Jeshi latuhumiwa na mauaji ya vijana
Raia wameiambia BBC kuwa, vijana
kadhaa wameuawa kwa kupigwa na wanajeshi wa serikali mjini Maiduguri,
Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.
Imamu mmoja ameiambia BBC kuwa vijana 11 kutoka mtaa anaoishi, wameuawa vijana wanne kati yao wakiwa wanawe wa kiume.
Mauaji
hayo yanayodaiwa kufanywa na wanajeshi wa serikali, yametokea ambapo
shirika la kutetea haki za kibinadam la Amnesty International,
limeshutumu maafisa wa ulinzi wa serikali kwa kuwanyanyasa raia wakati
walipowasaka wanamgambo wa Kiislamu.
Lakini msemaji wa jeshi katika eneo hilo la Maiduguri amekanusha madai hayo na kusema hana taarifa kuhusu tukio hilo.
Hata hivyo Luteni Kanali Sagir Musa, ameiambia BBC kuwa uchunguzi utaanzishwa kufuatia madai hayo.
Maiduguri ni ngome ya wapiganaji wa Kiislamu wa
Boko Haram, ambao wanapambana na jeshi la serikali wakitaka sheria za
Kiislamu maarufu kama sharia kutumika nchini humo.
Mamia ya watu wameuawa katika maeneo ya
Kaskazini na Kusini mwa Nigeria, katika mashambulio yanayosadikika
kutekelezwa na kundi hilo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Ripoti ya shirika la Amnesty International
iliyochapishwa hiyo jana, imesema kuwa wanajeshi hao wa serikali
walihusika na visa vingi vya ukiukwaji wa haki za kibinadam, wakati wa
operesheni zao za kuthibiti wapiganaji hao wa Boko Haram.
Malam Aji Mustapha, ambaye ni Imamu katika
msikiti mmoja mjini Maiduguri, amesema, baada ya maombi ya Alhamisi
asubuhi, wanajeshi walimkamata na kumpeleka pamoja na watoto wake hadi
uwanja mmoja ambako watu wengine wanaendelea kuzuiliwa.
Amesema walipofika kwenye uwanja huo waliamriwa kulala chini huku maafisa hao, wakiwafanyia uchunguzi mmoja baada ya mwingine.
No comments:
Post a Comment