Aliyekamatwa na pembe za ndovu ni askari wetu - JWTZ
Pembe za ndovu.
JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),
limesema kwamba mwanajeshi aliyekamatwa juzi katika tukio la ujangili
mkoani Arusha ni askari wake.
Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe jana
alimtaja askari huyo kuwa ni mwenye namba MT 59509 Sajenti, Azizi
Athuman Yusufu ambaye alisema ni askari wa jeshi hilo na alikuwa dereva
wa mkufunzi wa kijeshi kutoka Zimbabwe anayefundisha hapa nchini.
Hata hivyo Kanali Mgawe alisema mkufunzi huyo
wa kijeshi, hakuwapo wakati wa tukio hilo. “Kweli huyo ni askari wetu.
Alikuwa anamwendesha mkufunzi wa kijeshi kutoka Zimbabwe. Siku hiyo
alimrudisha nyumbani kwake saa saba mchana na kwenda kupaki gari. Lakini
baadaye saa moja usiku, alikwenda kulichukua gari hilo na kutokomea
nalo kusikojulikana hadi alipokutwa katika tukio hilo,” alisema Kanali
Mgawe.
Wakati JWTZ likitoa taarifa hiyo, Polisi
mkoani Arusha jana lilieleza jinsi askari huyo alivyokamatwa. Hata hivyo
namba ya askari huyo ilitofautiana na namba ya askari ikimtaja kuwa ni
mwenye namba MT 59503.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus
Sabas alisema askari huyo alikamatwa saa 5:00 usiku wa Januari 20 mwaka
huu. Alikutwa na pembe mbili za ndovu na bunduki moja aina ya Riffle
yenye namba 458.
“Tunaamini bunduki hiyo ndiyo iliyotumika kwenye uwindaji huo haramu,” alisema.
Kamanda
Sabas alidai kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa na wenzake zaidi ya wawili
ambao walikimbia wakati mwenzao huyo anakamatwa eneo la Manyara Kibaoni
Wilaya ya Karatu mkoani Arusha.
“Gari lililohusika kwenye uhalifu huu
limethibitika kuwa ni mali ya JWTZ na uchunguzi unaendelea kujua namna
gani wahusika walifanikiwa kuondoka nalo kambini na kwenda kulitumia
kwenye uhalifu huo,” alisema Sabas.
Awali, habari kutoka eneo la tukio zimeeleza
kuwa gari hilo lilikuwa na zaidi ya abiria watatu ambao mara baada ya
matairi mawili kupasuka, moja la mbele kulia na jingine la nyuma kushoto
watu wawili waliteremka na kutokomea porini na mizigo isiyojulikana.
Ilidaiwa kuwa baada ya wananchi kufika kwa nia
ya kutoa msaada kwa majeruhi, mtuhumiwa aliyekutwa akiwa amevaa jaketi
la JWTZ na suruali ya jinsi pamoja na bunduki, aliwahakikishia wananchi
waliotaka kuwakimbiza watu hao wakidhani wamemwibia wasishughulike nao
kwa kuwa hajaibiwa chochote.
Baada ya wananchi na askari wa jeshi la polisi
waliofika kumtilia shaka mtuhumiwa, msako ulifanyika kuelekea
walikokimbilia abiria hao garini na mizigo, lakini hawakuonekana.
No comments:
Post a Comment