Sheikh Ponda kusomewa maelezo ya awali leo


Katibu wa Taasisi za Jumuiya za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda

Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, jijini Dar es Salaam, leo inaanza kusikiliza maelezo ya awali dhidi ya kesi inayomkabili Katibu wa Taasisi za Jumuiya za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda (54) na wenzake 49.

Sheikh Ponda na wenzake, wanakabiliwa na mashitaka matano yakiwamo ya kula njama, kuingia, kujimilikisha ardhi kwa jinai, wizi wa mali ya Sh. milioni 59.6.

Aidha, Sheikh Ponda pia anakabiliwa na shitaka la kufanya uchochezi wa kutenda makosa hayo.

Uamuzi wa kuanza kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao umefikiwa baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka, kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Maelezo hayo ya awali dhidi ya Sheikh Ponda na wenzake, yatasomwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Victoria Nongwa.

Oktoba 18, mwaka huu, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na kusomewa mashitaka, lakini Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) aliwasilisha hati ya kiapo cha kupinga dhamana ya Sheikh Ponda kwa maelezo kuwa ni kwa ajili ya usalama wake na maslahi ya Taifa.

Mbali na Sheikh Ponda, washtakiwa wengine ni Kuluthumu Mohamed, Zaldah Yusuph, Juma Mpanga, Farida Lukoko, Adamu Makilika, Athuman Salim, Seleman Wajumbe, Salum Juma, Salum Mkwasu na Ramha Hamza.

Wengine ni Halima Abas, Maua Mdumila, Fatihiya Habibu, Hussein Ally, Shabani Ramadhani, Hamis Mohamed, Rashid Ramadhani, Yusuph Penza, Alawi Alawi, Ramadhani Mlali, Omary Ismail, Salma Abdulatif, Khalid Abdallah, Said Rashid, Feswali Bakari, Issa Wahabu, Ally Mohamed, Mohamed Ramadhani, Abdallah Senza, Juma Hassan na Mwanaomary Makuka.

Washtakiwa wengine ni Omary Bakari, Rashid Ndimbu, Hamza Ramadhani, Ayoub Juma, Maulid Namdeka, Farahan Jamal, Smalehes Mdulidi, Jumanne Mussa, Salum Mohamed, Hamis Khalid, Dite Bilal, Amiri Said, Juma Yassin, Athuman Rashid, Rukia Yusuph, Abubakari Juma na Ally Salehe.

Upande wa mashitaka ulidai kuwa katika shitaka la kwanza, Oktoba 12, mwaka huu eneo la Temeke jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote 50 walikula njama ya kutenda makosa.

Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa siku ya tukio la kwanza katika eneo la Chang’ombe Markas, wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote 50, kwa jinai walivamia kwa nia ya kutaka kujimilikisha kiwanja ambacho ni mali ya Agritanza Ltd.

Ilidaiwa kuwa katika shitaka la tatu kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka huu eneo la Chang’ombe Markas, pasipo uhalali na uvunjifu wa amani, washtakiwa wote kwa pamoja walijimilikisha ardhi ambayo ni mali ya Agritanza Ltd.

Katika shitaka la nne, ilidaiwa kuwa kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka huu eneo la Chang’ombe Markas, washtakiwa wote kwa pamoja waliiba vifaa mbalimbali vya ujenzi yakiwamo matofali 1,500, tani 36 za kokoto na nondo vyote vikiwa na thamani ya Sh. 59,650,000, mali ya Agritanza Ltd.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa katika shitaka la tano linalomkabili Sheikh Ponda peke yake, kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka huu eneo la Chang’ombe Markas, mshtakiwa akiwa Katibu wa Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, aliwashawishi wafuasi wake kutenda makosa ya jinai.

Washtakiwa wote walikana mashitaka yao kwa nyakati tofauti.

 

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment