MTU aliyepiga picha na Mbunge wa Arusha mjini,
Godbless Lema akiwa amevalia sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ), amehukumiwa kifungo cha miaka minne jela.
Abubakari Kikulu (29), alipiga picha na mbunge
huyo Desemba 23 mwaka jana, baada ya Lema kumaliza kuhutubia mkutano wa
hadhara eneo la Mererani, ikiwa ni sehemu ya mikutano aliyoifanya
kutokana na Mahakama ya Rufani Tanzania kumrejeshea ubunge wake.
Mbali na kupiga picha hiyo na Lema pamoja na
Mbunge wa Arumeru Mashariki Joshua Nassari, kijana huyo alionekana
katika picha hiyo akionyesha vidole viwili, ambayo ni alama ya Chadema.
Hata hivyo, baada ya picha hiyo, JWTZ
lilimtilia shaka kijana huyo na kutangaza rasmi kumsaka, ili
lijiridhishe kama ni mmoja wa wanajeshi wake.
Baada ya kumsaka kwa
takriban siku 12, kijana huyo alikamatwa Januari 13, katika Mji wa
Bomang’ombe wilayani Hai na baada ya kupekuliwa alikutwa na sare hizo.
Jana, Kikulu alifikishwa mahakamani mjini
Moshi, akiwa chini ya ulinzi wa polisi na kusomewa mashtaka mawili,
ambayo yote alikiri kuyafanya kama ilivyodaiwa mahakamani.
Baada ya
kukiri kosa hilo Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa
Kilimanjaro, alimhukumu kifungo cha miaka minne jela, ili iwe fundisho
wa wakosaji wengine wa aina hiyo.
Kabla ya hukumu hiyo, Wakili wa
Serikali, Ignas Mwinuka alimsomea mshtakiwa huyo mashitaka yake mawili,
likiwamo la kujifanya Ofisa wa Jeshi, wakati akijua ni uongo.
Wakili
huyo alidai mahakamani kuwa Januari 3, mwaka huu katika eneo la
Bomang’ombe wilayani Hai, mtuhumiwa huyo alijitambulisha kama mtumishi
wa umma.
Katika shtaka la pili, wakili huyo alidai siku
hiyo hiyo katika Mtaa wa Msikitini, eneo hilo la Bomang’ombe, mtuhumiwa
alipatikana na sare za JWTZ kinyume cha sheria.
Sare hizo ni pamoja na suruali moja, mashati
mawili na kofia mbili, vyote vikiwa na alama za Jeshi la Wananchi wa
Tanzania la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Baada ya
Hakimu Kobelo kumuuliza mshtakiwa kama ni kweli alitenda makosa
anayoshitakiwa, mshtakiwa huyo alikiri makosa yake katika hali ambayo
haikutarajiwa.
Kutokana na kukiri kwake makosa hayo, Hakimu
Kobelo alimhukumu kifungo cha miaka miwili kwa kosa la kwanza la
kujifanya Ofisa wa JWTZ na miaka mingine miwili kwa kosa la pili.
Hata
hivyo, Hakimu Kobelo alisema kuwa kwa kuwa adhabu hizo zinakwenda kwa
pamoja (concurrent), mshtakiwa huyo atatumikia kifungo cha miaka miwili
jela.
Kwa mujibu wa hakimu huyo, kosa alilolifanya
mtuhumiwa huyo ni baya na linastahili adhabu kali, ili iwe fundisho kwa
watu wengine wanaotumia vibaya sare za majeshi nchini.
No comments:
Post a Comment