Walimu watatu shule moja wafa ajalini
Walimu
watatu na walezi wawili wa wanafunzi katika shule ya Scolastica iliyopo
eneo la mji mdogo wa Himo, wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro,
wamefariki katika ajali mbaya ya gari mjini humo.
Katika ajali hiyo iliyotokea, pia walimu wanane wamejeruhiwa, baadhi
vibaya na wengine kupata majeraha madogo madogo na kutibiwa katika
Hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi na
kuruhusiwa.
Ajali hiyo ilitokea Disemba 10, mwaka huu, majira ya saa 2:30 usiku,
wakati walimu na walezi hao wakitoka kwenye mazishi ya mwanafunzi wa
kidato cha tatu wa shule hiyo, Jackson Kisiri, aliyefariki kwa kugongwa
na pikipiki eneo la Kwa Mrefu wilayani Arumeru, mkoani Arusha.
Akizungumza mara baada ya kupatiwa matibabu na kuruhusiwa
katika hospitali ya KCMC, Mkuu wa shule hiyo, Marko Shiloli, alisema
kwenye gari hilo kulikuwa na walimu kumi, walezi wawili na dereva na
kwamba walimu watatu walifariki katika eneo la tukio na walezi hao
walikutwa na mauti wakiwa KCMC.
Alisema mwanafunzi huyo alifariki wakati akiwa likizo nyumbani kwao na
kwamba walimu na walezi hao walikwenda kwenye mazishi yaliyofanyika
Disemba 10, mwaka huu nyumbani kwao.
Kamanda wa Polisi Mkoani Kilimanjaro, Robert Boaz, amethibitisha kutokea
kwa ajali hiyo, hata hivyo alisema chanzo halisi hakijafahamika.
Alisema gari lililokuwa na walimu hao lilikuwa likitokea mkoani Arusha kwenda Himo.
Kamanda Boaz alisema ajali hiyo ilihusisha gari lenye namba za usajili T
771 AQD mali ya shule hiyo lililokuwa linaendeshwa na Alexanda Mosha
(54), ambalo liligongana ubavu wa kulia na lori aina ya Fuso lenye namba
za usajili T 212 AHH likiwa na tela lenye namba za usajili T 653 AAJ
likiendeshwa na Omar Abdalah (37).
Alisema ajali hiyo ilitokea karibu na mto Kikavu Chini mahali yalipo
makaburi ya raia wa Japan wilayani Hai na kwamba dereva wa gari la shule
ya Scolastica anaendelea na matibabu hospitalini.
Mkuu wa shule hiyo aliwataja walimu waliofariki kuwa ni, Julius Kimario
(28) wa masomo ya Kiingereza na general study, Joseph Leon Okolot raia
wa Kenya wa somo la Historia aliyefariki wakati akifanyiwa upasuaji
kutokana na kuvuja damu nyingi na Bernard Amukunyo (30) wa masomo ya
Jiografia na Historia raia wa Kenya.
Wengine waliofariki ni Ernest Ambani (48) mlezi wa wanafunzi wa kiume na
Nelly Sasaka Deruya raia wa Kenya ambaye alikuwa mlezi wa wanafunzi wa
kike shuleni hapo.
Shiloli alisema kwa mujibu wa watu walioshuhudia ajali hiyo, chanzo cha
ajali kinaelezwa ni dereva wa gari lao kutaka kulipita gari lililokuwa
mbele yake ambalo lilikuwa halionyeshi mwelekeo sahihi kwani mara kwa
mara dereva alionyesha ishara ya kusimama na kumruhusu dereva kupita.
“Nilikuwa nimekaa mbele, wakati ajali inatokea nilikuwa nimelala
nakumbuka tulikuwa tumeongozana na lori ambalo lilikuwa halieleweki kama
linakwenda au la na ndipo dereva akaamua kulipita na wakati akijitahidi
kurudi sehemu yake akakutana na lori na kukwaruza gari pembeni ...
nilishtuka watu wakilia na wengine wakiwa nje na kuona waliokufa pale
pale watatu … nimeumia kidogo,” alisema.
Mwalimu huyo mkuu alisema ni pigo kubwa kwa shule hiyo kupoteza walimu
na walezi hao na kwamba miili yao imeharibika vibaya na inatakiwa
kuzikwa mapema kwamba kwa sasa
wanawasiliana na ndugu wa marehemu na kama taratibu zikikamilika watazikwa leo.
Ofisa Habari wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Gabriel Chisseo, alisema kati ya majeruhi waliofikishwa hospitalini hapo,
wawili walifariki wakati wakipata matibabu ambao ni Nelly na Joseph.
Alisema pia walipokea miili ya watu watatu waliokutwa na mauti eneo la
tukio na kwamba kati ya majeruhi wanane, watano akiwamo aliyetambulika
kwa jina la Peter Mlay wameruhusiwa kati ya juzi na jana baada ya
kupata matibabu na watatu wapo wodi za wagonjwa wa kawaida wakiendelea
na matibabu.
Kamanda Boaz aliwataka madereva kufuata sheria za barabarani na abiria
kuwa wa kwanza kutoa taarifa juu ya madereva wanaokiuka sheria za
usalama barabarani na si kuwa wachochezi wa madereva kuongeza mwendo
hasa katika msimu huu wa sikukuu za krismasi na mwaka mpya ambao watu
wengi huelekea makwao kwa ajili ya sikukuu hizo.
No comments:
Post a Comment