu aliyekuwa Rais kwa kukosa kukabiliana vilivyo na
waasi wa Tuareg ambao walianza harakati zao mwezi Januari.
Lakini waasi walianza kutumia pengo lililoachwa la madaraka na kutwaa eneo zima la Mali ikiwemo mji wa Timbuktu.
Wapiganaji wa kiisilamu ambao sasa
wametofautiana na wenzao wa Tuareg, wameanza kutumia sheria za kiisilamu
katika maeneo wanayodhibiti. Kuna ripoti za watu kuuawa kwa kupigwa kwa
mawe na kukatwa viungo vyao vya mwilini.
No comments:
Post a Comment