Waasi wa DRC wakataa kuondoka Goma


Maelfu ya watu wamelazimika kutoroka mapigano

Waasi wa M23 wamekataa pendekezo la viongozi wa mataifa ya eneo la Maziwa Makuu la kuwataka wakomeshe mapigano na kuondoka mjini Goma.

Waasi hao wanaipinga serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kupigana nalo katika eneo la mashariki mwa taifa hilo.

Hatua ya waasi hao kuuteka mji wa Goma yapata wiki moja iliyopita imezua wasiwasi kwamba huenda yakatokea mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Awali, serikali ilisema haiwezi kufanya mazungumzo na waasi hao hadi pale watakapoondoka mjini Goma.

Kupitia taarifa, marais wa Rwanda, Kenya, Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo waliiambia M23 "ikomeshe mapigano mara moja na iondoke Goma", na hali kadhalika "ikome kusema kwamba inakusudia kuipindua serikali."

Marais hao pia walipendekeza kwamba:-

  • Serikali hiyo iangalie upya "matakwa halali ya M23"
  • M23 iondoke katika maeneo iliyoteka na kusogea takriban umbali wa kilomita 20 kutoka Goma katika kipindi cha siku mbili
  • Kuundwa kwa kikosi cha pamoja cha wanajeshi kutoka nchi za kikanda, serikali, na waasi watakaokuwa katika uwanja wa ndege wa Goma
  • Polisi wa Goma warudishiwe silaha na kurudi kazini
  • Walinda amani wa Monusco wawekwe katika eneo huru, kati ya Goma na ngome ya waasi hao.

No comments:

Post a Comment