Mbivu, mbichi darasa saba wakati wowote

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Phillip Mulugo

Wizara  ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, inatarajia kutangaza matokeo ya Mtihani wa Taifa wa darasa la saba uliofanyika Septemba, mwaka huu wiki hii au mwanzoni mwa wiki ijayo.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Phillip Mulugo, aliliambia NIPASHE kutoka Mbeya kuwa wamepanga matokeo ya darasa la saba yatolewe wiki hii na kama itashindikana, basi mwanzoni mwa wiki ijayo.

Tangu wiki iliyopita, wananchi wamekuwa wakiuliza matokeo ya darasa saba ili kama watoto wao watamechaguliwa kuendelea kidato cha kwanza, wafanye maandalizi.

Imekuwa kama mazoea miaka ya nyuma matokeo ya mitihani darasa la saba kutolewa kabla ya  Krismas.

Hata hivyo, mwaka huu wananchi wameingiwa na wasiwasi kutokana na kusalia siku chache kufikia Krismasi.

Katibu wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Dk. Joyce Ndalichako, alisema watahiniwa 894,881 walifanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka huu.

Alisema kati ya watahiniwa hao waliosajiliwa, wavulana ni 426,285 sawa na asilimia 47.64 na wasichana 468,596 sawa na asilimia 52.36.

Mitihani hiyo ya mwaka huu ilifanyika  kwa mfumo mpya wa usahihishaji unajulikana kama ‘Optical Mark Reader’ (OMR).

Watahiniwa walitumia fomu maalum za teknolojia kujibia maswali zitakazosahihishwa kwa mashine maalum.

Mfumo huo una lengo la kupunguza ubabaishaji wa matokeo kwa ujumla kwa watahiniwa hao.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment