Makamu Mwenyekiti wa chadema Taifa, Said Arfi
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
kimezidi kuandamwa na migogoro baada ya jana kuibuka mwingine mkubwa
katika kikao chake cha ndani mkoani Katavi kiasi cha kumfanya Makamu
Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Said Arfi, kutupa kadi yake ya
uanachama.
Huu ni mgogoro wa pili mkubwa kuripotiwa
katika kipindi cha juma moja lililopita baada ya ule wa wilayani Karatu
ambako pamoja na mambo mengine uliishia kwa Kamati Kuu kuusimamisha
uongozi wote wa chama hicho wilaya.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili jana
zimeeleza kuwa Arfi ambaye ni Mbunge wa Mpanda Mjini, alitishia kujitoa
Chadema jana, katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya chama hicho Mikoa ya
Katavi na Rukwa kilichoketi Namanyere, Nkasi na kufikia uamuzi wa
kumsimamisha Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Mkoa wa Rukwa, Laurent
Mangweshi.
Katika kikao hicho, Arfi anadaiwa kuichukua
kadi yake ya Chadema na kumtupia Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Rukwa,
John Mallack akitangaza kuachia nyadhifa zote alizonazo, kisha kuondoka
ukumbini, kabla ya kufuatwa na wazee wa chama hicho na kumsihi aichukue
kadi yake hiyo.
Alifikia hatua hiyo baada ya kutokea
sintofahamu kati ya wajumbe wa kikao hicho katika uamuzi huo uliofikiwa
kwa kupiga kura za ndiyo na hapana.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya
kikao hicho vilifafanua kuwa Arfi alikerwa na kauli iliyotolewa na
Mangweshi kuwa katika Uchaguzi Mkuu uliopita, alipokea rushwa kutoka kwa
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Vyanzo hivyo vya habari vimeeleza kuwa
kutokana na hali hiyo, Arfi alipandwa na hasira na kuamua kumrushia kadi
Mallack kisha kutoka nje ya ukumbi.
“Hatua hiyo ilifanya wajumbe wa kikao hicho
nao kutoka nje ya ukumbi na kuanza kumbembeleza ili asichukue uamuzi huo
na kisha wakamwekea kadi yake ya uanachama katika mfuko wake wa shati,”
alisema mmoja wa makada hao.
Arfi mwenyewe hakupatikana jana kuzungumzia
tukio hilo baada ya simu ya mkononi kuita muda wote bila kupokewa na
hata alipotumiwa ujumbe, hakujibu.
Mallack akizungumza na gazeti hili kwa simu
alikiri Arfi kurusha kadi mezani kisha kutoka nje ya ukumbi, lakini
akasema suala hilo lilishughulikiwa na wazee na kumalizwa.
“Ni kweli
unajua huyu ni Makamu Mwenyekiti wetu wa Taifa, sasa inapotokea vijana
wadogo wakamtuhumu kwa tuhuma za uongo na ambazo hazipo inatia hasira,
ndiyo maana huyo kijana tumemvua uongozi,” alisema Mallack.
Tuhuma za Mangweshi
Mangweshi
alisimamishwa uongozi baada ya kutuhumiwa kwa mambo mbalimbali ya
kiutendaji ndani ya chama hicho ikiwamo kumkashifu Arfi.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari,
Mallack alisema kuwa Magweshi amevuliwa uongozi baada ya chama hicho
kujiridhisha kuwa alitenda makosa hayo.
Alisema kamati ya ushauri
ilimwita ili kujibu tuhuma mbalimbali zilizokuwa zikimkabili ikiwamo
kutoa taarifa zisizo rasmi bila kufuata taratibu za chama.
“Pia amepatikana na hatia ya kuandika barua za
kashfa na kuzipeleka makao makuu ya chama kumkashifu Arfi pamoja na
viongozi wengine wa chama akiwamo Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa.
