Hukumu rufaa ya Lema yaiva
Habari zilizopatikana jana kutoka mahakamani hapo
zilisema kuwa jopo la majaji watatu waliosikiliza rufaa hiyo
limeshakamilisha kuandika hukumu yake na kwamba itasomwa kesho kuanzia
saa 3:00 asubuhi.
Lema ambaye ni kada wa Chadema, alivuliwa ubunge
Aprili 5, mwaka huu katika hukumu iliyotolewa na Jaji Gabriel Rwakibalia
kutokana na kesi iliyofunguliwa na makada watatu wa CCM; Mussa Mkanga,
Happy Kivuyo na Agnes Mollel, wakipinga ushindi wake katika uchaguzi
mkuu wa 2010.
Pamoja na kumvua ubunge, Jaji huyo pia alimwagiza
Msajili wa Wilaya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kuiarifu Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (Nec), kuhusu Lema kutiwa hatiani na kuhukumiwa kwa Kifungu
cha 114 cha sheria ya uchaguzi ambacho kinamnyima kupiga au kupigiwa
kura kwa kipindi cha miaka mitano.
Matumizi ya kifungu hicho ni miongoni mwa hoja
zilizowasilishwa na Lema kupitia kwa mawakili wake akidai Jaji alikosea
kwa sababu makosa yaliyomvua ubunge hayaangukii kwenye vitendo vya
rushwa, kuzuia watu kupiga kura.
Jaji Rwakibarila alimvua Lema ubunge baada ya
kuridhika kuwa alitumia lugha na kauli za udhalilishaji dhidi ya
aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk Batilda Burian), inayoangukia kwenye
Kifungu cha 113.
Kutokana na hukumu hiyo, Lema, kupitia kwa
mawakili wake Method Kimomogoro na Tundu Lissu alikata rufaa Mahakama ya
Rufani, akiwasilisha hoja 18 za kuipinga.
Hukumu ya Jaji Rwakibarila pia ilipingwa na
mawakili wa Serikali waliokuwa wakimwakilisha Mwanasheria Mkuu katika
shauri hilo, Timon Vitalis na Juma Masanja ambao wanadai haina hadhi ya
kuitwa hukumu kutokana na kujaa dosari za kisheria.
Hata hivyo, wakati Lema akikata rufaa, warufaniwa;
Mkanga, Mollel na Kivuyo nao waliwasilisha rufaa kupitia kwa Mawakili
wao, Alute Mughwai na Modest Akida kupinga uamuzi wa Jaji Rwakibarila
kutupilia mbali baadhi ya madai yao.
Lema na mmoja wa wakili wake, Kimomogoro jana
walithibitisha kwa nyakati tofauti kupokea hati za kuitwa mahakamani
kusikiliza hukumu hiyo.
Taarifa kwamba hukumu itasomwa kesho zilitawala
Jiji la Arusha jana na viongozi wa Chadema wakiongozwa na Katibu wa
Mkoa, Amani Golugwa walionekana wakijiandaa kuelekea Dar es Salaam
kusikiliza uamuzi huo.
Akizungumza kwa simu jana alasiri, Golugwa
alisema ataongoza kundi la wanachama na viongozi zaidi ya 40 kutoka
Arusha kwenda Dar es Salaam leo.
Rufaa
Rufaa hiyo ilisikilizwa na jopo la Majaji, Salum Massati, Bernard Luanda wakiongozwa na Jaji Nathalia Kimaro.
Siku ya usikilizwaji upande wa wajibu rufaa waliweka pingamizi
dhidi ya rufaa ya Lema, wakidai kuwa ilikuwa na dosari za kisheria, huku
wakiomba Mahakama hiyo itupilie mbali bila kutoa nafasi yoyote ya
kukatwa upya.
Katika uamuzi wake dhidi ya pingamizi hilo,
Novemba 8, 2012 Mahakama ya Rufani ilitupilia mbali rufaa hiyo ya Lema
baada ya kukubaliana na hoja za pingamizi lakini ikatoa fursa ya kukatwa
upya katika muda wa siku 14 kwa mujibu wa Kifungu cha 111 cha Kanuni za
Mahakama ya Rufani.
Baada ya kufanya marekebisho hayo ndani ya muda huo kama alivyoamuriwa na Mahakama, ilisikilizwa Desemba 4, 2012.
