Zombe kizimbani tena

Aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam (RCO), Abdallah Zombe

Mahakama  ya Rufani leo inatarajia kusikiliza rufaa ya Jamhuri dhidi ya kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva taksi mmoja, iliyokuwa inamkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam (RCO), Abdallah Zombe na wenzake wanane.

Rufaa hiyo itasikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti Jaji William Mandia, Wengine ni Nathalia Kimaro na Catherine Oriyo.


Kwa mujibu wa ratiba ya orodha ya kesi zilizopangwa kusikilizwa mwezi huu na mahakama hiyo, kesi ya Zombe na wenzake itasikilizwa leo saa 3:00 asubuhi.


Oktoba 6, mwaka 2009, Mkurugenzi wa Mashtaka  (DPP), alikata rufaa hiyo iliyosajiliwa kwa namba  254/2009, akipinga hukumu iliyotolewa Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam na Jaji Salum Massati (kwa sasa jaji wa mahakama ya rufani) iliyowaona Zombe na wenzake hawana hatia na kuwaachia huru.


“Katika kesi hii upande wa mashitaka licha ya kuleta mashahidi 37 na vielelezo 23, umeshindwa kuithibitishia mahakama kuwa ni kweli washitakiwa wote ndiyo waliowaua marehemu na kwa sababu hiyo nawaachia huru washitakiwa wote.


“Na kwa kuwa mahakama hii imewaona washitakiwa si wauaji, hivyo kuanzia sasa naliagiza Jeshi la Polisi liende kuwasaka wauaji wa marehemu wale, na Zombe na wenzake waachiliwe huru,” alisema Jaji Massati na kuuacha umati wa watu ukiwa umeshangaa.


Jaji Massati, alisema kamwe mahakama haiwezi kumhukumu mshitakiwa kwa ushahidi dhaifu na wa kusikia kama uliowasilishwa mahakamani hapo, kwani kwa kufanya hivyo ni kukiuka sheria.


“Mahakama haipo kwa ajili ya kuonea mtu kwa kumhukumu kwa ushahidi wa kusikia, ambao haukubaliki kisheria,” alisema Jaji Massati.


Jaji Massati aliagiza upande wa Jamhuri kuwasaka na kuwafikisha mahakamani waliohusika na mauaji ya wafanyabiashara hao wa madini kutoka Mahenge mkoani Morogoro, Sabinus Chigumbi maarufu kama Jongo na ndugu yake Ephrahim Chigumbi, Mathias Lunkombe pamoja na Juma Ndugu, dereva teksi.


Zombe na wenzake walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya kukusudia ya wafanyabiashara watatu wa madini wa Mahenge Morogoro na dereva wa teksi wa Manzese  Dar es Salaam.


Walishtakiwa kuufanya mauaji hayo Januari 14, mwaka 2006 katika msitu wa Pande uliopo Mbezi Luis, Jijini Dar es Salaam.


Mbali na Zombe, washtakiwa wengine walikuwa ni ASP Christopher Bageni, ASP Ahmed Makelle, Konstebo Noel Leonard, Konstebo Jane Andrew, Koplo Nyangerela Moris, Konstebo Emanuel Mabula na Koplo Felix Sedrick,


Wengine walikuwa ni Konstebo Michael Shonza, Koplo Abeneth Salo, Koplo Rashid Lema (aliyefariki kabla ya kujitetea), Koplo Rajabu Bakari na Koplo Festus Gwabisabi.


Kabla ya Zombe na wenzake kuonekana wana kesi ya kujibu, Mahakama Kuu iliwaachia huru Konstebo Noel, Koplo Nyangerera, Konstebo Shonza  baada ya mahakama kuwaona kuwa hawakuwa na kesi ya kujibu.


Agosti 17, mwaka 2009, Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam liwaachia huru washtakiwa wote, ikisema kuwa baada ya kusikiliza ushahidi na hoja za mawakili wa pande zote, imeridhika kuwa washtakiwa hawakuwa na hatia ya mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili.


Jaji Massati aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo alisema kuwa alibaini kuwa walioshtakiwa siyo walioua, bali wauaji hawakuwapo mahakamani. Hivyo aliiagiza Jamhuri kuwasaka na kuwafikisha mahakamani wauaji wa wafanyabiashara hao.


Hata hivyo, hadi leo Jeshi la Polisi halijawakamata wauaji hao na kuwafikisha mahakamani.


Baada ya hukumu ya Jaji Massati, ambayo iliacha mjadala miongoni mwa jamii, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) alikata rufaa katika Mahakama ya Rufani, akipinga hukumu hiyo, akidai kuwa Jaji Massati alikosea kuwaachia huru washtakiwa hao kwa kuwa ushahidi wa mazingira ulionyesha kuwa Zombe na wenzake walihusika na mauaji hayo.


Pia, DPP alibainisha kwamba hukumu hiyo haikuwa ya haki kwa Jamhuri akidai kwamba kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, washtakiwa wote walikuwa na hatia.


Baadhi ya wananchi, ndugu na jamaa wa marehemu hawakuridhishwa na hukumu hiyo na waliishia kusema kuwa wanamuachia Mungu.


“Wazee wa baraza walishasema kuwa anayo hatia, leo mahakama inasema hawajaua, sisi raia tunajiuliza haki ipo wapi? Tunaiomba serikali kukata rufaa la sivyo serikali imeshindwa kazi, na hatuitaki tena,” alisema Ramadhan Abdallah, huku akishangiliwa na mamia ya wananchi wenzake.


Kabla ya Zombe na wenzake kukamatwa na kufunguliwa mashtaka, Januari 23, 2006, Rais Jakaya Kikwete aliunda tume iliyoongozwa na Jaji Mussa Kipenka kuchunguza mauaji ya wafanyabiashara hao.


Kuundwa kwa tume hiyo kulitokana na malalamiko kutoka kwa watu mbalimbali na vyombo vya habari juu ya utata wa vifo hivyo.


Baada ya mauaji hayo, Zombe, aliitisha mkutano wa waandishi wa habari na kusema kuwa polisi waliwakamata watu hao katika eneo la Sinza Palestina na kwamba baadaye walianza kuwarushia risasi polisi na polisi kufanikiwa kuwaua katika eneo la barabara ya Sam Nujoma.


Zombe alidai kuwa siku hiyo asubuhi watu hao walipora fedha katika duka la vito eneo la Kariakoo na baadaye jioni kupora fedha nyingine katika Kampuni ya Bidco iliyoko Mwenge huku akionyesha fedha taslimu Sh. milioni tano ambazo alidai kuwa polisi waliziokoa kutoka kwa watu hao.

 

No comments:

Post a Comment