Polisi Dar bado wawasaka walioua, kupora milioni 150/-


Jeshi  la polisi nchini limesema linaendelea na uchunguzi wa kuwabaini waliohusika na tukio la uporaji wa Sh. milioni 150 eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na NIPASHE, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Marietha Minangi, alisema jeshi la polisi bado linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na hakuna mtuhumiwa mwingine aliyekamatwa.

Alisema polisi wanaendelea kuwahoji vijana wawili wasukuma mikokoteni wanaotuhumiwa kuhusika na tukio hilo na kama watabaini kuwa hawakuhusika, watachiwa.

Kamanda Minangi alisema mpaka sasa fedha hizo zilizoibiwa hazijapatikana.

Hata hivyo, alisema polisi wanahisi majambazi wawili waliofanikiwa  kukimbia, walitoroka na kiasi hicho cha fedha.

Alisema majeruhi wa tukio hilo wanaendelea vizuri katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Tukio hilo la ujambazi lilitokea juzi katika mtaa wa Livingstone na  Mahiwa eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Mbali na kuchukua kiasi hicho cha fedha, majambazi hao waliwaua watu wawili na kuwajeruhi wengine watatu.


No comments:

Post a Comment