Hoja za warufani
Lema
aliyeibuka na ushindi wa zaidi ya kura 19,000 dhidi ya Dk Burian, anadai
Jaji Rwakibarila alimvua ubunge kwa kuzingatia ushahidi wa mdomo usio
na nyaraka za kuuthibitisha kinyume cha sheria.
Alitoa hoja 18 kupinga hukumu hiyo na pia
alimtuhumu Jaji Rwakibarila kutozingatia ushahidi wake na mashahidi wake
watatu kwa madai kuwa walikuwa wanachama na viongozi wa Chadema, hivyo
walikuwa na masilahi, lakini papohapo akakubali na kutumia ushahidi wa
wanachama na viongozi wa CCM.
Kwa upande wake, Wakili Vitalis alidai kuwa
Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilikosea kutengua ubunge wa Lema, kwa madai
ya kutumia lugha za matusi, akidai kuwa Bunge limeruhusu wanasiasa
kutukanana kwenye kampeni.
Alisema kwa mujibu wa Kifungu cha 108 cha Sheria
ya Uchaguzi , Sura ya 313 ya 2010, matusi si miongoni mwa mambo ambayo
yanaweza kutengua matokeo ya uchaguzi na kwamba Bunge liliruhusu
kutukana kutoka na kufanya marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi ya 1995
baada ya hukumu ya kesi kati ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na
Aman Walid Kabouru.
Vitalis alidai kuwa sheria ilikuwa ikiruhusu
matokeo ya uchaguzi kutenguliwa kutokana na lugha za matusi, lakini
baada ya hukumu ya kesi ya Kabouru Januari 1995, Julai mwaka huo Bunge
lilifanya marekebisho na kuondoa suala la matusi katika mambo yanayoweza
kutengua uchaguzi.
Pia alidai kuwa kifungu cha 108 (2) cha Sheria ya
Uchaguzi kinaeleza aina za ubaguzi zinazokatazwa ni pamoja na wa kidini
na kikabila na kwamba aina nyingine kama makazi (Uzanzibar, Ubara)
hazijatajwa.
Wakili Vitalis alidai kuwa wajibu rufaa hawakuwa
na haki ya kufungua kesi kupinga ushindi wa mrufani (Lema), kwa kasoro
zilizotokea wakati wa kampeni kwa sababu hawakuwa wahusika katika
mchakato wa kampeni za uchaguzi huo.
Vitalis alidai kuwa anayepaswa kufungua kesi
mahakamani kwa madai ya lugha ya matusi ni yule aliyetukanwa kwa kuwa
hayo ni maumivu ya mtu binafsi na kwamba hata anapokufa, madai yake nayo
hufa wala hayawezi kuendelezwa na mtu mwingine.
“Sasa iweje kwa mtu ambaye yuko hai lakini watu wengine ndiyo waje mahakamani kufungua kesi?” alihoji wakili huyo.
Warufaniwa
Hata hivyo, hoja hizo zilipingwa na Wakili Mughway akidai kuwa si kweli kwamba Bunge limeruhusu kauli za matusi kwenye kampeni.
“Sikubaliani na maneno ya AG (kupitia Wakili
Vitalis) kuwa ni ruksa wanasiasa kutukanana,” alisema na kusisitiza kuwa
madhumuni ya kukataza vitendo hivyo ni kudumisha siasa safi na
kuhakikisha nchi inatawaliwa na siasa safi.
Alisema kwa mujibu wa Kanuni ya 2 (2) (b), viongozi na wagombea
hawatakiwi kutumia lugha za matusi wala kejeli za namna yoyote wala
udhalilishaji wa namna yoyote.
Katika rufaa yao, warufaniwa hao walidai kuwa Jaji
Rwakibalira alikosea katika hukumu yake kwa kuchanganya vituo
vilivyotolewa ushahidi na mashahidi wanne na hatimaye akakataa ushahidi
mmojawapo, pamoja na tarehe za ratiba ya kampeni za CCM na Chadema.
Pia walidai Jaji alikosea kwa kuamua kuwa hata
kama Lema kwenye kampeni zake alidai kuwa Dk Burian ni mkazi wa
Zanzibar, na hatafaa kwa hiyo ukazi si sifa ya kuchaguliwa kuwa mbunge.
No comments:
Post a Comment