Kikundi cha Jumuiya ya wanafunzi nchini India wakiwa wameshika mabango
wakati wa maandamano ya kupinga vitendo vya ukatili likiwamo kitendo cha
ubakaji kilichofanywa kwa mwanamke aliyefariki. Picha na AFP
NEW DELHI, India
BABA wa binti aliyefariki
dunia baada ya kubakwa na kuteswa amesema kuwa anataka jina la binti
yake litajwe hadharani ili afahamike na kuwa mfano kwa waathirika
wengine wa vitendo vya ubakaji.
Mzazi huyo amesema hayo katika mahojiano
yaliyochapishwa leo na gazeti moja la Uingereza, ambapo alisema anaona
kwamba ni sahihi kwa dunia kujua jina halisi ya binti huyo.
Baba huyo
aliliambia gazeti hilo la Sunday People kuwa binti yake hakuwa na kosa
na alikufa wakati akijaribu kujihami na yeye kama mzazi anajivunia
mwanaye huyo kwa ushujaa wake.
“Binti yangu hakufanya jambo lolote baya, alikufa
wakati alipokuwa akijaribu kujitetea. Ninajivunia ujasiri wake. Kulitaja
wazi jina lake kutawapa ujasiri wanawake wengine ambao wamewahi
kukumbwa na matukio kama haya. Watapata ujasiri mpya kupitia kwa binti
yangu,” alisema baba huyo.
Anasema kutajwa jina la mwanawe kutawapa
moyo wanawake wengine waliobakwa na kufanikiwa kubaki hai na kuwapa
nguvu ya kusonga mbele na maisha. Sheria za India zinazuia kujulikana
hadharani kwa waathirika wa visa vya ubakaji.
Kauli ya baba huyo
inakwenda sambamba na ombi la mmoja wa mawaziri nchini humo, Shashi
Tharoor ambaye alisema kwamba ni vyema jina la binti huyo likitajwa
hadharani ili litumike kaka chanzo katika kutunga sheria mpya dhidi ya
wabakaji.
Wiki iliyopita, Tharoor ambaye ni Waziri mdogo wa Elimu
alizitaka mamlaka zinazohusika kuliweka wazi jina la binti huyo ili
kutoa fursa kwa sheria mpya kumtumia kama mfano wa waathirika wa ubakaji
unaofanywa kwa makundi nchini humo.
“Labda tu kama wazazi wake
watazuia, lakini atapewa heshima na kutumiwa kama chanzo cha sheria mpya
dhidi ya wabakaji. Huyu alikuwa binadamu mwenye jina, hakuwa alama ya
ishara,” alisema.
Binti huyo aliyekuwa na umri wa miaka 23 alifariki
dunia akipatiwa matibabu nchini Singapore baada ya kuvamiwa, kubakwa na
kuumizwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake akiwa mjini New Delhi,
India.
Sheria hizo zina lengo la kumsitiri mwathirika na kumuwepusha
na usumbufu wa vyombo vya habari hasa ndani ya taifa hilo ambapo
unyanyapaa dhidi ya watu waliobakwa ni mkubwa sana.
Baba mzazi wa
binti huyo aliliambia pia shirika la habari la Reuters kuwa hana
pingamizi lolote kwa vyombo vya habari kulitaja na kulitumia jina la
mwanawe katika mikasa ya ubakaji.
No comments:
Post a Comment