MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbles Lema
MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbles Lema wa Chadema,
anatarajia kuhutubia mkutano mkubwa mjini Dodoma baada ya kupokewa kwa
maandamano yanayotarajia kuanzia Ihumwa kilomita 14 kutoka Dodoma Mjini.
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari
na kusainiwa na Katibu wa Chadema Wilaya ya Dodoma mjini, Jella Mambo,
ilieleza kuwa msafara wa Lema utaanzia katika Kijiji cha Ihumwa ikiwa ni
safari yake kuja bungeni.
Lema ataingia Dodoma na kutinga bungeni baada
ya kushindwa kushiriki mikutano mitatu ya Bunge baada ya kuvuliwa ubunge
wake na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Aprili 5, mwaka jana.
Hata hivyo, Desemba 21 mwaka jana, mbunge huyo
machachari alirudishiwa ubunge wake baada ya jopo la majaji kuridhika
na sababu za rufaa yake na kumpa ushindi kuwa ni mbunge halali za Jimbo
la Arusha Mjini.
Mambo alisema jana kuwa mapokezi ya Lema
yatakuwa ni makubwa kuliko mapokezi yoyote ambayo yamewahi kufanyika
katika Mji wa Dodoma na kuwa yataongozwa na msafara wa mapikipiki,
magari pamoja na msururu mrefu wa watu.
Katibu huyo alisema kuwa mara baada ya kuingia
mjini Dodoma, msafara wa Lema utakwenda moja kwa moja Ofisi za Chadema
mkoa ambako mbunge huyo pamoja na msafara wake watakwenda kusaini kitabu
cha wageni.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, mara baada ya
kusaini kitabu msafara huo utakwenda katika Viwanja vya Shule ya
Sekondari ya Central ambako hakutakuwa na jambo lolote litakalofanyika
zaidi ya utambulisho na kisha mbunge huyo kupewa nafasi ya kuhutubia
mkutano wa hadhara utakaoanza saa 10 jioni.
Kwa muda wa wiki sasa viongozi wa Chadema wa ngazi ya mkoa na wilaya wamekuwa wakihaha kwa kufanya maandalizi ya mkutano huo.
No comments:
Post a Comment