Mwenyekiti wa tume ya mabadiliko ya katiba Jaji warioba
MIKUTANO ya kukusanya maoni ya upatikanaji
wa Katiba Mpya Visiwani Zanzibar, imeingia dosari baada kuzuka ghasia na
baadhi ya watu kujeruhiwa kwa kuchomwa visu.
Vurugu hizo ambazo chanzo chake ni siasa,
zilitokana na wafuasi wa baadhi ya vyama vya siasa, kuvamia mikutano
iliyokuwa ikifanyika Unguja na kusababisha hofu za kiusalama.
Baadhi ya maeneo ambayo wanasiasa hao
walivamia mikutano ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kusababisha
ivunjike ni Shehia za Magomeni na Mpendae Mkoa wa Mjini Magharibi.Hii ni
mara ya kwanza ghasia kuzuka katika mikutano ya kukusanya maoni ya
Katiba Mpya visiwani humo.
Tukio la kuchomana visu, lilitokea katika
Shehia ya Mpendae baada ya vurugu zilizosababishwa na vijana kuvamia
mkutano uliokuwa ufanyike jana mchana.
Vijana hao walianzisha ghasia
hizo baada ya kutaka kuvunja utaratibu uliokuwa umewekwa. Walitaka wakae
mbele ya wengine waliokuwa wametangulia katika mkutano huo.
Hatua hiyo ilipingwa na kuibua ghasia ziliozababisha watu kadhaa kujeruhiwa kwa visu.
Tukio jingine lililovuruga mkutano huo ni lile
lililotokea katika Shehia ya Magomeni, Jumatatu wiki hii baada ya
kuibuka kwa mvutano baina ya makundi mawili yenye misimamo tofauti juu
ya mfumo wa Muungano; kuna wanaopinga na wanaoukubali.
Misimamo hiyo imeelezwa kujikita katika misingi na sera za vyama vyao vya kisiasa.
Katika misimamo hiyo, CUF kinaamini katika
Serikali ya Zanzibar na Tanganyika kila moja kuwa na mamlaka kamili na
Muungano uwe wa mkataba wakati, CCM kinasimamia kwenye Serikali mbili;
Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Shehia ya Magomeni
Saa mbili kabla mkutano
kuanza, watu wengi walifika Uwanja wa Mzalendo ambako mkutano ulitakiwa
kufanyika. Walijipanga kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na Tume ambao
ni aliyewahi kufika ndiye anayetangulia kutoa maoni.
Hali hiyo ilisababisha wakazi wa Shehia hiyo
waliokuwa wenyeji wa mkutano, kukosa nafasi ambayo ingewawezesha kutoa
maoni kwa mazungumzo ya ana kwa ana.
Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni,
Salmin Awadh Salmin, alisema hawakuwa tayari kuwa wenyeji wa mkutano
ambao hawatashiriki akisema waliokuwa wamejipanga wote walifikishwa
kituoni hapo kwa magari kwa lengo maalumu la kuwakosesha wenyeji kutoa
maoni yao, kwa kuwa inafahamika kuwa wengi wao ni wana CCM.
Hoja hizo alizitoa kwa wajumbe wa Tume ambao
pia hawakuridhishwa na hali ya usalama katika eneo hilo kutokana na
vurugu zilizokuwa zikifanywa na wafuasi wa CCM na CUF.
“Kwa hali ilivyo, hatuwezi kupata utulivu
utakaowezesha tufanye kazi kwa ufanisi na kumaliza mkutano kwa amani
bila fujo. Natangaza rasmi kuwa leo hakuna mkutano,” Mwenyekiti wa Timu
ya Tume hiyo inayokusanya maoni visiwani hapa, Profesa Mwesiga Baregu.
Akizungumza baada ya kuvunjika kwa mkutano
huo, Salmin alisema waliokuwa wamefika kutoa maoni walikuwa wakitaka
kunadi misimamo ya vyama vyao akisema hiyo ni hali ya kihistoria
inayowakabili wakazi visiwani humo.
“Hata katika kupata huduma za kijamii, siasa inapewa kupaumbele
na hili ndilo chimbuko la matatizo yote haya, ndiyo maana hata maoni
yanayotolewa ni ya aina mbili, Muungano udumu au uwe wa mkataba na
serikali mbili.
Dalili za vurugu
Dalili za kuwapo kwa
vurugu zilianzia kwenye mkutano uliofanyika Jumatatu asubuhi kwenye
Viwanja vya Kibanda Maiti katika Shehiya ya Kwa-Alamsha, ambako watu
waliotaka Muungano ubaki, walizomewa huku waliotaka Serikali ya Zanzibar
na Tanganyika kila moja ikiwa na mamlaka kamili, muungano uwe wa
mkataba walishangiliwa.
Hali hiyo ilitawala mkutano huo bila kujali
jitihada za Profesa Baregu kukemea mara kwa mara hali hiyo. Pamoja na
kwamba maoni yatafanyiwa mchujo, Wananchi hao wanaamini kuwa upande
utakaotoa maoni kwa wingi ndiyo utakaoshinda kwa matakwa yao kuingizwa
kwenye Katiba Mpya.
Mbunge amshambulia Mratibu
Katika mkutano
uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Wandarasi, Shehia ya Meya, Mbunge wa
Viti Maalumu (CCM), Faharia Shomari alimshambulia Mratibu wa shughuli za
Tume visiwani humo, Ahmed Haji Saadat kwa maneno akiwambia:
“Mimi ni Mjumbe wa Tume ya Bunge ya Sheria
na Katiba. Nilihusika kutunga sheria inayowaongoza kufanya kazi hii,
inatakiwa wakazi wa shehia mnayofanyia mkutano watoe maoni kwa
kuzungumza, wengine wapewe fomu; tatizo wewe unajidai mkubwa kuliko hata
tume yenyewe. Mikutano yote umeivuruga wewe, tangu mwanzo nilikwambia,
kiko wapi sasa,” alisema mbunge kwa hasira.
baada ya mashambulizi hayo, Saadat naye
alijibu: “Mheshimiwa, ninakuheshimu sana, ikiwa tatizo unaliona ndani ya
sheria na unakiri ulihusika kutunga sheria hiyo bila kueleza uzoefu
ulionao kwa mazingira ya Zanzibar, wewe ni sehemu ya tatizo. Tangu
nilipokuwa Mji Mkongwe umekuwa ukinifuata kwa maneno, tatizo lako hasa
nini?”
Zogo hilo lilikuwa kubwa na kusababisha askari kumwondoa
mbunge huyo kumpeleka pembeni. Lakini baada ya muda, mbunge huyo
alijivuta mpaka alikokuwa Saadat na kuanza tena kumwandama kwa maneno
akisema: “Kiko wapi? Jana hamkufanya mkutano kwa kujidai kwako, leo pia
zogo hilo, huenda msiufanye kwa kujidai mkubwa lol, unajidai una nguvu
kuliko hata wajumbe wa tume? Kiko wapi sasa?”
Maneno hayo yalimkera Mratibu huyo ambaye alimtaka athibitishe anayomtuhumu kwa maandishi.
Iliwalazimu askari polisi kuingilia kati tena kati na kumshauri Saadati kumfungulia mashtaka mbunge huyo.
Mbunge huyo alitoa maoni yake kwenye Jimbo la
Mji Mkongwe, Vuga na kuhudhuria mkutano wa maoni uliyofanyika siku hiyo
hiyo kwenye Hoteli ya Bwawani ambako inadaiwa kuwa ndiko alikoanza
kuzozana na Saadat; akimtuhumu kupendelea wanaotaka muungano uwe wa
mkataba na Serikali ya Zanzibar yenye mamlaka yake kamili.
Tuhuma hizo zilitokana na Saadat kukataa
kuruhusu kundi la wanawake ambao Shomari alitaka wakatoe maoni tofauti
na utaratibu uliowekwa ambao unampa nafasi aliyewahi kufika na kujipanga
kwenye foleni kutoa maoni kwanza.
“Nimeishakuona unapendelea watu wa mkataba,
subiri nitakuripoti kwa (mmoja wa wajumbe ambaye pia ni kada wa CCM),”
Shomari alisikika akimweleza Saadat ambaye alimjibu kuwa kinachoangaliwa
si nani wala itikadi gani, bali utaratibu uliowekwa tu.
No comments:
Post a Comment