*Askari mwenzao aanika kilichotokea
Mkuu wa Polisi nchini, Said Mwema
Mapya yameendelea
kuibuka kufuatia madai kuwa vifo vya watu watatu wakiwamo polisi wawili
wilayani hapa vimetokana na askari hao kukusanya kwa nguvu mapato ya
serikali.
Habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zimedai kuwa askari hao wa Kikosi
cha Usalama Barabarani, walikwenda katika kijiji na kata ya Mugoma
kukamata vyombo vya usafiri na watu wanaoendesha bila leseni ili
kuhakikisha wanafikisha kiwango cha makusanyo ya serikali waliyopangiwa
kila mwezi.
Chanzo chetu kimeeleza kuwa Askari wa Usalama Barabarani wanapaswa
kukusanya kiasi kisichopungua Shilingi milioni tatu kila mwezi na hatua
hiyo imekuwa ikiwalazimu kwenda kukamata na kutoza faini mbalimbali
katika maeneo hata yasiyo na usalama kwa maisha yao.
Kikizungumzia tukio la mauaji hayo, chanzo hicho kilidai kuwa kitendo
cha polisi kwenda kukamata pikipiki iliyokuwa ikitengenezwa na mtuhumiwa
huyo ambaye ni fundi jirani na gulio la kijiji hicho, hakikuzingatia
taratibu.
Kwa msingi huo, chanzo hicho kimeeleza kwamba Mkuu wa Kikosi cha Usalama
Barabarani ndiye anayepaswa kuwa mlalamikiwa wa kwanza katika mauaji
hayo.
“Unajua ndugu mwandishi, haiwezekani kwenda kukamata pikipiki za watu
hadi ndani ya gulio...mbaya zaidi unakwenda kukamata na pikipiki
inayotengenezwa kwa fundi. Hakika hapa busara haikutumika hata kidogo,
ndiyo maana mauaji kama haya yametokea,” kilidai chanzo hicho na
kuongeza:
“Pamoja na kwamba Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani kuwa mlalamikiwa
wa kwanza, kwa kiasi kikubwa serikali yetu nayo inachangia maana sisi
askari wa usalama barabarani tunalazimika kuhakikisha tunafikisha
kiwango cha fedha tunazopangiwa kwa kila mwezi na inapotokea tarehe
zinaelekea ukingoni na makusanyo hayajafikia, matokeo yake ndiyo hayo.”
Chanzo hicho kilipingana na taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Philip Kalangi, kwamba askari hao
walikuwa kwenye operesheni maalum ya kukamata watu wasio na leseni na
vyombo vya moto visivyofaa kwa matumizi ya usafirishaji wa abiria.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, taarifa hiyo imechakachuliwa kwa lengo la kukwepesha ukweli wa jambo hilo kujulikana.
“Hakika hapakuwa na operesheni maalum kama Kamanda alivyodai isipokuwa
ni utaratibu wetu wa kawaida kwenda kukusanya mapato ya serikali. Tatizo
hapa ni kutaka kukwepesha ukweli wa mambo. Aidha, yeye mwenyewe au mkuu
wa upelelezi wa wilaya ambaye atakuwa ameamua kuchakachua maelezo ili
kuweka kinga ya kuonekana askari walikuwa kwenye makosa,” kilidai chanzo
hicho.
Hata hivyo, Kamanda Kalangi alipoulizwa jana kuhusiana na taarifa hiyo, alisisitiza kuwa ilikuwa operesheni.
“Mimi ndiye Kamanda, kama kuna anyepinga taarifa nilizozitoa kamuulize huyo huyo,” alisema Kamanda Kalangi.
Alisema kutokana na mauaji hayo, Mkuu wa Polisi nchini, Said Mwema,
ametuma kikosi maalum kutoka makao makuu ya polisi kinachotarajiwa
kuingia mkoani Kagera jana. Hata hivyo, hadi jioni hakikuwa kimewasili.
Alisema kikosi hicho kitaungana na wenzao wa mkoani Kagera kuchunguza
kwa kina mauaji hayo askari hao wawili pamoja na raia mmoja.
WATU 11 WASHIKILIWA
Kadhalika, Kamanda Kalangi alisema mpaka juzi usiku, watu 40 walikuwa
wametiwa mbaroni kufuatia msako mkali wenye lengo la kuwabaini
waliohusika na mauaji hayo.
Bila kuwataja majina yao, alisema baada ya kufanyika upelelezi kwa watu
hao, wengine 29 waliachiwa huru huku 11 wakiendelea kuchunguzwa.
Kamanda Kalangi alisema idadi ya watuhumiwa hao inaweza kupungua au kuongezeka zaidi kwa kuwa upelelezi bado unaendelea.
Polisi waliopoteza maisha katika tukio hilo ni Koplo Paschal na Konstebo
Alexander na raia ni Said Mkonikoni (24), aliyekuwa mkazi wa Kata ya
Mugoma.
Katika tukio hilo ambalo wananchi walilazimika kujichukulia sheria
mkononi kwa kuwaua polisi wawili, pia waliteketeza kwa kukichoma moto
Kituo cha Polisi cha Mugoma na kusababisha nyaraka za serikali,
pikipiki, baiskeli na silaha kuungulia ndani.
Hata hivyo, thamani ya uharibifu huo bado haijafahamika mpaka sasa.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na NIPASHE walidai kuwa hawana amani
kutokana na kamata kamata inayoendelea kufanywa na polisi na kusababisha
baadhi yao kushindwa kwenda kufanya shughuli za uzalishaji mali
wakihofia kutiwa nguvuni.
Hali hiyo imedaiwa kusababisha baadhi ya wananchi kugeuka wakimbizi
baada ya kuvuka mpaka na kuingia nchini Burundi kukwepa kukamtwa na
polisi wanaoendesha msako katika maeneo mbalimbali ya wilayani humu.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment