Walowezi wa kiyahudi wanaoishi katika Ukingo wa Magharibi
Katibu mkuu wa
Umoja wa mataifa, Ban Ki Moon, ameonya kuwa mpango wa Israeli wa ujenzi
wa makao mapya ya walowezi utakuwa na athari mbaya kwa nafasi ya
kupatikana amani na Palestina.
Israeli inasema inapanga kuongeza nyumba elfu
tatu kwa makaazi yaliopo tayari na inatarajia kuongeza makaazi mapya
kuunganisha yale yaliopo katika ukingo wa Magharibi na Jerusalem
Mashariki.
Ilitangaza mpango huo kufuatia kura
iliyopigwa katika Umoja wa mataifa iliyoipandisha Palestina hadhi kuwa
dola muangalizi katika umoja huo.
Hapo jana kiongozi wa Palestina Mahmoud Abbas
alipokewa kwa shangwe mjini Ramallah katika ukingo wa Magharibi
aliporudi nyumbani kutoka kwenye mkutano huo.
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ameahidi kuendelea na mpango wake wa ujenzi.
Katika taarifa yake Jumapili, Bwana Ban
alielezea wasiwasi mkubwa kuhusu mpango ulioidhinishwa wa nyumba mpya
elfu tatu zinazotarajiwa kujengwa Mashariki mwa Jerusalem na katika
ukingo wa Magharibi.
Lakini alisisitiza kuwa mpango wowote wa kujenga makaazi katika sehemu inayojulikana kama E1, kati ya Jerusalem
na makaazi yaliyoko Ukingo wa Magharibi ya Maaleh Adumim, lazima
usitishwe. "Hatua hii itakuwa pigo kubwa kwa fursa iliyopo ya mazungumzo
ya amani'' alisema bwana Ban.
Marekani ilisema kuwa mpango huo hausaidii
chochote bali utaathiri hatua zilizofikiwa za amani. Naye Mkuu wa sera
katika Muungano wa Ulaya Catherene Ashton, alielezea wasiwasi kuhusu
mpango wa ujenzi wa makaazi mengine ya walowezi.
No comments:
Post a Comment