'Askari' aliyepiga picha na Lema anaswa

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz.

Hatimaye makachero wa Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro wamemnasa mtu aliyedai kuwa ni mwanajeshi na kupiga picha na Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, Jeshi hilo kwa kushirikiana na  JWTZ, walimkamata mtu huyo aliyejulikana kwa jina la ‘Kamanda’ wilayani Hai akiwa na sare mbili za polisi.

Mtuhumiwa huyo katika tukio hilo alipiga picha na Lema pamoja na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema), wakati wa kumkaribisha Lema mkoani Arusha baada ya kushinda rufaa ya uchaguzi.. Habari za kuaminika zilizofikia NIPASHE na kuthibitishwa na Kamanda Boaz zimeeleza kuwa mtu huyo amekamatiwa wilayani Hai jana akiwa na sare mbili za jeshi la polisi. 

Taarifa za ndani zimeeleza kuwa kukamatwa kwa mtu huyo kumetokana na juhudi za Kamanda wa Makosa ya Jinai mkoani hapa, Ramadhani Nn’azi, kuweka mtego wa kiintelijensia baada ya kuwakamata marafiki wa mtu huyo anayejulikana kwa jina la ‘kamanda’ katika mji wa Mererani.

“Ni kweli tunamshikilia mtu huyu…aliyepiga picha na wabunge wa Chadema akiwa na sare mbili za jeshi ila hatuwezi kutoa taarifa kwa sasa kwa kuwa kuna uchunguzi unaendelea,” alisema Kamanda Boaz Taarifa zilizozagaa katika mji wa Moshi zinaeleza kuwa mtu huyo ni mwanajeshi ila jeshi la wananchi limemkataa kwakuwa ameonyesha ushabiki kwa Chadema jambo ambalo ni hatari kwa nchi.

Hata hivyo, kamanda Boaz alipinga taarifa hizo akidai sio za kweli na kuwa taarifa zaidi zitatolewa. Awali baada ya kuchapishwa kwa picha za mtu huyo aliyedai ni mwanajeshi kutoka Monduli, JWTZ lilitoa taarifa likieleza kushtushwa na tukio hilo na kusema kwamba linamtafuta mtu huyo kwa udi na uvumba ili kujiridhisha kama kweli ni askari wake. 

Mbali ya taarifa hiyo, Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe alisema endapo itabainika kuwa aliyevaa sare hizo ni mwanajeshi, moja ya hatua dhidi yake ni kufukuzwa kazi mara moja.

Mbali na hatua hiyo, Kanali Mgawe alisema kuanzia sasa, Jeshi limepiga marufuku mtu yeyote kuvaa sare zake katika mikutano yote ya siasa na atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kinidhamu.

Kuhusu kitendo cha askari huyo kupiga picha na Lema, Kanali Mgawe alisema moja ya masharti muhimu ya askari anapiojiunga na jeshi ni kutambua na kutii sheria inayomzuia kujihusisha na masuala ya siasa na kwamba kitendo cha mtu huyo kimemshangaza na kumfanya amtilie shaka kama kweli ni askari aliyekamilika.

No comments:

Post a Comment