Serikali, mwekezaji kujenga nyumba za askari

Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kushirikiana na mwekezaji inatarajia kujenga nyumba za askari na majengo ya biashara katika eneo la Oysterbay Polisi, Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, ili kukabiliana tatizo la uduni wa makazi ya watumishi hao wa umma.


Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Msemaji wa Wizara hiyo, Issac Nantanga, alipozungumza na waandishi wa habari na kuongeza kuwa mradi huo unatarajia kuanza muda wowote baada ya upembuzi yakinifu kukamilika.

Alisema mradi huo, ambao utagharimu Sh. bilioni 426.6, utahusisha ujenzi wa hospitali ya kisasa, ukumbi wa mikutano, hoteli, ofisi za kukodisha na nyumba za kupangisha.

Nantanga alisema nyumba 350 za askari zitajengwa kupitia mradi huo katika eneo la Mikocheni na Kunduchi na kwamba, zitakapomalizika zitasaidia kupunguza tatizo la makazi kwa watumishi hao.

Alisema mkataba huo unasema kwamba, majengo yote yatakayojengwa yatakuwa mali ya serikali na itayakodisha kwa mwekezaji kwa Sh. bilioni 4.36 kwa mwaka.

No comments:

Post a Comment