Mkulo: Sababu zilizonifanya nistaafu ubunge hizi hapa
Mbunge wa Kilosa (CCM), Mustafa Mkulo
Mbunge wa Kilosa (CCM), Mustafa Mkulo ameeleza sababu zilizomfanya kutangaza kustaafu ubunge mwaka 2015.
Mkulo ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Fedha katika Serikali ya Awamu
ya Nne alisema umri aliofikia unamlazimisha kustaafu masuala ya ubunge.
Mkulo aliliambia gazeti hili jana kuwa pamoja na uamuzi wake huo
pia changamoto za vijana zilizopo bungeni nazo ni ishara tosha ya yeye
kuachia ngazi.
Alisema bunge kwa sasa idadi kubwa ni ya vijana, hivyo kwa umri
wake ameonelea kuwaachia kuchukua nafasi yao, ingawa alisema uamuzi wake
haumaanishi wazee wasiendelea kuwania nafasi hiyo.
Mkulo ambaye Septemba 26 mwaka jana alitimiza umri wa miaka 66,
alianza ubunge 2005 na hadi kufikia mwaka 2015 amehudumu nafasi hiyo kwa
vipindi viwili.
“Vipindi viwili vinanitosha sana kwa upande wa ubunge,” alisema
nakuongeza kuwa, amekuwa serikalini tangu akiwa na umri wa miaka 25,
hivyo kama ni kutumikia wananchi amewatumikia ipasavyo.
Mkulo mwenye shahada ya uzamili kwenye masuala ya fedha aliyoipata
kwenye Chuo Kikuu cha SouthWest, London, Uingereza kati ya mwaka 1975 na
1977, alishika nyadhifa mbalimbali serikali.
Miongoni mwa hizo ni Naibu Waziri wa Fedha alioupata 2006 hadi 2008
alipoteuliwa kushika uwaziri kamili wa wizara hiyo lakini mapema mwaka
jana alienguliwa kwenye wadhifa huo kutokana na tuhuma mbalimbali.
Azma ya Mkulo ya kutogombea tena nafasi hiyo kwa mara ya kwanza
aliitangaza Machi, 2011 na kisha kurudia kutangaza nia yake hiyo
mwishoni mwa mwaka jana.
Wakati akitangaza kwa mara ya pili, Mkulo alisema kwa kuwa sasa
bado ni mbunge hadi 2015, ataendelea kutekeleza ahadi zake na kuwasaidia
wananchi wa jimbo hilo kama alivyowaahidi.
Hatua ya kutangaza kwa mara ya pili ya kutogombea ubunge, ilikuwa
ni kujibu tetesi zilizokuwa zikienea kuwa kutokana na uamuzi huo,
hatatoa msaada wowote kwa wananchi wake waliomchagua.
Kwa mujibu wa Mkulo, amefikia uamuzi huo kwa hiari yake na kupata
ridhaa ya familia yake na kwamba ataendelea kubaki kuwa kada wa CCM
akitoa ushirikiano wa hali na mali kwa chama chake na hata kwa mgombea
wa nafasi ya ubunge wa jimbo hilo atakayechaguliwa mwaka 2015.
No comments:
Post a Comment