Katibu Mwenezi wa Chadema Mikoa ya Rukwa na
Katavi, John Matongo alisema kabla ya kupewa adhabu ya kusimamishwa,
amewahi kuonywa mara kadhaa lakini ameshindwa kujirekebisha.“Hali hiyo ya mwenyekiti ingeachwa iendelee, ingeweza kuleta mgawanyiko na uchonganishi kwa viongozi wa kitaifa,” alisema.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa kikao hicho
hakikuendeshwa kwa amani baada ya pande mbili zinazovutana kutofautiana
waziwazi kuhusu uamuzi wa kumsimamisha mwenyekiti huyo kiasi cha
kulazimu hatua hiyo ifikiwe kwa kupiga kura.
Kura hizo zilipigwa na wajumbe 36 na matokeo yakaonyesha kuwa 24 waliafiki uamuzi huo na 12 kuukataa.
Akizungumza na mwandishi wetu, Magweshi alisema “Sina taarifa yoyote juu ya tukio hilo kwani sina barua rasmi.”
Alipoulizwa kama alishiriki kikao hicho, alikubali na kusema kilikuwa kikijadili mambo mbalimbali ya chama hicho.
Tanga nako si shwari
Uongozi
wa Chadema mkoani Tanga umeapa kumshughulikia Katibu wa Baraza la
Vijana mkoani hapa, (Bavicha), Deogratias Kisandu kwa kile kilichoelezwa
kuwa ni utovu wa nidhamu.
Akizungumza na waandishi wa habari, katibu wa
chama hicho Mkoa wa Tanga, Saidi Mbwete alisema kitendo cha Katibu huyo
kumtaka Dk Slaa ajiuzulu kwa kumiliki kadi ya CCM ni utovu wa nidhamu.
“Kurudisha kadi ya chama cha awali, ni hiari
ya mwenye kumiliki kadi hiyo kwani ni yake kwa sababu ameinunua na
kuilipia,” alisema Mbwete.
Mgogoro wa Karatu
Wakati hayo
yakiendelea mgogoro wa Wilaya ya Karatu, umechukua sura mpya baada ya
wajumbe wa Kamati ya Utendaji Wilaya hiyo kugoma kujiuzulu kwa maelezo
kuwa Kamati Kuu ya Chadema haina mamlaka ya kuwaondoa.
Wakati viongozi hao wakitoa tamko hilo jana,
tayari Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa Chadema, Benson Kigaila
ametua Karatu jana, kufanya maandalizi ya mikutano ya Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe kuanzia Jumamosi hadi Jumapili ili kukutana na
viongozi wa chama hicho wadau wake katika kile kinachoelezwa kuweka
“mambo sawa.”
Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Karatu, Moshi
Darabe na Mbunge wa Karatu, Mchungaji Israel Natse walisema jana kwamba
wamesikitishwa na uamuzi ya kamati kuu ya kutangaza kusimamisha kamati
hiyo yenye wajumbe 17 bila kuwasikiliza.
Darabe alisema awali, Kamati ya Utendaji ya
Karatu, ndiyo ilikuwa inawatuhumu baadhi ya viongozi kwa kudhoofisha
chama hicho na kushauri wachukuliwe hatua ambao ni Diwani wa Karatu
Mjini, Jubilate Mnyeye, Katibu wa Wilaya hiyo, Raurence Bortha,
Mwenyekiti wa Bavicha Wilaya, Joseph Mtui na Katibu wake, Melkiori Mao.
“Sasa kamati kuu iliwaita na kuwahoji,
tulitarajia wangetoa uamuzi kuhusiana na tuhuma tulizowapa lakini
kusimamisha kamati nzima tunadhani si sahihi na pia ni ukiukwaji wa
katiba ya chama,” alisema Darabe.
Natse alisema kikatiba, wanaamini kamati ya utendaji inaweza kuwajibishwa na mkutano mkuu wa wilaya na siyo kamati kuu.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema,
John Mnyika alisema jana kuwa kimsingi, uamuzi uliofanyika ni wa
kuisimamisha kamati ya utendaji kufanya kazi na si kuivunja au
kuifukuza.
Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo alisema
wakati huu ambao kamati hiyo imesimamishwa, Kamati Kuu ya chama ndiyo
inayofanya uangalizi wa moja kwa moja kwa Wilaya ya Karatu kupitia mfumo
itakaouweka hadi uamuzi mwingine utakapotolewa.
No comments:
Post a Comment