Maafisa kutoka Marekani
na shirika la kujihami la NATO wanasema jeshi la Syria limekuwa
likifyatua makombora ya masafa mafupi katika vita dhidi ya waasi, huku
mzozo nchini humo ukizidi kuzorota.
Maafisa hao, ambao hawakutaka kutajwa, wanasema
makombora hayo, yanofanana na yale ya Scud, yalifyatuliwa kutoka
Damascus hadi maeneo ya kaskazini yanayodhibitiwa na waasi.
Msemaji mmoja wa Wizara ya Nchi za Kigeni wa Marekani, Victoria Nuland, alisema serikali ya Syria inatumia silaha hatari.
Ingawaje alisema kuwa hatatoa "habari za
kinaganaga kuhusu makombora hayo", alithibitisha kwamba "hivi majuzi
ufyatuliaji wa makombora ulikuwa umeonekana".
Upinzani
Bi Nuland alisema: "Vile serikali hiyo
inavyozidi kukata tamaa ndivyo tunavyoshuhudia kuongezeka kwa visa vya
ukatili na kutumika kwa silaha kali zaidi."
Msemaji wa White House Jay Carney alisema iwapo
taarifa kusuhu urushaji wa Scud ni za kweli basi "hili ndilo tukio la
hivi karibuni kutoka serikali inayokata tamaa, na ambayo imepuuza
umuhimu wa maisha ya binadamu na wa wananchi wake".
Jumatano, zaidi ya nchi 100 chini ya jina
Marafiki wa Syria, zilikutana nchini Morocco na kukubali kutambua
upinzani wa National Coalition for Syrian Revolutionary and Opposition
Force, kiwe chama pekee kitakachowakilisha wananchi wa Syria.
No comments:
Post a Comment